Habari

Julius Nyaisangah kuzikwa Tarime, Mike Mhagama akumbuka jinsi alivyokuwa mjuzi na kiongozi bora

Mwili wa aliyekuwa mtangazaji mkongwe nchini na meneja wa Abood Media, Julius Nyaisangah unasafirishwa leo kwenda kwao wilayani Tarime mkoano Mara kwa mazishi. Nyaisangah alifariki jana akiwa mjini Morogoro kwa ugonjwa wa Kisukari.

424976_333927119973228_1272853026_n

Mtangazaji wa zamani wa Radio One, Mike Mhagama ni miongoni mwa watu wengi waliokipokea kifo cha Julius Nyaisangah..

1392910_10151904421099330_2044904326_n
Mike Mhagama na marehemu Nyaisangah

Kama ilivyokuwa kwa watangazaji wengi wa enzi hizo, Mike Mhagama aliyekuwa maarufu kwenye kipindi cha DJ Show alivutiwa kuingia kwenye fani hiyo baada ya kumsikiliza.

Mike ameandika kwenye ukurasa wa Facebook:

“Nilipokuwa mdogo nilisikiliza sana Radio na Kipindi cha kwanza kuwa na mapenzi nacho kilikuwa “Disco Show” cha RTD kikiendeshwa na Uncle Julius Nyaisangah nilipenda kuwa kama yeye nikiwa mkubwa. Nilivutiwa na usomi wake wa habari,uendeshi wake wa vipindi “Live” kama wakati ule akifungua Club ya usiku ya Bilicanas kwa matangazo “live” kutoka Mtaa wa Mkwepu.Umahiri aliokuwa nao haupingiki na alikuwa mkomavu mno katika taaluma.

Nilipoomba kazi Radio One alikuwa kati ya wakongwe walionifanyia usaili.Alifurahishwa na usaili ule na alinipa alama “A”.Alikuwa si mchoyo wa kile anachokifahamu katika taaluma.Aliwahi kuniuliza kipindi fulani kama nitauweza “umaarufu” maana una karaha zake.Alikuwa mcheshi na daima alikuwa akipenda kampani yetu kwenda kula supu au kukamata mbili tatu huku akituusia mengi kuhusu taaluma hii.

Alinisimamia katika utayarishi wa vipindi vile vya OB (Club Billicanas au Sabasaba) ambacho kilikuwa kikienda “live” tena kutoka Club Billicanas zamu hii kupitia Radio One na miye kuwa mwendeshi wake mkuu katika kipindi hiki chini ya usaidizi wa Monica Mfumia.Uncle alikuwa mwingi wa Tabasamu hata akiwa amechukia na alikuwa muwazi kwako kama umemkera.

Mwaka 2007 nilipokwenda kumtaarifu ofisini kwake Radio One kuwa namkaribisha katika harusi yangu,alifurahi sana lakini pia alisikitika sana na kusema hatoweza kuhudhuria kutokana na safari ya kikazi Afrika Kusini aliyokuwa aende na Mwenyekiti Mzee Mengi lakini alikuwa nami mpaka siku mbili kabla ya harusi kuhakikisha ananisaidia katika lolote analoweza.Na ndipo pia akanikabidhi kopi ya picha yenye timu nzima ya Radio One kama zawadi nikumbuke tulikotoka.Picha hii ndiyo inayozungushwa kwenye mtandao mpaka leo hii ikiwa kwa mara ya kwanza watu kutambua kikosi halisi cha kwanza cha Radio One.Picha hii ina sahihi yake upande wa kulia chini.Uncle hakupenda makuu!

Alipokuwa na udhuru “aliniomba” nimsaidie kusoma taarifa za habari hasa za saa mbili usiku ambazo mara nyingi alipangiwa yeye makusudi hasa ukizingatia zilitaka mtu mwenye “Commanding Voice” kama yeye kutokana na kusikilizwa na “wakuu” wengi.Kwa mtu wa wadhifa wake (alikuwa mkuu wangu wa kazi) kamwe isingekuwa lazima “kuniomba” bali “angenipanga” tu kusoma habari!Uncle alipenda usawa! Kuna siku niliwahi kumnung’unukia kwa nini napangwa vipindi vingi kuliko wengine,alicheka na kusema Mike kuna sababu ni kwa nini,wewe fanya tunachokuomba ufanye halafu utaniambia miaka 20 toka sasa faida yake!Alikuwa mwalimu tosha katika fani!

Uncle ni kati ya wanataaluma wachache walionivutia kuingia katika taaluma hii kutokana na uwezo walionao katika kucheza na lugha na namna wanavyofanya kazi,bila yeye na wengine wachache pengine ningekuwa aidha mwanasheria au mwanadiplomasia taaluma ambazo kwangu zilikuwa mbadala!

Daima Uncle tutakukumbuka,umetuachia ukiwa lakini kazi ya Mungu Daima haina makosa.Umetangulia nasi tunafuata.Kama asemavyo rafiki yako mkubwa Charles Hilary…Areee mmang’ana tutaonana na pumzika kwa Amani! We Will Miss You Dearly.”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents