Bongo5 Makala

Miaka 10 ya THT: Ilikuwa ni safari yenye misukosuko na mafanikio makubwa sana – Ruge (Video)

Tanzania House of Talent, THT, inaadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake. Kilele cha maadhimisho hayo ni Jumamosi hii pale Escape One.
Kwa mujibu wa mwanzilishi wa THT, Ruge Mutahaba, safari ya miaka 10 ya taasisi hiyo haikuwa rahisi hata kidogo.

“Ni safari yenye misukosuko zaidi,” Ruge ameiambia Bongo5. “Lakini kwa jicho la mwanzishaji safari, ni safari yenye mafanikio makubwa sana. Kwa jicho la nje unaweza ukaiona kama ni safari ya kwenye mawimbi makali.”

Ruge anasema wazo la kuanzisha THT miaka 10 iliyopita lililianzishwa kwa ushirikiano wake na aliyewahi kuwa mtangazaji wa Clouds FM, Sebastian Ndege ambaye kupitia kipindi chake cha Njia Panda, vijana wengi walikuwa wakimuomba msaada wa kwenda kurekodi nyimbo zao studio.

“Kwahiyo akawa anatoa hela wanarekodi, na mimi vile vile nafuatwa na watu naombwa unawapa hela ya kwenda tu studio. Tukagundua kwamba kila unayemrekodi baada ya miezi mitatu anarudi tena anataka kurekodi wimbo mwingine. Tukagundua kwamba kuna tatizo. Kwanini tusikatae kuanza kutoa hizi hela, tuanzishe kama system ya chuo ambako mtu anayetaka kupata hela ya studio lazima apite kwenye darasa fulani,” amesema.

Baada ya wazo hilo kupita, anasema waliamua kuanza na vijana wanaoishi katika mazingira magumu ambapo baadhi ya vijana wa mwanzo walikuwa ni wale waliokuwa wakilala kwenye maeneo ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

“Lakini hata mwaka haukipita, tukagundua kwamba inawezekana tunakosea. Ukiwaweka watu ambao wote wanahitaji msaada, hakuna anayejisukuma. Kila mtu atakuwa anaishi maisha ya kusubiri msaada. Na hata THT ilipoanza ikaanza katika mtazamo huo. Watu wakafikiri kwamba hii ni sehemu ambayo inabidi ulete sabuni, ulete nguo. Kwahiyo tukaona kwamba tupafungue waanze kuja watu wote ilimradi una kipaji.”

Mwasiti alikuwa mmoja wa wasanii walioingia THT mwanzoni kabisa japo hakuwa akiishi katika mazingira magumu kama wengine ingawa alikuwa na kipaji kikubwa.

Kwa upande wa Barnaba, muimbaji ambaye leo hii anasifiwa kuwa miongoni mwa watunzi bora wa nyimbo nchini alikataliwa kuingia THT kwa mara ya kwanza.

“Alikataliwa na Mwasiti wakati anafanya interview. Wakati mimi naingia jioni nakutana na Barnaba akiwa mdogo sana wa miaka 16, machachari kwelikweli. Nikasema ‘huyu jamaa vipi’ wakasema huyu amekuja bado mdogo’ nikasema ‘no huyu mwacheni akulie hapa hapa,” anakumbushia Ruge.

Msanii mwingine aliyekataliwa kuingia THT enzi hizo alikuwa ni Diamond Platnumz.

“Nakumbuka Nash (Designer) ambaye wakati huo ni sehemu ya mwanafunzi, yeye alimkatalia Diamond kwenye interview. Kwahiyo mimi kwangu naviona kama changamoto sana mwanzoni kwasababu sisi wenyewe tunajifunza lakini inabidi ufanye kazi ya kufanya maamuzi ya kuwa huyu anaweza huyu hawezi.”

Ilichukua takriban miaka mitatu wazo la awali la THT likaanza kupevuka na kuonesha dalili za kuzaa matunda. Ni katika muda huo ndipo walipoanza kufikiria kuondoka kutoka kwenye kuwa sehemu kama ya watu kujifunza na kutengeneza mazingira ya wasanii kufanya show ili mradi uweze kujiendesha wenyewe bila kuendelea kutumia fedha zao za mfukoni.

Safari haikuwa rahisi kiasi ambacho kuna wakati alitaka kukata tamaa ya kuendelea na THT kutokana na sababu mbalimbali.

“Mimi muda wangu mwingi nipo Clouds, kwanza kukatokea ile hali ya kutooeleweka. Kukatokea kama mtazamo kwamba THT ni kama kitengo cha Clouds. Kwahiyo hata vijana unaotaka kuwasaidia, ukipeleka nyimbo kwenye sehemu nyingine wanaanza kupata ugumu. Kwahiyo tukawa tunawaza kwamba hiki tunachokifanya pia hakina maana kama hakiwasaidii sana sana kinawaumiza vijana.”

Ndipo hapo walipofikiria kutafuta mtu ambaye angeweza kuisimamia full time ambapo walipata volunteer wa Uingereza aitwaye Rebecca.

“Yeye ndio akaanza kufanya kazi ya kutafuta wadhamini, kutafuta professionalism kwenye show, kuanza kuibadilisha sasa THT kuanza kuwa katika mrengo wa biashara.”

Ruge anasema jambo muhimu analojivunia katika miaka 10 ya THT ni ule uwezo wa kutengeneza wasanii wengi wenye uelewa kuwa sanaa ya ubunifu ni biashara.

“Nimejaribu kuondoa ile dhana ya kufikiria kwamba hii ni msaada au hiki kitu unafanya kwasababu unapenda,” anasema.

“Hii ni kitu unafanya kwasababu ni sehemu ya maisha yako na inatakiwa kutengeneza maisha yako.”

“Cha pili ni kutengeneza msingi wa vijana ambao wengi wanaelewa kwamba unaweza ukawa ni msanii mkubwa sana lakini bado nidhamu ni sehemu ya maisha unayotakiwa kuwa nayo.”

Kingine anachojivunia ni kuondoa dhana kuwa THT ni sehemu ya wasanii waliopita au kusoma THT tu.

“Studio hakuna mtu ambaye unaweza kuniambia haji kurekodi. Na sisi hatuchaji THT, tunakuambia kama unaamini wimbo ni nzuri, unaweza kuchangia chochote unachoweza. Kwahiyo tuna watu kama akina Diamond, Ommy, Alikiba tunafanya naye sana kazi kwa mfano anatumia ile bendi THT siku zote akina Linex, Shaa, Vanessa, yaani hakuna msanii anayeitazama sasa kama ni kitu cha watu fulani.”

Wakati THT inaadhimisha miaka 10, imeamua kusitisha kupokea wanafunzi wapya na kuongeza pia kitengo cha fashion and designing. Kwa kuanza Ruge anasema wabunifu na wanamitindo wakubwa wakiwemo Ally Rehmtullah na Flaviana Matata wamejitokeza kuwa sehemu ya mradi huo.

Kuwezesha hili, amepatikana mdhamini ambaye atalipia gharama za mafunzo nje ya nchi kwa wabunifu watatu yatayochukua kipindi cha miezi mitatu ambao wakirejea watakuwa na uwezo wa kusambaza elimu hiyo kwa wabunifu wengine.

Akitoa ushauri kwa watu wengine wenye nia ya kuanzisha kitu kama THT, Ruge amesema kitu cha kwanza na cha muhimu ni kuwa na ‘passion’ na kitu hicho na kufuta wazo la fedha kwanza.

“Ni ajabu sana mtu akiingia akawaza kama wazo la biashara,” anasisitiza. “Fanya biashara yako nyingine, hakikisha hiyo biashara yako imesimama.”

Kingine anasema ni kujifunza kusamehe kwakuwa miradi hiyo hutengeneza imani kwa watu kuwa mtu kama yeye ana uwezo wa ‘kutengeneza maisha ya mtu na kutotengeneza ya mwingine’.

“Nimeishi kwa lawama na maneno mengi sana na unaweza ukakuta kuna kipindi ‘ahh mi nataka kuacha hivi vitu sababu hizi hazistahili. Sipati kitu chochote katika hiki kitu lakini kwanini unapata hizi lawama! Lakini unagundua kwamba hufanyi kwasababu yako wewe, unafanya kwaajili ya wale wengine wanaofaidika na hili jambo.”

“Mimi nina miaka kama minne hivi, niliacha kuchukua nyimbo za wasanii wa THT na kupeleka kwenye redio popote pale hata kwangu pale Clouds. Ni kwasababu naamini nyimbo ndio inayomuuza mtu. Utakuta watu wengi wanazihesabu nyimbo za THT zinazopigwa kuliko ambazo hazipigwi.”

Kwa sasa Ruge amesema anajiondoa kwenye upande wa manejimenti ya THT ili kuwapa nafasi vijana wengine kuisimamia.

“Miaka 10 kwangu mimi THT imetosha katika kuwa moja kwa moja ndani nawaachia vijana wapo wengi wataendelea na mimi ntaendelea kubaki THT kama mbunifu.”

THT inabaki kuwa taasisi yenye mchango mkubwa kwa muziki wa Tanzania iliyosaidia kuzaliwa wasanii wakubwa wakiwemo Amini, Barnaba, Linah, Recho, Ditto, Mwasiti, Mataluma, Makomando, watayarishaji wakiwemo Ema The Boy, Nash Desigher, Tudd Thomas na wengine bila kusahau bendi yenye wapiga vyombo mahiri na dancers wanaotumiwa na wasanii kibao.

Related Articles

Leave a Reply

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents