Habari

Mfumuko wa bei waongezeka kutoka asilimia 4.5 hadi 4.8

Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Novemba 2016 umeongezeka hadi kufikia asilimia 4.8 kutoka asilimia 4.5 iliyokuwapo mwezi Oktoba, 2016 kutokana na kuongezeka kwa bei ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.

inflation-and-deflation-graph

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim Kwesigabo amesema kuwa bidhaa za vyakula zikiwemo ngano,mbogamboga, mtama, na vinywaji baridi zimechangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei nchini.

“Bidhaa nyingine zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei nchini ni Nishati , mafuta na viatu huku akibainisha kuwa kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya nchini zimeongeka na kufikia 104.32 kwa mwezi Novemba 2016 ikilinganishwa na 99.54 za mwezi Novemba mwaka jana,” alisema Kwesigabo.

Kwa upande wa mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi ameeleza kuwa umeongezeka kwa asilimia 1.1 kwa mwezi Novemba ikilinganishwa na asilimia 0.1 ya mwezi Oktoba kutokana na kuongezeka kwa Fahirisi ya baadhi ya bidhaa zikiwemo unga wa ngano, unga wa mihogo, unga wa mahindi, mtama, dagaa, mchele.

Aidha, alisema kuwa thamani ya shilingi ya Tanzania hupima badiliko katika kununua bidhaa na huduma zilezile za mlaji ambazo shilingi ya Tanzania ingeweza kununua katika kipindi tofauti, ikiwa fahirisi za bei za Taifa zinaongezeka uwezo wa shilingi ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma hupungua.

Kwa upande wa mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki Kwesigabo alisema kuwa una mwelekeo unaofanana ambapo Kenya umeongezeka na kufikia asilimia 6.68 mwezi Novemba kutoka 6.42 za mwezi Oktoba huku Uganda ikiwa na mfumuko wa bei wa asilimia 4.6 mwezi Novemba kutoka asilimia 4.5 za mwezi Oktoba.

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents