Habari

Mbowe azidi kubanwa kuhusu ufisadi

MWENYEKITI wa Democratic Party, Christopher Mtikila, amesema Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, hana haki ya kuivalia njuga kashfa ya ufisadi wa mabilioni yaliyochotwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kuwa naye anakabiliwa na shutuma za kukalia fedha za wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Theopista Nsanzugwanko

 

 

 

MWENYEKITI wa Democratic Party, Christopher Mtikila, amesema Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, hana haki ya kuivalia njuga kashfa ya ufisadi wa mabilioni yaliyochotwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kuwa naye anakabiliwa na shutuma za kukalia fedha za wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

 

 

 

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mtikila alisema deni la Mbowe, jitihada zake za kukataa kulilipa kwa wakati na madai ya kupotezwa kwa nyaraka za kimahakama zinazohusu suala hilo, ni sawa na ufisadi ambao alisema una sura nyingi na zote ni hatari kwa taifa.

 

 

 

“Ni ufisadi wa hatari mno kwa nchi kuliko kuzunguka nchi nzima kutangaza ufisadi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku (akina Mbowe) wakifukia ufisadi wao,” alisema Mtikila katika mkutano huo.

 

 

 

Maelezo ya Mtikila yamekuja, ikiwa ni siku mbili baada ya Mbowe naye kuitisha mkutano wa waandishi wa habari akilalamikia habari zilizoandikwa katika baadhi ya magazeti wiki iliyopita juu ya kesi ya madai inayomkabili kiongozi huyo, mkewe na mkurugenzi mwingine wa Mbowe Hotels, kutokana na mkopo waliochukua kutoka NSSF (wakati huo NPF) kwa ajili ya ukarabati wa ukumbi wa starehe wa Billicanas.

 

 

 

Wakati akijitetea kuhusu madai hayo, Mbowe alidai vyombo vya habari vilivyoanika taarifa juu ya kesi hiyo vinatumiwa ili kudhoofisha jitihada zake na za Chadema katika kukabiliana na wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) uliotokea BoT.

 

 

 

Katika mkutano wa jana, Mtikila alieleza kushangazwa kwake na lawama za hivi karibuni za Mbowe juu ya kuchotwa kwa takribani Sh bilioni nane kutoka akaunti ya EPA kunakodaiwa kufanywa na kampuni moja ya mawakili, huku akifumbia macho kuchukuliwa kwa Sh bilioni 84 za NSSF kunakoelezwa kufanywa na mfanyabiashara mmoja maarufu wa Dar es Salaam.

 

 

 

“Siasa safi ni ushindani wa ajenda na viwango vya uhanga kwa ajili ya ukombozi wa nchi yetu. Hatuwezi kulaani ufisadi wa CCM wa kuwanunua wapinzani na kunyamazia Chadema wanapofanya ufisadi kwa sababu upendeleo ni ufisadi pia,” alidai Mtikila.

 

 

 

“Ni kweli kwamba Mbowe hakuwa na uwezo wa kulipa deni au ni tatizo lake tu la kimaadili? Kama kweli ilitolewa amri ya Mahakama ya kukamatwa, lakini akakwepa na faili la Mahakama limepotezwa kukwamisha utekelezaji wa amri dhidi yake, je, ni kweli ndiye anayefaa kuliko wanachama wote kuongoza Chadema na kugombea urais? Je, tunakosea tukiamini kuwa chama hiki ni mafisadi,” alisema Mtikila.

 

 

 

Akizungumzia kauli hiyo ya Mtikila, Mbowe alimpa changamoto mwanasiasa huyo kutumia udhaifu anaouona kwa Chadema kukiinua chama chake cha DP na kuacha kuingilia masuala ya vyama vingine.

 

 

 

Alisema tuhuma za deni analodaiwa na NSSF amekwishalitolea ufafanuzi na kuongeza kuwa anamheshimu Mtikila kama kiongozi wa chama na hataki malumbano naye.

 

 

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents