Siasa

Marekani yampa tuzo Mengi

MWENYEKITI wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, amepokea rasmi tuzo inayoheshimika ya Martin Luther King. Mengi ambaye anakuwa Mtanzania wa nane kutwaa tuzo hiyo alikabidhiwa tuzo yake nq Balozi wa Marekani hapa nchini, Mark Green.

na Martin Malera

 

MWENYEKITI wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, amepokea rasmi tuzo inayoheshimika ya Martin Luther King. Mengi ambaye anakuwa Mtanzania wa nane kutwaa tuzo hiyo alikabidhiwa tuzo yake nq Balozi wa Marekani hapa nchini, Mark Green.

 

Taarifa rasmi ya iliyosambazwa kwa vyombo vya habari na ubalozi wa Marekani hapa nchini inaeleza kwamba, Mengi alitwaa tuzo hiyo kutokana na kutoa mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa akitumia vyombo vya habari anavyomiliki.

 

Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mengi alisema tangu alipoanzisha magazeti mawili ya This Day na Kulikoni yanayoandika habari za uchunguzi kuhjusu masuala mbalimbali yanayohusu rushwa wamekuwa wakipokea vitisho vya aina tofauti.

 

Alisema ingawa vitisho hivyo vilikwenda sambamba na kupoteza maisha kwa baadhi ya wafanyakazi, hawajawahi kutishika na akawataka waandishi wa habari kuendeleza mapambano dhidi ya ufisadi nchini.

 

Sambamba na hilo, Mengi alisema kutokana na mchango mkubwa wa vyombo vya habari kufichua habari za ufisadi na kwa ushirikiano anaouonyesha Rais Jakaya Kikwete, anaamini siku moja Tanzania itaondokana na tatizo la rushwa.

 

“I have a dream that one day Tanzania will be free from corruption,” alisema Mengi kwa Kiingereza akieleza namna anavyotamani kuiona Tanzania ikiwa taifa lisilo na rushwa siku moja.

 

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, Mengi alisema kazi ya kuanzisha vyombo hivyo maalumu kwa ajili ya kuibua ufisadi ilikuwa ngumu kiasi cha kujijengea maadui mbalimbali waliochukizwa na harakati za magazaeti hayo kuibua maovu katika jamii.

 

“Lakini tulibaki imara, tukaendelea na kazi bila kuogopa vitisho na tunaamini jamii itaelewa jukumu letu kama kioo chao ambacho watakitunza badala ya kukivunja kwa sababu ya kuibua maovu,” alisema Mengi.

 

Mengi alisema athari za rushwa ni kubwa na mbaya, bila kujali ukubwa wake, kwani inaondoa haki, uhuru na kuleta ubaguzi, mambo ambayo Martin Luther King, mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu wa Marekani aliyepoteza maisha akipigania haki za watu weusi nchini humo, alikuwa akipambana nayo.

 

“Kwa namna ya pekee kabisa, napenda kuishukuru Serikali ya Marekani kwa kunipa tuzo hii kubwa na ya hshima duniani. Hii imenipa nguvu na hamasa ya kupambana na ufisadi na maovu mengine katika jamii.

 

“Hata hivyo tuzo hii si yangu, bali ni kwa ajili ya waandishi wa habari wanaoibua taarifa za ufisadi,” alisema Mengi.

 

Mengi pia alisema tuzo hiyo anaitoa kwa Rais mstaafu, Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Rais Jakaya Kikwete, ambao alisema katika utawala wao wameonyesha dhamira ya kweli ya kupambana na rushwa.

 

Akizungumza nje ya ukumbi huo, Mengi alitoa changamoto kwa wamiliki wengine wa vyombo vya habari kuacha tabia ya kuingilia kazi za waandishi kwa kuwachagulia habari za kuandika na kuwawezesha waweze kufanya kazi za habari za uchunguzi kwa ufanisi.

 

Kwa upande wake, Balozi Green alisema vyombo vya habari duniani kote ni njia pekee ya kupambana na vitendo vya ufisadi na ndiyo maana katika baadhi ya nchi hakuna uhuru kamili wa vyombo vya habari.

 

“Hapa Tanzania nafurahi kusema kuwa kuna uhuru mkubwa wa vyombo vya habari na Serikali ya Marekani itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha inaendelea kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari wanaoandika habari za uchunguzi,” alisema Balozi Green.

 

Akimzungumzia Mengi, Balozi Green alisema hakuna shujaa aliyeacha vyombo vyake vya habari kuwa huru kufanya kazi za uchunguzi kama Mengi.

 

“Kutokana na ushujaa wake, mwaka huu hatukusita kabisa kutoa tuzo hiyo ya heshima ya Martin Luther King kwa Mengi, kwa kuwezesha vyombo vyake vya habari kufanya kazi nzuri ya habari za uchunguzi kuhusiana na rushwaÂ…,” alisema Balozi Green.

 

Alisema mbali ya kuwezesha vyombo vyake vya habari kufanya habari za uchunguzi, balozi huyo alisema Mengi kama Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa vyombo vya habari nchini (MOAT), amewezesha hata waandishi walio nje ya vyombo vyake kuibua habari za ufisadi.

 

Baadhi ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Dk. Salim Ahmed Salim, mzee Rashid Mfaume Kawawa, Jaji Joseph Warioba, Idd Simba, Joseph Butiku, Askofu Kakobe, Askofu Method Kilaini, Sheikh Othman Matata na Askofu Alex Malasusa.

 

Mbali ya Mengi, Watanzania wengine waliokwisha kuzawadiwa tuzo hiyo na miaka yao kwenye mabano ni Rashid Kawawa (2007), Salim Ahmed Salim (2006), Gertrude Mongella (2005), Mama Justa Mwaituka (2004), Profesa Geofrey Mmari (2003), Jaji Francis Nyalali (2002), Jaji Joseph Warioba (2001) na Mwalimu Nyerere (2000).

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents