Wema Sepetu

Maoni: Wema Sepetu watazamaji wa show yako wengi ni watu wa kawaida, Kiingereza kingi cha nini?

Ilani: Ukitaka kuangalia kipindi cha reality TV cha Wema Sepetu, ‘In My Shoes’ na shule hukwenda, nakushauri ukae na kamusi ya Kiingereza – Kiswahili ili uweze kwenda naye sawa. Hii ni kwasababu, asilimia 50 ya lugha anayoitumia mrembo huyu ni Kiingereza ambayo kwa Watanzania wengi imewapita kushoto.

Wema in my shoes

Nimesikia watu wengi mno wakilalamika kuwa matumizi ya Kiingereza kingi kwenye show yake yamewafanya wasikipende kipindi hicho na kunifanya nihoji, nani walengwa hasa wa kipindi chake? Kwa niaba yao ningependa kulifikisha ombi lao kwa Wema kuwa atumie zaidi Kiswahili katika kuongea ili wengi wamwelewe. Pamoja na kwamba Wema ndivyo alivyo na hata wakati akihojiwa kwenye TV/RADIO ndivyo huongea, ajizuie katika kipindi chake ili kila mtu amfuatilie.

Katika elimu yangu ya uandishi wa habari na utangazaji wa radio/TV nilifundishwa kuwa, wakati wa kuandaa kipindi chochote kile, ni lazima ubainishe, walengwa wa kipindi chako (target audience). Kwa kuangalia umaarufu wa Wema Sepetu, hakuna shaka kuwa walengwa wake wakubwa, ni watu wa kawaida kabisa ambao ndio wanunuaji wakubwa wa magazeti ya udaku yaliyolikuza jina lake nchini na wamekuwa wakimpenda sana.

Kwa namna anavyokiendesha kipindi chake kwa kusimulia matukio yanayooneshwa kwenye kipindi, walengwa ni wale wanaokielewa Kiingereza. Swali ni je, wasomi, raia wa kigeni au watoto wa Masaki, Osterbay na maeneo mengine ya watu wa hali ya juu wanaosoma ama waliosoma kwenye shule za kishua wanakiangalia kipindi hicho? Sio kweli na kama wapo basi ni wachache.

Watu kama hao kwanza hawatumii ving’amuzi vinavyotumika na watu wa hali ya kawaida ambako TV za kibongo zipo. Watu wa maeneo hayo, huangalia DSTV zaidi ambako huko hupenda kuangalia vipindi vya kinyamwezi kama, Keeping Up With the Kardashians, Ice Loves Coco, The Hustle Family ya T.I na Tiny ama The Real Husbands of Hollywood na zingine kibao. TV za kibongo huangaliwa kwa nadra na tena labda wakati wa taarifa ya habari saa 2 usiku, na baada hapo huendelea kuangalia TV za nje.

Kipindi cha Wema Sepetu ambacho huoneshwa na runinga ya EATV, kinaangaliwa zaidi na watu wa kawaida ambao kwa bahati mbaya amekuwa akiwatenga kwa kupenda mno kuongea Kiingereza. Tanzania bado hatujafika huko na hilo Wema anapaswa aliweke kichwani mwake. Asiletee maisha ya Hollywood kwenye kipindi kinachoangaliwa na Mtanzania wa kawaida.

Kama angekuwa hajui kabisa Kiswahili, basi hilo lingeeleweka. Abadilike..

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents