Habari

Manyaunyau jela miaka 3 kwa utapeli, alidai angemfufua marehemu

Mkazi wa Dar es Salaam, Dunia Salumu maarufu kwa jina la Dk. Manyaunyau, amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela pamoja na kulipa fidia ya Sh milioni 10 baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha Sh milioni 29.6 kwa njia ya udanganyifu.

scan0006

Manyaunyau anadaiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mlalamikaji, Tekra Modesta kama malipo ya kazi ya kumfufua marehemu kaka yake aliyefahamika kwa jina moja la Modest ambaye alifariki dunia miaka kadhaa iliyopita.

Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Flora Haule, alisema mtuhumiwa huyo ametiwa hatiani baada ya ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka kujitosheleza.

“Mahakama inatoa hukumu kwa mtuhumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa fidia ya Sh milioni 10 baada ya kumaliza kutumikia kifungo chake ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,” alisema Hakimu Flora.

Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanne ambao wote waliithibitishia mahakama juu ya mtuhumiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kwa njia za udanganyifu.

Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Estar Kyala, aliiambia mahakama kuwa hakuna kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa na hivyo kuiomba kutoa adhabu kali ili kuwa fundisho kwa wote wenye tabia kama hizo.

Katika maelezo ya awali, ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mlalamikaji kama malipo ya tukio la kutaka kumfufua kaka wa mlalamikaji.

Ilielezwa kuwa mtuhumiwa alipokea fedha hizo kwa awamu mbili tofauti ambapo awali Mei 2007 jijini Dar es Salaam alipewa kiasi cha fedha ambacho hakikufahamika.

Mei Mosi, mwaka 2008 mtuhumiwa alipokea kiasi kingine cha fedha kama malipo kwa ajili ya kumalizia kazi yake ya kumfufua marehemu ambaye ni ndugu wa mlalamikaji jambo ambalo alishindwa kulitekeleza.

Manyaunyau amejizolea umaarufu mkubwa katika maeneo mengi nchini kwa kile kinachodaiwa kuwa anao uwezo wa kutibu na kuwafichua wachawi popote walipo sambamba na staili yake ya kunyonya damu ya paka akiwa katika shughuli zake za uganga.

Katika tukio lililovuta wakazi wengi wa Dar es Salaam, Manyaunyau anadaiwa kumwibua nyoka ambaye alikuwa tishio na kuzusha hofu kubwa kwa wakazi wa maeneo ya Manzese Midizini ambapo ilidaiwa kuwa alikuwa akiwagonga watu katika mazingira ya kutatanisha katika njia inayopita kwenye makaburi.

Inaaminika kuwa baada ya kuitwa, Dk. Manyaunyau aliweza kumuibua nyoka huyo na kuonekana hadharani tukio lililohisiwa kuwa ni la kimazingara zaidi.

Chanzo: Mitandaoni

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents