Bongo Movie

Mambo ya msingi ambayo kila muigizaji wa Tanzania anapaswa kujua

Kuna waigizaji wengi hapa bongo na kila mmoja anataka kuonekana ni bora zaidi kwa kila anachokifanya. Habari ya kusikitisha ni kwamba ni wachache sana walioweza kushika nafasi za juu kwa watazamaji wao. Wengine wanaendelea kushangaa kwanini filamu zao hazijaweza kukubalika mitaaani. Uigizaji ni kama taaluma zingine ambazo ukishindwa kufanya mambo ya msingi, utaendelea kuwakera watazamaji wako siku zote na kufanya filamu hiyo kuchukiwa.

Lulu akiwa na tuzo yake

Katika mambo yote huwezi kubadilisha namna unavyoonekana kwenye camera na namna sauti yako ilivyo. Bali kuna vitu vichache ambavyo unaweza kuvifanyia kazi na vikakusaidia kuboresha uwezo wako wa kuigiza.  Ingawa wengi wanadhani kuigiza ni rahisi si rahisi kama unavyodhani, unahitaji bongo wa ziada na akili zinazofanya kazi vizuri sana.

Jifunze namna ya kuigiza Kwako Kama nilivyoseam kuigiza si rahisi hivyo unahitaji kujifunza namna unavyoonekana kwenye taaluma hiyo. Ukitaka kujifunza unatakiwa uwe chini ya mtu ambaye anajua kuigiza na anaweza kukukochi ukawa muigizaji mzuri. Jifunze kwa waigizaji wakubwa wenye malengo na wanaofanya vizuri, angalia maisha yao ya kila siku, wanapenda kufanya nini na wanafanya maamuzi gani? Kama utagundua marehemu Kanumba alikuwa anakua katika uigizaji wake kila siku, inamaanisha alikuwa anajifunza kitu kipya na namna gani aweze kutoka katika kila filamu.

Usiwe Mchelewaji kwenye Mazoezi hata kama utakuwa maarufu kiasi gani, unahitaji kuwa mtu ambaye anazingatia muda na kuweka umuhimu wa matumizi ya muda hasa unapoandaa filamu mpya. Usifikiri unajua sana kiasi kwamba unafika kwenye mazoezi muda unaojisikia, la hasha unakatisha tamaa watu wengine na uwezekano wa kufanya chini ya kiwango ni mkubwa.

Tambua Mipaka yako: Inawezekana ni jambo la kawaida, ila kuna waigizaji wengi amabao hawawezi kwenda kulingana na maeneo yao ya uigizaji. Hakikisha unajua mazingira ya kile unachokwenda kukifanya kwa kurudia mara nyingi zaidi ili kikae kwenye mawazo na utendaji wako kabla ya kufanya rekodi ya mwisho. Hutakiwi kufanya mazoezi ya namna ya kuongea peke yake bali hata namna utakavyoongea, utaonekanaje na mwitikio wa viungo vyako vya mwili vitashabihiana vipi. Usipende kuja na mistari yako au maneno yako kinyume na mwandishi wa hilo igizo au filamu.

Unatakiwa uwe Msikilizaji Mzuri: Ninaamini wewe ni msikivu, sikiliza unachoambiwa. Unahitaji kujua namna ya kumsikiliza mwongozaji wa filamu kwa sauti na ishara na kuweza kutafakari na kupambanua kwa umakini na haraka kabla ya kuendelea na kitu kingine.

Hakikisha Mwonekano wako ni Sahihi: Hakuna kitu kibaya au watazamaji wasichopenda kuona tofauti kati ya nafasi ya mtu anayeigiza na nafasi hiyo. Mfano, mtu anaigiza maisha ni magumu au mabaya lakini mwonekano wake hauonyeshi hata kidogo kwa hiyo nafasi. Utaona jamaa ni mnene, anavaaa nguo nzuri, sura imenawili n.k. Unajifunza mini pale 50 Cent alipototeza uzito wa kutosha ili aweze kwendana na nafasi ambayo alikuwa anacheza kwenye filamu? Alitaka mwonekano wake use sahihi na watu wavutiwe na nafasi ambayo alikuwa anakonda kucheza. Kuna wengine wanaigiza nafasi za ukurugenzi wa makampuni hawajui lugha za kibiasharara au lugha za kiuongozi kwenye makampuni, namna ya kuongea, mwitikio wa mambo na namna ya kufanya maamuzi.

Jitoe kwa Moyo wote kwa kile unachoenda kukifanya: Waigizaji ambao wanasoma na wanajifunza vitu vingi hula wanavutia kuwatazama. Ila waigizaji ambao hawaonekani kusoma na kujifunza wanakera kuwatazama kwasababu hawana kitu kipya kwenye taaluma yao. Unapojitoa kwa moyo wote kwa kile unachokwenda kukifanya unahitaji kupunguza visingizio vya kuchelewa kwenye foleni. Hakuna mtu asiyejua kwamba bongo kuna foleni hivyo unahitaji kuondoka mapema nyumbani kwako ili uweze kufika kwa muda muafaka sehemu fulani. Kitu kingine unatakiwa kujua kuna watu wengi wanaweza kucheza nafasi yako ukileta upuuzi au ukashindwa kufanya kwa moyo wako wote.

Heshimu watu unaofanya nao kazi. Watu unaofanya nao kazi ndio wanakusaida kukua na kwenda mbele kila siku, jitahidi kutengeneza mahusiano na hao watu na kuheshimu utu wao na nafasi zao. Usiwachukulie poa na kuwafanyia mambo ya hiana, lugha chafu na kudharau jinsi walivyo. Hautaweza kufika mbali, kwani kiwango chako kitashuka na kupotea kabisa. Huwezi kwenda peke yako unahitaji watu wa kwenda nao.

Unapokuwa mwigizaji si rahisi kama watu wanavyodhani, kuna muda mrefu ambao hutakuwa na fedha za kutosha, kukataliwa na ushindani mkubwa katika tasnia hiyo. Lakini hutoweza kufanikiwa endapo utaruka na kuacha mambo ya msingi kuweza kufika kule unakotaka kwenda. Hebu jichunguze kama unafanya hayo mambo kwenye taaluma yako ya uigizaji halafu hone kama ndivyo watazamaji na wenzako wanavyokutizama.

Awali Mwaisanila

A Personal Career Development specialist, passionate about empowering emerging generations of student, graduates and working class.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents