Bongo5 Makala

Mambo 10 mastaa wanaweza kujifunza kutokana na deal la bilioni 8.5 kati ya Kidoti na Wachina

Nilibahatika kuhudhuria uzinduzi wa kampuni ya Jokate Mwegelo, ‘Kidoti Loving’ October 2012 jijini Dar es Salaam ambapo mrembo huyo alizindua brand yake hiyo iliyokuwa na bidhaa za nywele za weaving.

Jokate na Mr Deng wakisaini mkataba
Jokate Mwegelo na CEO wa kampuni ya Rainbow Shell Craft ya China, Deng Guoxun wakisaini mkataba wa ubia huo mbele ya wageni na waandishi wa habari Ijumaa iliyopita kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam

Baada ya miaka miwili, nimefanikiwa tena kuhudhuria sherehe ya kusaini mkataba wa ubia kati ya kampuni ya Kidoti na kampuni ya China, Rainbow Shell Craft wenye thamani ya shilingi bilioni 8.5. “Tutajenga viwanda, kufungua maduka. Kuiweka Kidoti kama brand namba moja nchini na kwingine,” alisema Jokate. “Wamewekeza kiasi hicho cha fedha ili kuliwezesha hilo na pengine mengi zaidi. Ni kitu cha kunufuika sote.”

Hakuna anayebisha kuwa Jokate amepiga bao na ndio maana mastaa kibao wakiwemo Wema Sepetu, Nancy Sumari, Penny, Lulu na wengine wamempongeza.

“Way to go baby girl,” aliandika Wema kwenye Instagram. “What can I say, I’m more dan proud… Let this be a challenge to every youth. Yes it is possible. Mi nathubutu kusema Umetisherrr… #Hatari #SayGoodbyeTo2014 …. 2015 is mos def a good year for u,” aliandika Wema.

“Huge Congrats to the little sister. Young, amazingly beautiful and getting it! #BossMoves,” aliandika Nancy huku Penny akichagiza, “Jojo darling you are a motivation and a half. I say thank u inspiring most of us…congratulations.”

Hilo ni deal kubwa zaidi lililowahi kufanywa na staa wa Tanzania hivyo kuna mengi ya kujifunza. Haya ni mambo 10 ambayo mastaa wengine wanaweza kujifunza kutokana na mkataba huo mnono alioupata Jokate.

1. Mastaa ni migodi inayotembea

Mwanamuziki, muigizaji wa filamu, model au staa mwingine anayependwa ni mgodi unaotembea. Zinahitajika tu mbinu za kuyabaini madini hayo na kuanza kuyachimba. Katika ulimwengu huu ambao ununuaji wa nyimbo au album umepungua kwa kiasi kikubwa, pamoja na kutumia show kama njia za kuingiza mkwanja, mastaa katika nchi zilizoendelea wamewekeza nguvu zao nyingi kwenye kutumia brand zao kuanzisha biashara.

Kwa mfano, album ya mwisho aliyotoa Dr Dre ni ‘2001’ iliyotoka mwaka 1999, lakini mwaka huu amekuwa msanii aliyeingiza fedha nyingi zaidi kwa kuweka benki dola milioni 620, asante kwa brand yake yenye mafanikio, Beats By Dre.
Huo ni mfano mmoja tu kati ya mingi ambayo wanaweza kuitumia. Na sasa tuna mfano wa karibu kabisa kutoka kwa Jokate ambaye safari yake baada ya miaka mitano inaweza kumfikisha katika sehemu ambayo tunaweza tusiamini.

2. Anza tu, mengine yatakuja

Nakumbuka baada ya Jokate kuingiza nywele zake za weaving sokoni, alikutana na upinzani mkubwa kutoka kwa brands zingine zilizozoeleka kama Darling na zingine. Na kwakuwa Watanzania wengi huamini zaidi bidhaa za nje kuliko za nyumbani, wasichana wengi huenda walizipa mgongo weaving za Jokate. Na ndio maana mwaka 2014 wote Kidoti ilikuwa kimya kiaina.

Huo ni muda ambao nahisi alikuwa akijipanga ili kuongeza nguvu zaidi baada ya kubaini changamoto mbalimbali kwenye biashara hiyo. Leo hii amepata wawekezaji wenye nguvu ya kujenga viwanda na ambao wamepania kuifanya Kidoti kubwa brand kubwa Afrika Mashariki. Amepata wawekezaji ambao wamemtoa kwenye biashara ya nywele tu hadi kuingia kwenye bidhaa zingine kama sandals, mikoba na vitu vingine.

Ukiangalia mfano wa Dr Dre na headphones zake pia ni vilevile. Wakati wanaanzisha Beats Electronics na Jimmy Iovine mwaka 2008, hawakuwahi kuwaza kuwa brand yao itakuwa kubwa kiasi cha kuwavutia Apple kuinunua kwa dola bilioni 3 mwaka huu.

3. Onesha kuwa unaweza kusimama mwenyewe

Wakati Jokate anaizindua Kidoti Loving mwaka 2012, hakukuwa na mwekezaji mkubwa nyuma yake. Kile alichoweza kukikusanya kwenye kazi zake ndicho alichotumia kuanzisha kampuni yake. Ule usemi kuwa aliyenacho huongezewa unahusika hapa. Hakuna mwekezaji anayeweza kukupa shilingi bilioni 8.5 kama hana uhakika kuwa una uwezo wa kusimama kwa miguu yako pia.

4. Ota mambo makubwa na thubutu

Jokate alikuwa anazijua brands kubwa za weaving na vitu vingine vya urembo, lakini hiyo haikumkatisha tamaa kuanzisha ya kwake. Uthubutu huo ndio umemfikisha hapo alipo leo. Na ndio maana niliwahi kuandika makala inayohusu kasumba ya wasanii wa Tanzania kukimbilia kwenye biashara ya t-shirts zenye majina ya nyimbo zao wakati wana uwezo wa kufanya mambo makubwa zaidi.

Nilisema ni bora kama wangeanzisha clothing line ambayo itakuwa ikitoa designs mbalimbali zenye ubora mzuri. Wasanii wana uwezo wa kufanya mambo makubwa zaidi ya kuprint t-shirt 100 za shilingi 20,000 na tena kwa msimu.

5. Una mtaji wa kuanzia – mashabiki

Ukiwa staa, nyuma yako unakuwa na kundi kubwa la mashabiki watakaokuunga mkono kwa lolote utakalolifanya. Kama ukifiria kutengeneza biashara kuwalenga wao, haiwezi kufeli kwakuwa tayari utakuwa na kianzio cha wateja wako. Hebu fikiria leo Diamond Platnumz akiamua kuanzisha perfume yenye kiwango kizuri, inayonukia vizuri, kwa nguvu aliyonayo sasa, unadhani itafanikiwa kiasi gani? Lazima ipige bao!

6. Kuna watu wenye hela nyingi wako tayari kuwekeza kwenye jina lako

Katika biashara kuna kitu kinaitwa ‘Venture Capital’ ikimaanisha mtaji ambao mtu huwekeza kuanzisha mradi mpya ambao anaamini utamlipa pia. Msanii anaweza akawa na ndoto kubwa ya kuanzisha mradi ambao kwa wakati huo anaweza akawa hana mtaji wa kutosha. Mathalan amefikiria kuanzisha biashara inayohitaji mtaji wa dola milioni 10. Hii ni fedha nyingi sana kwa msanii wa Tanzania kuwa nayo.

Lakini huko nje kuna wafanyabiashara ambao dola milioni 10 ni asilimia 0.01 ya utajiri alionao. Kama akibaini kuwa msanii huyu ana akili, ana nguvu, ana timu, anajiweza, ana ushawishi na ana wazo lenye kila dalili kuwa litafanikiwa, hawezi kufikiria mara mbili kuwekeza fedha hizo kusupport idea yake ya biashara. Mfanyabiashara kama huyu anahitaji tu kujua kuwa fedha yake itarudi au itakuwa kwenye mikono salama.

7. Usifikirie wawekezaji wa ndani peke yake

Maswali ambayo wengi tunajiuliza leo ni wapi Jokate aliwapata wachina hawa walioamua kuja Tanzania na kumpa booster ya shilingi bilioni 8.5! Jibu analo mwenyewe na kama ukimuuliza swali hilo, kwa busara hawezi kukuambia kwakuwa hilo ni suala ‘classified’ lakini fundisho hapa ni kuwa kuna wawekezaji nje ya nchi wanaotafuta mtu wa kuingia naye ubia wawekeze mamalioni ya shilingi. Unawapataje? Bahati mbaya wawekezaji kama hawa hawatakufuata wewe kwakuwa una jina kubwa Tanzania, utasubiri mno. Wawekezaji hawa ni kuwakutafuta na kuwaimbisha! Tumia connections zako kuwabaini.

8. Tengeneza timu ya watu wenye uelewa wa masuala ya biashara, usijaze washkaji

Miradi mingi ya mastaa wa Kibongo inafeli kwasababu hutengeneza timu iliyojaa washkaji ambao michango yao ya kimawazo huwa haina tija. Kama unaweza, ajiri wahitimu wa chuo. Ajiri vijana wanaoweza kuandika proposal za biashara, ajiri vijana wanaoweza kukusaidia kwenye masuala ya masoko, mawasiliano nk. Hakuna mwekezaji atakayemwaga dola milioni 5 kwenye timu iliyojaa wapambe na wapiga majungu!

9. Vitendo zaidi, maneno machache

Ni vizuri kutangaza mipango, matarajio na ndoto lakini pale ambapo mambo yanapokwama ni rahisi kujilaumu kwanini ulisema. Hivyo ni bora kuhakikisha kitu kimekamilika asilimia 100 na kufanya uzinduzi wa kishindo. Ziko wapi ndala za Juma Nature alizodai anaanzisha? Zaidi ya mwaka mmoja amekuwa akisema kontena lipo njiani! Alipagawa zaidi baada ya kusikia Jokate anakuja na bidhaa kama hiyo bila kujua kuwa mwenzake kajipanga na kwamba hakuna biashara yenye sharti la ‘exclusivity’ lasivyo leo tusingekuwa na makampuni zaidi ya manne ya simu.

10. The sky’s the limit!

Unaweza kufanya lolote kama utajituma, utaamini na ukimuamini muweza!

Related Articles

3 Comments

Leave a Reply

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents