Burudani

Mama aua mtoto wake kisa kukataa shule

Mkazi wa Nsumba katika Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza Joyce Mathayo (33), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kumpiga mtoto wake Mathayo Manisi (12) na kumuua kwa kosa la utoro shuleni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini hapa jana alisema tukio hilo lilitokea Januari 11, mwaka huu saa 4 asubuhi.

Alisema Mary alikamatwa na polisi baada ya kumpiga fimbo mtoto wake huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu sehemu mbalimbali za mwili na kumsababishia kifo, kitendo ambacho ni kosa la jinai.

Kamanda Msangi alisema siku ya tukio, mtoto huyo alimkatalia mama yake kwenda shule na kusema hataki shule tena, ndipo mama huyo alipopatwa na hasira na kuanza kumpiga fimbo sehemu mbalimbali za mwili na kumsababishia kifo muda mfupi baadaye.

Alisema baada ya mtoto huyo kufa, wananchi waliamua kutoa taarifa Kituo cha Polisi na polisi walifika mapema kwenye eneo la tukio na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa.

“Mtuhumiwa yupo katika mahojiano na polisi, pindi uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani, mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na timu ya madaktari kutoka Hosipitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure na tayari umekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya maziko,” alisema.

Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, Kamanda Msangi ametoa wito kwa wazazi kuwalea watoto wao katika maadili mema na nidhamu kwa kuwaelimisha mambo mazuri na mabaya ili kuepusha kutoa adhabu za vipigo kwa watoto kwa kujenga familia bora isiyo ya ukatili.

Source: Habari Leo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents