Bongo5 Makala

Makala: P-Square wametuburudisha na kutuachia funzo muhimu

Nikiwa na begi langu lenye camera ya kazi, niliwasili Leaders Club mapema mida ya saa 2 kasoro hivi usiku. Nakubali, ndio nilienda mapema mno. Si kwasababu nilikuwa nimeipania show ya P-Square, lahashaa. Nilihitaji tu kuwasili mapema ilimradi nisipitwe na kila jambo muhimu litakalotokea.

Peter akiimba wimbo kwa hisia kali

Nje ya Leaders, ulinzi ulikuwa mkali mno. Walionekana askari wengi kuanzia kwenye kona ya kwanza ya kuingia Leaders baada ya kuiacha barabara ya lami. Muonekano huo tu, ukanipa faraja kubwa kuwa mali na watu muda wote wa show watakuwa salama.

Kulikuwa na njia moja tu ya kuingilia iliyogawanishwa katika vimilango vingine zaidi ya sita vilivyosimamiwa na askari wa ulinzi waliokuwa na sare zao. Hapo nikakaguliwa kwa vifaa maalum kuanzia chini na ndani ya begi langu ili kuangalia kama nilikuwa na bomu ndani… Lol… usishtuke, nilikuwa nimebeba camera yangu tu, hakuna kingine. Itifaki ilizingatiwa.

Ndani palikuwa pameshaanza kuchangamka. Kwa mbali nilimuona DJ Sama kwenye 1 na 2 akifanya yake kama wasemavyo wenyewe wazee wa East Africa Radio. Eneo la mbele jirani na jukwaa tayari palikuwa pamejaa. Watu wengi hasa wazungu waliokuwa wamechangamka kiaina, walionekana kukunwa na burudani hiyo na kucheza kwa raha zao.

Kwa pembeni kidogo kulikuwa na sehemu ya VIP iliyokuwa imetengwa na Hennesy. Palikuwa pametengenezwa vizuri na wale walioweza kumudu walijimwaya kule.

Mwanzoni palianza kama kuboa kiaina, hivyo nikaenda pembeni kidogo kutafuta kinywaji changu kupoza koo. Kama kawaida pembezoni mwa uwanja kulikuwa na vibanda kadhaa vilivyokuwa vikitoa huduma ya bites na misosi mbalimbali.

Haukupita muda mrefu, washereheshaji wa siku hiyo, Dulla Mjukuu wa Ambua na T-Bway walivamia stage kutokea chini kwa ngazi maalumu zilizotengenezwa kupanda zenyewe kutoka chini hadi juu huku wao wakiwa wameinama kama kiumbe cha ajabu kilichoanguka kutoka mawinguni.

Shangwe zilitawala baada ya wawili hao kuanza kutangaza na kuwapandisha watumbuizaji wa kwanza, dancers walioshinda shindano la Dance 100. Sikupenda performance yao japo walipata shangwe za hapa na pale. Sababu kubwa ya kutopenda kile walichokifanya ni aina yao ya uchezaji kwa kutumia zaidi sauti za effects na si kwa kucheza kwenye wimbo unaoeleweka. Kingine ni utengezaji wao mbovu wa megamix yao iliyokuwa na nyimbo fupi na ambazo hazishiki.

Performance ya kwanza ya kueleweka ilianza baada ya Ben Pol aliyesindikizwa na msanii wake Alice kupanda. Akiwa amevaa koti la rangi ya blue bahari lilitengenezwa na mbunifu wa mavazi, Pedaih wa PSJ Couture, Ben Pol alionesha ukomavu katika uimbaji wake kwa kutumbuiza hits zake zote kwa ustadi mkubwa.

IMG_7915
Ben Pol

Alifuatia Lady Jaydee na dancers wake. Mkongwe huyo alikuwa amevalia mavazi kama askari jeshi wa kike anayeshiriki kwenye gwaride na kupendeza sana. kama kawaida yake, Lady Jaydee alizikonga vyema nyoyo za waliohudhuria kwa kutumbuiza nyimbo zake za zamani na za sasa zikiwemo Yahaya na Joto Hasira.

Lady akiwa ndani ya mavazi kama ya askari wa kike
Lady Jaydee

Wakati akiimba Joto Hasira ndipo alipomkaribisha rasmi Profesa J kuchukua usukani wa show. Profesa alikuwa amesindikizwa na rapper ambaye sijawahi kumuona lakini aliyemudu vyema kumpa tafu Mchawi huyo wa rhymes kufanya show nzuri pia.

IMG_2902 - Copy
Profesa Jay

Niseme wazi, Joh Makini ndiye aliyekuja kuipa uhai hip hop. Japokuwa yeye hakuwa akipigiwa vyombo na bendi, show yake iliwasha moto Leaders Club. Mwamba huyo wa Kaskazini alitumbuiza nyimbo zake zote zilizohit na nusu ya uwanja ulisikika ukimalizia mashairi yake. Kuanzia Higher, Stimu Zimelipiwa, Hao, Niaje ni Vipi, Manuva na zingine.
IMG_2951
Joh Makini

Baadaye, Joh alikuja kupewa kampani na Weusi, Nikki wa Pili na G-Nako na kuongezea nyimbo zingine, Nje ya Box na Bei ya Mkaa.

Nikki wa Pili baada ya kupanda kumpa shavu kaka yake Joh Makini
Nikki wa Pili

Mpaka Weusi wanaondoka kwenye stage, wapenzi wa burudani walikuwa tayari kuumudu moto uliokuwa unakuja wa P-Square.

Alikaribishwa DJ Mafuvu kuwaweka sawa kwanza na ndipo bendi yenye watu wanne tu ilipanda kuweka sawa vifaa vyao.

P-Square walipopanda, uwanja mzima wa Leaders Club ulizalisha shangwe nene kuwakaribisha. Peter na Paul wakaanza kuangusha fire. Kitu kimoja ambacho mimi kiliniacha mdomo wazi, ni muziki mzito uliokuwa ukipigwa na watu wanne tu, na kufanya uonekane kama unachezwa na watu zaidi ya 10.

Bendi ya P-Square inajua haswaaa. Ilikuwa ikipiga nyimbo zao kwa ustadi kiasi ambacho ilikuwa rahisi mno kuyadanganya masikio yako kuwa unachokisia pale huenda sio live bali ni CD. Tofauti yake ni kuwa, P-Square wanajua mno kutengeneza ladha tofauti ya nyimbo zao na kuzifanya ziwe tamu zaidi zinapoimbwa live. Kwa mfano, walikuwa wakianza kwa kuimba kama slow na baadaye kuja kuuimba wimbo kwa namna ulivyozoeleka.

Paul akivuta hisia
Paul Okoye

Kwa namna ambavyo walikuwa wakilitawala jukwaa, ni halali P-Square wawe wasanii wanaolipwa zaidi barani Afrika. Si kwa maneno tu, nimeamini kuwa, ni wasanii wachache sana wa Afrika (ukiwatoa DRC) wenye uwezo wa kutumbuiza vizuri zaidi live. Nadiriki kusema kuwa, unaweza kuwaweka Davido, Iyanya na Wizkid pamoja lakini hawawezi kufikia uwezo wa mapacha hawa.

Kuna mambo kadhaa niliyojifunza kwenye show hiyo ambayo ni pamoja na:

Kutengeneza versions tofauti za nyimbo

Hiki si kitu kipya sana, na wasanii wengi hufanya hivi pale wanapokuwa wakiimba live. Lakini P-Square walinigusa zaidi kwa jinsi wanavyofanya wao. Baadhi ya nyimbo zao za kuchangamka ambazo nilitegemea wangezikimbiza kama kawaida, walizitengenezea ladha nyingi tamu ya kusikilizika zaidi. Hakuna wasiwasi kuwa, jamaa hawa hufanya mazoezi makali na bendi hiyo na kila wimbo ulibadilishwa na kupigwa katika aina ambayo usingeweza kuona hata chembe ya kosa.

Nyimbo zilizokuwa zinagusa mapenzi na uhusiano waliziimba kwa hisia kali na kwa uwezo wao wote. Huu ulikuwa ni uimbaji kama wa msanii mchanga aliyependa kwenye stage kubwa kama ile kwa mara ya kwanza na anayetaka kuwadhihirishia watu kuwa ana uwezo mkubwa.

Paul akiimba kwa hisia
Paul akiimba kwa hisia

P-Square walitumbuiza kama si wasanii wale matajiri tunaowafahamu. Kwao kila show ni muhimu na ni lazima wazikonge nyoyo za mashabiki.
Peter akiimba kwa hisia
Peter

Bendi ni zaidi ya wafanyakazi, ni familia..

Peter alisema wapigaji wa vyombo wa bendi yao ni watu waliokuwa nao tangu enzi za utoto miaka iliyopota. Ni washkaji zao wanaotembea nao kila mahali. Uhusiano uliopo kati ya P-Square na bendi hiyo ni mkubwa kiasi cha kuchukuliana kama familia. Uhusiano huo ndio unaoleta kile nilichokishuhudia siku ile.

Kuengage na mashabiki

P-Square si wasanii tu, ni entertainers. Nilifurahishwa na uwezo wao mzuri wa kuwashirikisha watazamaji kwenye show yao. Kwa mfano walianzisha mashindano ya kizushi pale pale jukwaani ili kuonesha nani kati yao ndiye mwenye kipaji zaidi. Mwanzoni Peter alivuta juu shati lake na kuonesha six pack yake kifuani, huku Paul akidai kuwa yeye hana six pack bali anayo one pack kubwa zaidi na kutoa suruali yake kubaki na boxer, hali iliyoamsha shangwe za hatari.

Baaadaye Paul alikamata gitaa la besi akitaka aoneshe uwezo wake. Peter akasikika akisema, amekua pamoja kwenye nyumba moja na hajawahi kumuona kaka yake akipiga gitaa. ‘His name is Paul Okoye, Paul Okoye disgrace yourself,’ alisema Peter. You got one pack, show them one pack or 2 pack, go go let me see,’ aliongeza. Akiwa ameshika gitaa lake, Paul alisema ‘I am about to do 2 Pac, let’s go’ na ndipo alipoanza kupiga bass ya wimbo wa 2 Pac ‘Do For Love’, bendi ikampokea na Peter kuanza kuimba chorus ya wimbo huo.

Baada ya hapo Peter alishikaa gitaa la solo na kucharaza wimbo wa Ja Rule aliomshirikisha Ashanti, Always on Time kabla ya kupiga wimbo wa The Product G&B na Wyclef – Cluck Cluck.

Surprises

Peter Okoye ametoka kufunga ndoa hivi karibuni lakini ili kuwafurahisha zaidi watu aliamua kumkosea kidogo mkewe Lola Omotayo kwa kumfanyia surprise msichana mrembo aliyekuwa pale. Alimpandisha juu mrembo huyo na kumvalisha saa yake kabla ya kumbusu na kuibua shangwe zito Leaders Club.
Onyinye akivishwa saa na Peter
Mrembo akivishwa saa na Peter

Onyinye - Peter amkibusu

Onyinye - mrembo akifurahia

Hakuna anayeweza kuiongelea vibaya show hiyo iliyohudhuriwa na watu wa kila aina wakiwemo wazungu kibao wa mataifa mbalimbali.

Show ilihudhuriwa na watu wa mataifa mbalimbali

Ilikuwa ni show ya watu wengi lakini iliyokuwa na heshima kubwa. Kwa aina ya watu wale waliohudhuria siku hiyo, nilipata picha kuwa burudani ni kiwanda kikubwa kinachoweza kuwapa kipato kikubwa si tu wanamuziki wanaotumbuiza, bali waandaji wenyewe pia kama tu kila kitu kikifanywa vizuri.

Hakikuwa kitu cha kawaida Leaders kujaa vile ilhali kiingilio kilikuwa ni shilingi 35,000 hadi 50,000 uwanjani. Inawezekana kabisa kufanya maandalizi kama hayo kwa kutumia wasanii wa hapa hapa nyumbani na kwa kiingilio kama hicho, kwa kuweka bendi ya uhakika na wasanii wakalipwa mathalan shilingi milioni 50 kila moja.

Kwa mfano huo, waandaaji wa matamasha wanaweza kutengeneza tamasha la muziki (music festival) la hata siku tatu mfululizo na kama line up ya wasanii ikiwa ya kueleweka na muziki upigwe live, Dar inaweza kuwa na tamasha lake sawa na Sauti za Busara lilivyo.

Niwapongeze sana East Africa Radio kwa maandalizi mazuri ya show hiyo. Watu wengine wanaoandaa matamasha kama hayo, wajifunze kitu kutoka kwenye show hiyo ili tukuze zaidi kiwanda cha burudani nchini.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents