Bongo5 Makala

Makala: BSS msiwalazimishe washiriki waimbe Bongo Flava tu!

Juzi (Jumapili) shindano la Bongo Star Search limefikia patamu haswaa! Kulikuwa na mpambano mkali wa washiriki wote bora waliopatikana kwenye usaili wa mikoa mbalimbali nchini.

Washiriki 50 walikuwa wakipambana kuingia kwenye Top 20. Kila mshiriki alitupa karata yake aliyoamini ingeweza kuwavutia majaji watatu waliokuwa wametega maskio yao ili kusikia vizuri vipaji hivyo.

Lilikuwa ni jambo la kawaida baadhi ya washiriki kuangua vilio baada ya kuambiwa kuwa jana ulikuwa ni mwisho wa safari yao. Kilichotia huruma zaidi ni mshiriki mmoja wa kike aliyegoma kuondoka baada ya kuambiwa kuwa hatoweza kuendelea. Msichana huyo alipiga magoti chini na kuanza kulia kwa uchungu akiwabembeleza majaji wampe nafasi ya pili, lakini ombi lake halikupitishwa.

Ikiwa chini ya udhamini mpya na mnono, Bongo Star Search ya mwaka huu inaonesha kuwa na ushindani mkali kwakuwa dau la shilingi milioni 50 si dogo.

Lakini kuna kitu kinaleta shida kidogo. Majaji kutawaliwa na ‘ubongo flava’ zaidi na kusahau kuwa muziki ni universal language. Kuna washiriki wenye uwezo mzuri katika uimbaji wa nyimbo za R&B ambao inaonekana wanakatishwa na tamaa na majaji.

Kuna mshiriki mmoja wa kiume ambaye aliimba wimbo ‘mtamu’ wa mwanadada Brandy uitwao ‘True’ unaopatikana kwenye albam yake ya mwaka 2008, Human. Kwa wanaoufahamu wimbo huo, walijisikia raha kwakuwa kijana aliuimba vile vile, tena kwa sauti ya kiume.

Bahati mbaya ni kuwa karibu majaji wote walikuwa hawaujui wimbo huo na hivyo kuchukulia poa uimbaji huo. “Tatizo umezidisha uzungu sana,” ilikuwa ni kauli ya Master J baada ya mshiriki huyo kuimba. Pamoja na kwamba mshiriki huyo alifanikiwa kuingia Top 20, majaji wanapaswa wakumbuke kuwa wanakuza kipaji cha Tanzania kiwe pia na uwezo kimataifa.

Wengi wanazijua nyimbo hizo, hivyo wanafurahia kuusikia wakiziimba. Panapokuwa na washiriki wenye uwezo wa kuimba muziki wa nje, show inakuza wigo wa kuangaliwa zaidi. Na kipaji ni kipaji tu. Jaji mzuri anaweza kukijua kipaji cha mtu hata kama akiimba kichina.

“This is my 1st TIME watching Epic BSS since season 2..pamoja na UDHAMINI mnono wa mwaka huu lakini naona MATATIZO yaleyale..na leo nimegindua TATIZO jipya..”ubongo fleva” wa majaji…najiuliza hili ni shindano la kuibua VIPAJI vya BONGO FLEVA tu..?mshiriki akiimba aina nyingine ya muziki anaambiwa abadili aimbe BONGO FLEVA…na nashangaa inaonesha wazi kuna baadhi ya nyimbo majaji hawazifahamu..itabaki kusubiri kwa TPF,” aliandika meneja wa vipindi wa Ebony FM ya Iringa, Renatus ‘Bizzo’ Kiluvia kupitia Facebook.

“Kwa mtazamo wangu nilikuwa naona,majaji kila mtu angepewa aina yake ya muziki na kabla hajapewa nafasi lazima ajue na aupende aina ya huo muziki vizuri na wasanii wake. Mfano mzuri BSS majaji,HIP HOP na nyimbo za dini wanadiss kinoma hata uimbeje, yote naona kama kukosekana mtu anaejua vizuri nyimbo hizo,” aliandika Noah Mwakalindile.

Maoni hayo yanaonesha jinsi tatizo hilo lilivyoonwa na watu wengi hivyo majaji wanatakiwa walizingatie hilo.

Mashindano haya yangewapika zaidi washiriki hawa ili wawe wanamuziki wa kimataifa kwa kuwapa uwezo wa kuimba nyimbo za aina mbalimbali na sio Bongo Flava tu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents