Makachero Waivuruga Tarime

Askari polisi anayeaminika kuwa wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kutoka mkoani Arusha, Emmanuel Zakaria, amekamatwa wakati akinunua kadi za uanachama katika ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Askari polisi anayeaminika kuwa wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kutoka mkoani Arusha, Emmanuel Zakaria, amekamatwa wakati akinunua kadi za uanachama katika ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Viongozi wa Chadema, walimkamata askari huyo jana, katika ofisi za chama hicho, zilizopo Mtaa wa Saronge mjini hapa.

Zakaria aliyekuwa amevaa nguo za kiraia, aliingia katika ofisi za Chadema mchana na kuomba auziwe kadi, lakini idadi yake haikujulikana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara (RPC), Liberatus Barlow, alisema polisi ina watumishi wengi, hivyo si rahisi kuzungumzia kwa undani kuhusu Zakaria.

“Polisi tuna watumishi wengi, sasa umejuaje kama huyo aliyekamatwa ni askari, na unataka kila kitu cha polisi lazima ukijue,“ alisema katika mahojiano kwa njia ya simu jana, ingawa hakufafanua.

Ofisa wa Chadema, Chacha Daniel Okong`o, akizungumza kwa niaba ya Katibu wa chama hicho wilaya ya Tarime, Joseph Antony, alisema wajumbe wa kikosi cha ulinzi cha Chadema, waliokuwa nje ya ofisi hiyo, walitoa taarifa zikielezea kuwa Zakaria ni askari polisi.

“Aliingia akaomba auziwe kadi, lakini kabla hajataja idadi, kuna vijana wetu walimtambua na kutuambia kwamba ni askari polisi, tukamuweka ndani na kuwapigia simu polisi, ndio hawa wamekuja, wamemtambua na kumchukua,“ alisema.

Magari mawili ya polisi aina ya Land Rover Defender, yakiwa na FFU wenye silaha za moto na mabomu ya machozi, walifika katika ofisi na kufanya mazungumzo na viongozi wa Chadema, kisha wakamchukua Zakaria na kuondoka naye.

Askari hao, walikuwa kwenye magari yenye namba PT 0947 na PT 1484, waliongozwa na Kamanda wa FFU Mkoa wa Mara, O.M Lyanga.

Kabla ya kuondoka katika eneo hilo, Lyanga alimshutumu Zakaria, kwa kile alichokiita kuwa ni “kuingia katika maeneo ya hatari.“

Naye Mwenyekiti wa chama cha DP, Christopher Mtikila, amesema ameanza kusambaza waraka wenye madai yanayohusu ripoti ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Zakayo Wangwe.

Wangwe alifariki katika ajali ya gari iliyotokea Julai 28, mwaka huu huko Pandambili mkoani Dodoma.

Waraka huo usio rasmi na usiotambulika na polisi, unataja majina ya watu mbalimbali na kuihusisha Chadema na kifo hicho.

Kamanda Barlow alithibitisha polisi kuuona waraka huo, na kusema jitihada za haraka zinafanywa ili kumhoji Mtikila.

“Hili halina ubishi, waraka huu umesambazwa na Mtikila, lakini tayari DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) ameunda kikosi kazi kitakachowasili mjini hapa wakati wowote,“ alisema.

Hata hivyo, Barlow alisema polisi haiwezi kumkamata na kumhoji Mtikila kuhusu waraka huo, kutokana na mazingira yanayotawaliwa na kampeni za ubunge na udiwani zinazoendelea jimboni hapa.

Alisema hatua ya kukamata na kuhoji inafanyika kwa kuzingatia matokeo ya mizania ya jeshi hilo, na kubaini tija ama madhara yanayoweza kutokea katika nyanja tofauti.

“Tunaweza kufanya uamuzi sahihi wa kumkamata na kumhoji mtu sahihi, kama ilivyo kwa Mtikila hapa, lakini suala la kutazama pia ni kuhusu wakati kama unaruhusu,“ alisema.

Aidha, Barlow alimuonya Mtikila kuiacha polisi kufanya kazi zake kwa uhuru na maadili yake, katika kuwashughulikia watu wanaotuhumiwa kumpiga kwa mawe hivi karibuni.

Mtikila alikaririwa akilishutumu jeshi hilo kwa madai ya kuwakamata watu wasiohusika katika shambulio hilo.

Mtikila alishambuliwa na kujeruhiwa akiwa jukwaani mjini hapa, alipodai kuwa kifo cha Wangwe kilisababishwa na Chadem

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents