Habari

Majaliwa awatumbua waofisa 4

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi maofisa misitu wanne, sambamba na kusimamisha shughuli zote za uvunaji wa mazao ya misitu wilayani Rufiji mkoa wa Pwani ili kupisha uchunguzi na kuweka mipango madhubuti ya kusimamia sekta hiyo.
majaliwapicha

Hatua hizo zilitangazwa Jumatatu hii mjini Rufiji, wakati Waziri Mkuu alipozungumza na watumishi wa wilaya ya Rufiji, kabla ya baadaye kuzungumza na wananchi kwenye ziara yake mkoani Pwani ya kukagua shughuli za maendeleo na kutoa maelekezo kwa watumishi wa sekta ya umma.

Waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Dk Paul Ligonja, Ofisa Misitu Wilaya, Gaudence Tarimo, Ofisa Misitu, Yonas Nyambua na Ofisa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wa Wilaya, Suleiman Bulenga.

“Kuanzia leo, nawasimamisha kazi watumishi hawa na geti la Ikwiriri liondolewe mara moja, ni kichaka cha wezi. Pia kazi za uvunaji misitu zisimame zote hakuna kuvuna hadi turatibu upya na kuangalia wapi pa kuvuna wapi si pakuvuna, maana misitu imekwisha na fedha zinaingia mifukoni mwa watu, serikali hainufaiki,” alisema Majaliwa.

Aidha, amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Njwayo kukusanya magogo yote yaliyopo misituni na kuyapiga mnada .

Aliitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda wilayani Rufiji, kufanya uchunguzi wa leseni za uvunaji magogo zilizotolewa ili kubaini zilizo halali.

“Rufiji ina sifa mbaya, inaongoza kwa uvunaji misitu bila kufuata taratibu na maofisa misitu wapo, hatuwezi kuendelea hivi,wasimame kazi,wizara itakuja kukagua na wale wasafi watarudi, wachafu njia hiyo nyeupe mwende,” alisema Waziri Mkuu.

Majaliwa ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na pia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji.

Chanzo:TBC

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents