Habari

Mahakama Kuu yazuia mali za Mbowe kupigwa mnada

Mahakama Kuu imezuia kupigwa mnada kwa vifaa vya kampuni ya Mbowe Hotels, inayomilikiwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kutokana na mzozo wa kodi ya pango baina ya kampuni hiyo na Shirika la Taifa la Nyumba (NHC).
Freeman-Mbowe

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Sivangilwa Mwangesi wakati akisikiliza maombi ya Mbowe Hotels Ltd dhidi ya NHC na kampuni ya udalali ya Fosters Auctioneers and General Traders.

Fosters ndiyo iliyopewa na NHC kazi ya kuondoa vifaa vya kampuni ya mbunge huyo wa Hai kutoka kwenye majengo yaliyoko Mtaa wa Mkwepu, ambako kulikuwa na klabu maarufu ya usiku ya Bilicanas na ofisi za Free Media, zote zikimilikiwa na mwanasiasa huyo.

NHC inadai kuwa Mbowe ameshindwa kulipa kodi ya pango ya Sh1.2 bilioni, jambo ambalo mwenyekiti huyo wa Chadema analipinga.

Katika maombi hayo, Mbowe anaiomba Mahakama iiamuru NHC na Fosters kumrejesha kwenye jengo hilo pamoja na mali na vifaa vyote vilivyochukuliwa na kampuni hiyo ya udalali.

Maombi hayo ya Mbowe yalikuwa yasikilizwe, lakini NHC waliweka pingamizi la awali wakiiomba mahakama iyatupilie mbali wakidai kuwa ni batili kwa kuwa yamefunguliwa chini ya kifungu cha sheria kisicho sahihi.

Kufuatia maombi hayo, mawakili wa Mbowe, wakiongozwa na Peter Kibatala, waliomba pingamizi hilo lisikilizwe kwa pamoja na maombi hayo.

Kibatala amesema maombi ni halali na kwamba kifungu cha sheria walichotumia ni sahihi kulingana na mazingira ya mgogoro huo.

Hata hivyo, mahakama iliamua kusikiliza pingamizi hilo kwanza.

Baada ya uamuzi huo, Kibatala aliomba mahakama itoe amri ya zuio la muda ili NHC isitekeleze azma yake ya kuzipiga mnada mali na vifaa hivyo.

Source: Mwananchi

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents