Mabadiliko makubwa Polisi

IGP MwemaJESHI la Polisi nchini limefanya mabadiliko makubwa ya kuwastaafisha kazi askari wake kwa mujibu wa sheria, huku wengine wakibadilishwa vituo vya kazi

 

 

IGP Mwema

 

 

 

na Kulwa Karedia

JESHI la Polisi nchini limefanya mabadiliko makubwa ya kuwastaafisha kazi askari wake kwa mujibu wa sheria, huku wengine wakibadilishwa vituo vya kazi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kwa niaba ya Mkuu wa jeshi hilo, Inspekta Jenerali (IGP) Said Mwema, Kamishina wa Utawala na Fedha wa jeshi hilo, Clodwing Mtweve alisema mabadiliko hayo yamegusa askari 700 wa ngazi zote wakiwamo wale ambao muda wao wa utumishi unatarajia kukoma Julai mosi, mwaka huu.

Alisema mabadiliko hayo yanawagusa makamanda wa polisi wa mikoa, wilaya na wakuu wa upelelezi wa mikoa na wengine kutokana na nafasi zao walizonazo.

Mtweve alisema makamanda wanaostaafu ni pamoja na Kamishina wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishina Msaidizi wa Polisi, David Saibullu.

Alisema katika mabadiliko yanayofanywa, nafasi ya Tibaigana inachukuliwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Suleiman Kova, wakati nafasi ya Kamanda Saibullu itachukuliwa na Kamishina Msaidizi wa Polisi, Leberatus Barlow, ambaye alikuwa Ofisa Mnadhimu Utawala na Fedha Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Kwa upande wa uhamisho wa makamanda wa mikoa, Kamishina Mtweve alisema aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Zelothe Stephen, amehamishiwa Mbeya na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow amehamishiwa Mwanza.

Alisema ACP Mark Kalunguyeye, aliyekuwa Kanda Maalum ya Dar es Salaam amepandishwa na kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, wakati ACP Ray Karama, aliyekuwa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Kanda Maalum ya Dar es Salaam, sasa anakuwa Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Wezi na Mifugo kilicho na makao makuu yake Arusha.

Wengine ni ACP Abdallah Msika, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, ambaye amehamishiwa Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam, huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Salewi amehamishiwa mkoani Kagera kushika nafasi ya Mssika.

Nafasi ya Salewi imechukuliwa na ACP A. Mwakyoma kutoka Makao Makuu ya Polisi.

Mabadiliko hayo pia yamemgusa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP M. Mshihili, aliyehamishiwa Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam, wakati nafasi yake ikichukuliwa na ACP Emson Mmari, kutoka Makao Makuu ya Upelelezi.

Kamishina Mtweve alisema wengine waliokumbwa na mabadiliko hayo ni ACP Lucas Kusima kutoka Baraza la Ulinzi na Usalama aliyepelekwa makao makuu, ACP Brown Lekey kutoka Makao Makuu ya Upelelezi kwenda Baraza la Ulinzi na Usalama Dar es Salaam, huku SSP Mary Nzuki aliyekuwa OCD Dodoma, akiwa Kaimu Kamanda wa Polisi Tazara na SSP Lucy Makelemo aliyekuwa OCS Uwanja wa Ndege Mwanza, akipandishwa kuwa Staff Officer 1, Dar es Salaam.

Pia mabadiliko hayo yamewagusa wakuu wa upelelezi wa mikoa (RCO) ya Mara, Kigoma, Shinyanga na Mbeya wanaotarajia kustaafu.

Kwa upande wa Mkoa wa Kigoma, RCO atakuwa SSP Msato Marijani, ambaye alikuwa OCD Wilaya ya Biharamulo, huku SSP Deusdit Kato aliyekuwa OCD Central Dar es Salaam amepelekwa Mkoa wa Mara.

Katika hatua nyingine, Kamishina Mtweve alisema jeshi hilo limefungua tovuti yenye anwani ya www.policeforce.go.tz na kuwasihi wananchi kuitumia kwa kutuma maoni na taarifa mbalimbali na kujisomea taarifa mbalimbali zihusuzo shughuli za jeshi hilo.

 

 

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents