Siasa

Lipumba arejea nchini, azungumzia ufisadi BoT

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amelishauri Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuunda kamati teule ya kuendeleza uchunguzi dhidi ya ufisadi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Na Dunstan Bahai

 
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amelishauri Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuunda kamati teule ya kuendeleza uchunguzi dhidi ya ufisadi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

 

Profesa Lipumba alitoa kauli hiyo jana kwenye mkutano wa hadhara Jangwani jiji Dar es Salaam muda mfupi baada ya kurejea nchini akitokea nchini Uswisi ambapo alilakiwa na umati mkubwa wa wafuasi wa chama hicho.

 

Septemba, mwaka jana, Profesa Lipumba aliteuliwa na Umoja wa Mataifa kuungana na timu ya wataalam wa Shirika la Maendeleo na Biashara la Umoja huo kupanga program za kushughulikia masuala ya umaskini katika nchi 50 duniani ikiwemo Tanzania.

 

Akizungumzia kuhusu kamati hiyo ya Bunge ya kuchunguza ufisadi, Profesa Lipumba alisema ni muhimu kwani wabunge ni wawakilishi wa wanachi hivyo, hawawezi kufanya udanganyifu.

 

Kuhusu ufisadi ulioibuliwa BoT, Profesa Lipumba alisema mashirika makubwa ya fedha duniani ndiyo yaliugundua na hivyo kuishinikiza serikali kufanya ukaguzi.

 

Aidha, aliishauri serikali kuondoa `uozo` uliopo ndani ya benki hiyo ili kutoa fursa nzuri kwa Gavana mpya kufanya kazi vizuri.

 

“Tumpongeze Rais Jakaya Kikwete kwa kumteua Profesa Benos Ndulu kuwa Gavana�huyu bwana namfahamu ni mchapa kazi mzuri, lakini hawezi kufanikiwa katika malengo ya kuiboresha BoT kama serikali haitawasafisha mafisadi waliobakia,“ alisema. huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu.

 

Hata hivyo, alisema hayo hayawezi kufanikiwa ikiwa madai yao ya kutaka Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi hayatafanyiwa kazi.

 

“Watu walisema sirudi, lakini leo nimerudi, tutahakikisha madai yetu ya Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi yanafanyiwa kazi,“ alisema.

 

Wananchi wengi waliohudhuria mkutano huo walikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua maendeleo ya mazungumzo ya kutafuta muafaka, lakini viongozi wote wakuu wa CUF waliokuwepo hakuna hata mmoja aliyezungumzia.

 

Profesa Lipumba alisema Watanzania hawafaidiki na maliasili zilizopo na kwamba ili serikali iwakwamue wananchi wake katika dimbwi la umaskini, iboreshe kilimo na kukuza ajira.

 

Alisema katika vikao vyao huko Uswisi, program kubwa waliyokuwa wanaona ni njia muafaka ya kuondoa umaskini katika nchi hizo 50, ni kuboresha miundombinu na kilimo.

 

Kuhusu ghasia za Kenya, Profesa Lipumba alisema kama viongozi wa Afrika Mashariki wangejifunza matukio ya Zanzibar na Pemba ya Januari 26 na 27, mwaka 2001, yanayotokea hivi sasa nchini huko, yasingetokea.

 

Pamoja na mapokezi hayo, CUF pia jana kilitumia tukio hilo na kumbukumbu ya kuwakumbuka wanachama wao waliopoteza maisha Zanzibar katika tukio hilo la Januari 21, mwaka 2001.

 

Mapokezi hayo yalihudhuriwa na viongozi wote wakuu wa CUF, wabunge wa upinzani na viongozi wa ushirika wa vyama hivyo unaofanywa na CUF, CHADEMA, TLP na NCCR-Mageuzi.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents