Habari

Linah na Makomando wazungumzia moto watakaouwasha kwenye Fiesta Iringa leo

Msanii nyota wa kike wa muziki wa kizazi kipya, Linah Sanga ‘Linah’, leo ataungana na kundi la Makomando kutoa burudani ya nguvu katika tamasha la Serengeti Fiesta litakalofanyika katika Uwanja wa Samora, mkoani Iringa.
Tamasha hilo limetua mkoa huo aliotoka Linah, ikiwa ni baada ya kuchengua maelfu ya wapenzi wa burudani kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora.

Mwanadada Linah akifanya yake

Katika tamasha hilo linalokwenda kwa kaulimbiu ya “Sambaza upendo” wasanii wakali zaidi ya 12 watapanda jukwaani kuwapagawisha wakazi wa mkoa huo.

“Tulifanya shoo ya aina yake Tabora na Geita na ni matarajio yangu kwamba mashabiki wa burudani wa mkoa wangu (Iringa) watazifunika shoo zote mbili zilizopita kwa kuhudhuria kwa wingi kumsapoti msanii kutoka mkoa wao,” alisema Linah. Kwa upande wao, Makomando wanaotamba na wimbo wao waliotoa hivi karibuni ambao umekuwa gumzo kwa sasa katika maeneo mbalimbali ukienda kwa jina la ‘Linah wa Mama’.

Wakali hao wa mtindo wa Kibaba baba, wameelezea kufurahishwa kwao kwa kupanda jukwaa moja na Linah na kuimba naye, wakitarajia mashabiki wao kupata burudani ya hali ya juu.

Wasanii wengine watakaotumbuiza katika tamasha hilo ni Juma Nature, Godzilla, Afande Sele, Young Killa, Madee, Mr Blue, Vanessa, Ommy Dimpoz, Mo Music, Baraka Da Prince na Ibra wa mkoani Iringa anayetamba na wimbo wa ‘Msela.’

Mbali ya tamasha hilo, kutakuwa na matukio kadha wa kadha kama bonanza la soka na dansi la Fiesta ambapo washindi watapata fursa ya kutua Dar es Salaam kushuhudia shoo ya mwisho ya Fiesta inayotarajiwa kufanyika Oktoba 18, mwaka huu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents