Burudani

Kwenye hili la Nay wa Mitego nimeona haya mambo nane

Wikiendi iliyomalizika ilikuwa na vugu vugu kubwa katika muziki wa Bongo Flava. Macho na masikio yalielekezwa kwa msanii Nay wa Mitego mara baada ya kukamatwa na polisi akiwa mkoani Morogoro.

Kila mtu alitaka kujua nini kinaendelea kuhusu yeye, hatimaye jana suala lake likamalizika na kuachiwa huru ili kuendelea na muziki wake. Katika suala lake kwa akili ya kawaida tu, niweza kuona haya mambo nane yafuatayo.

1. Muziki ni timing

Jana mtandao huu (Bongo5) uliandikia kuhusu wasiwasi walionao wasanii kwa wakati huu kuogopa kutoa nyimbo kutokana upepo wa kisiasa uliyopo ambao umewazoa hadi vijana ambao ndio ‘walaji’ wakuu wa muziki huu wa Bongo Flava. Swali la kujiuliza kwa nini Nay wa Mitego hakuogopa kutoa wimbo wake, jibu ni kwamba aliangalia ni kitu gani (current issue) ambacho akikiandikia kwa sasa mapokezi yake yatakuwa makubwa. Sidhani kama umenielewa.

Tembea na huu mfano, hayati Lucky Dube mfalme wa miondoko ya reggae barani Afrika hadi leo anakumbukwa kwa tungo zake zilizotukuka. Sababu ya wengi kumkumbuka na kumuenzi si kwamba alijua kuimba sana au alikuwa na muoneno mzuri (handsome), lah hasha bali muziki wake uligusa maisha ya wengi kwa wakati huo.

Wakati bara la Afrika linapigana dhidi ya ukoloni, wakati taifa la Afrika Kusini alipozaliwa linapigana kuuondoa utawala wa Makaburu. Unapotengeneza muziki unaogusa maisha ya watu na yale mambo wanayokumbana nayo kwa wakati huo ni rahisi kupenya na kuwafikia.

Kuna wimbo wa kundi la Weusi umetoka unaitwa ‘Madaraka ya Kulevya’ nao unakuja kwa kasi kubwa kutokana na maudhui yake na hali ya kisiasa ilivyo sasa, ingawa wimbo hauna uhusiano wa moja kwa moja na jambo tajwa ila kwa mujibu wa tafsiri za wengi ni kwamba Weusi wamelenga penyewe.

Pia nimesikia wimbo wa Rapa Baghdad uitwao ‘Usinipangie’ akiwa amechukua neno hili kutoka kwenye moja ya hotuba za Rais Dkt. Magufuli. Neno hili limekuwa linazunguka sana kwenye mitandao ya kijamii, na hata kutumika kama utani. Huu ndio mtindo wa kutoa wimbo kwa sasa, kama ulikuwa na wimbo wako ambao hagusi moja kwa moja yanayozunguzwa sasa inabidi uwe mpole kwanza.

2. Bongo Flava inagusa siasa

Kuna siku Rais Dkt. John Magufuli katika ziara yake mkoani Mtwara kwenye mazungumzo yake aligusia wimbo wa Darassa ‘Muziki’ kitu kilichofurahisha wengi. “Mkiambiwa changanya kama karanga ndio mnachanganyikiwa kabisa,” hayo yalikuwa maneno ya Rais Dkt. Magufuli na kufuatiwa shangwe kubwa uwanjani hapo. Hiyo ndiyo nguvu ya Bongo Fleva kwa sasa.

Katika hili la Nay wa Mitego nimeona vingozi mbali mbali wa kisiasa wakilijadili kupitia mitandao ya kijamii. Mbunge wa Kigoma Mjini na kiongozi wa cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kupitia mtandao wa Twitter aliandika, “Rais hana mamlaka yoyote kuamua wimbo uchezwe au usichezwe, ilikuwa ni makosa kumkamata Nay na agizo la Rais halina maana pia.”.

Aliyekuwa waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye naye hakuwa mbali. “Matumizi ya nguvu hayalipi! Kurekebisha kwa upendo hulipa! Hongera Rais, Hongera Mwakyembe kwa uamuzi wa busara dhidi ya muziki wa Ney!,” aliandika kupiti Twitter. Mbunge wa Kawe, Halima Mdee naye kupitia Twitter alisifia wimbo wa Weusi ‘Madaraka ya Kulevya, “Madaraka ya KULEVYA- WEUSI!!! Mmetishaa!!!!.”

Kwa mifano hiyo kadhaa utaona ni kwa namna gani muziki umevuka mipaka, si tu kwa vijana bali hata kwa viongozi wa kisiasa. Shikamoo Bongo Flava.

3. Mtihani wa pili kwa Dkt Mwakyembe

March 24 mwaka huu ndio Dkt Harrison Mwakyembe alikabidhiwa kijiti cha kuiongoza Wiraza ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoka kwa Nape Nnauye. Mtihadi wa kwanza ambao ulikuwa unamkabili Mwakyembe ni kuhusiana na ripoti ya kamati ambaye aliiunda mtangulizi wake, yaani Nape kuhusiana na kiongozi mmoja kudaiwa kuvamia studio za Clouds Media Group. Mwakyembe aliahidi kufuatilia suala hilo kwa kusikiliza upande wa pili katika shauri hilo ambao alidai haukupewa nafasi katika ripoti hiyo, hivyo kwa kiasi fulani mtihani huu yupo mbioni kuushinda.

Kuibukua hili la Nay wa Mitego na kushikiliwa na polisi ulikuwa ni mtihani mwingine kwake, kwani yeye kama waziri mwenye dhamana ya sanaa alitakiwa kuhusika moja kwa moja, aidha kwa kutetea au kuhakikisha hatua za kinidhamu zinachukuliwa kwa mhusika. Lakini baada ya tamko lake la jana pamoja kauli ya Rais Dkt. Magufuli ni kama suala hilo limemalizika, hivyo mtihani huo kwa Mwakyembe haupo tena.

4. Inawezekana kuwa na hit song bila video

Kwa sasa bila ubishi wimbo wa Nay wa Mitego ‘Wapo’ tayari ni hit bila hata ya kuwa na video. Kwenye hili ngoja nikueleza mambo mawili. Mosi: kumekuwepo na malalamiko kuwa wasanii wengi wa sasa wanawekeza fedha nyingi katika uandaaji wa video na kutozingatia upande wa audio kitu kinachoua muziki.

Pili: kwa sasa umekuwa ni mtindo wa kawaida msanii kuachia wimbo pamoja video yake ikiaminiwa ni moja ya sababu ya kuufanya wimbo kuwa hit. Wengine hutoa kwanza wimbo kisha kusikilizia na wakiona matokeo si mazuri hutoa video kama njia kuuboost muziki wake. Yote haya mawili yanawezekana lakini potelea mbali, sio deni. Nay wa Mitego kakiuka kanuni hizo mbili nilizotangulia kuzitaja na bado wimbo wake kuwa hit hadi kusifiwa na Rais Dkt. Magufuli. Hivyo wasanii wajielekeze zaidi kwenye utunzi kabla ya kuwaza video za gharama kubwa.

5. Nguvu ya mitandao ya kijamii

Takwimu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha watumiaji wa intaneti nchini wameongezeka hadi kufikia milioni 20 ikiwa ni sawa na asilimia 40 ya watanzania wote. Idadi hii inazidi kuongezeka kila siku, mwaka 2014 walikuwa watumiaji milioni 24 sawa na asilimia 29, mwaka 2015 milioni 17 sawa na asilimia 34.

Kundi hili la watu milioni 20 kuna uwezekano mkubwa wakawa watumiaji wa mitandao ya kijamii. Kama ni hivyo basi, mitandao ya kijamii kwa hapa nchini nguvu yake ni kubwa na inazidi kuongezeka. Wimbo wa Nay wa Mitego haukupelekwa wala kuchezwa katika chombo chochote cha habari lakini umekuwa hit hadi kufika Ikulu. Kwa sasa wasanii wana uwanja mpana wa kutangaza kazi zao ukilinganisha na hapo awali, hivyo ni vema kutumia fursa hiyo.

6. Nay wa Mitego hakui kwa Basata

Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) ndio kama Baba mlezi wa sanaa yetu, hivyo ana wajibu kukuza wasanii na kutoa maonyo kila mara bila kuchoko. Waswahili walisema mtoto akiunyea mkono haukati bali unapanguza na maisha mengine kuendelea. Mantiki ya mfano huo ni kwamba, licha ya adhabu ya kufungia kwa wimbo wa Nay wa Mitego kufutwa, si mara ya kwanza msanii huyu kukumbana na adhabu kama hiyo.

Wimbo wake uitwao ‘Niwachane’ uliotoka mwaka jana ulifungiwa licha ya kuaza kuchezwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari. Lakini la kushangaza kuhusu Nay wa Mitego na Basata, ni kwamba msani huyu kila akipewa adhabu amekuwa akikumbana na aina fulani ya msamaha, yaani tunaweza kusema anaokota dodo chini ya mnazi. Baada ya kutoa wimbo wake uitwao ‘Pale Kati Patamu’ alifungiwa kutojihusisha kabisa na shughuli za kisanaa, lakini baadaye alipokuja kukuaa na kuzungumza na Basata aliondolewa adhabu hiyo na kuamriwa kufanya marekebisho ya wimbo huo, hivyo kuwa huru tena kufanya muziki wake.

7. Umoja wa wasanii

Baada ya taarifa kutoka hiyo juzi kuwa Nay wa Mitego amekamatwa mkoani Morogoro, wasanii wengi wa Bongo Flava walionesha masikitikio yao kupitia mitandao ya kijamii huku wengi wakihoji kwanini inafikia hatua hiyo kabla hata ya Basata kuzungumza. Miongoni mwa wasanii hao ni pamoja na One The Incredible, Nick wa Pili, Barakah The Prince, Prof Jay, Ice Boy, Kala Jeremiah na wengineo. Huu ni moja ambao ni mara chache kushuhudia lakini kwenye hili limewezekana.

8. New school wajifunze kutoka old school

Mbunge wa jimbo la Mikumi Morogoro, Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay amejizolea umaarufu mkubwa kwa tungo zake zenye mafunzo na kukosoa. Utakumbuka wimbo kama Ndiyo Mzee, Kikao cha Zarura na Nang’atuka ziliilenga serikali moja kwa moja lakini uwasilishaji wa tuko zake ulikuwa wenye staha zaidi. Hii ndiyo sababu ya wananchi wa Mikumi kuamini Profesa Jay anaweza kuwa kiongozi wao na kumpa jukumu la kuwaongoza.

Twende twende nyuma, licha ya wimbo wa Nay wa Mitego ‘Wapo’ kuruhusiwa lakini bado maudhui yake si mazuri, yaani lugha iliyotumika si ya staha kiujumla na ameshindwa katika mambo mawili. Mosi: hakutumia lugha ya kisanaa ambayo ndani yake ina mafumbo zaidi, pili: ameshindwa kuficha hisia zake. Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ mmoja wa waanzilishi wa muziki wa kizazi kipya ambaye kwa sasa ni mbunge wa Mbeya Mjini aliwahi kuandika wimbo uitwao ‘Mikono mwa Polisi’ hii ni mara ya baada ya mwanafunzi mmoja huko Mbeya kuuwa akiwa kwenye maandamano. Lengo la Sugu kuandika wimbo huu ni kuileza serikali kuwa kilichotokea hakikuwa sawa na waliosababisha kifo cha huyo mwanafunzi wachukuliwe hatua. Wimbo hadi sasa zaidi ya miaka 10 unachezwa kwenye redio wala hajawahi kufungiwa.

Wasanii wa kizazi cha sasa (new school) wanapaswa kujifunza kutoka kwa wale wakongwe waliowatangulia. Wajue namna ya kukosoa kwa staha na kujenga hoja katika yale mambo ambayo wamelenga kuyafanyia mapinduzi, hiyo ndio maana ya sanaa.

Na Peter Akaro
Contact: 0755 299596

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents