Bongo5 MakalaBurudani

Kuchi Kuchi (Oh Baby) wimbo wa mwaka 2011 unaohit sasa Tanzania

Kama Joy Odiete maarufu kama Jodie akitua nchini leo, atashangaa mno kusikia wimbo wake wa mwaka 2011, Kuchi Kuchi (Oh Baby) ukichezwa kwenye mitaa ya mikoa karibu yote ya Tanzania.

jodie

Atakachoshangaa zaidi ni kwamba hata watu wa kijijini kabisa wanaufahamu wimbo wake na wengi wameuweka kwenye simu zao za mkononi kama muito wa simu ama kama wimbo wa kuwaburudisha wanapokuwa wamejituliza sehemu. Kama umesafiri na mabasi ya kwenda mikoani utakuwa umeiona video hiyo ikichezwa kwenye screen ndogo ya basi ulilosafiria.

Kwa maeneo ya vijijini, hakuna pikipiki ya abiria (bodaboda) isiyoucheza wimbo huo kwenye redio ndogo zilizofungwa kwenye pikipiki hizo za kichina. Kwa sasa haiwezi kupita siku bila kuusikia wimbo huo ukichezwa kwenye kituo cha redio unachopenda kusikiliza.

Hizo ndio sifa za hit single. Wimbo unaopata umaarufu na kupendwa na watu wa aina mbalimbali na tena bila kuzingatia umetoka zamani ama mpya. Pamoja na kuwa wimbo wa mwaka 2011, kwa masikio ya wengi, wimbo huo ndio kama umetoka jana.

Kwa ufupi ni kuwa, wimbo wa Jodie ni mkubwa nchini Tanzania kuliko hata ukubwa wa jina lake mwenyewe. Nina uhakika, watu wengi hata hawamjui sura yake, labda tu kwa wale waliokwisha kuiona video.

Binafsi, wimbo huu nimeufahamu mwanzoni kabisa mwa mwaka 2012. Niliufahamu baada ya kudownload nyimbo nyingi za Kinaijeria, ukiwemo Chop My Money (original) wa P-Square. Nilipousikia wimbo huu, moja kwa moja niliupenda sana na nakumbuka kipindi hicho nilikuwa nafanya kazi kwenye kampuni mpya iliyokuwa na radio ya online (mara baada ya kuondoka Radio Free Africa).

Amini usiamini, kipindi naupata wimbo huo, hakuna redio wala mtangazaji yeyote wa Tanzania aliyekuwa anaufahamu wimbo huo, hilo nina uhakika nalo. Pengine kama bado ningekuwa mtangazaji wa RFA, wimbo huo ningeanza kuucheza mimi kwenye redio mwanzoni mwa mwaka 2012.

Hata kwa Jodie, msichana aliyeshiriki mashindano ya Nigerian Idol na kuingia fainali japo hakushinda, Kuchi Kuchi ulikuwa ni wimbo uliomshangaza kwa jinsi ulivyokubalika na ilimchukua muda kiasi kuachia wimbo mpya.

Katika mahojiano aliyofanya na gazeti la Daily Independent mwaka 2012, Jodie alisema baada ya Kuchi Kuchi wengi walikuwa na matarajio makubwa kutoka kwake. “Watu walianza kutarajia mengi kutoka kwangu, walianza kutarajia makubwa. Na sikuwaangusha. Baada ya hit kama ile, sikutakiwa kuja na album mbovu. Si tena kuhusu mimi, ni kuhusu maelfu ya watu waliovutiwa na nyimbo zangu na brand yangu.Fikiria kununua album sababu ya wimbo wa Kuchi Kuchi na unakuta ni Kuchi Kuchi pekee unaoeleweka na zingine zote sio nyimbo nzuri, lazima utakuangushwa.”

Baada ya Kuchi Kuchi, Jodie aliachia wimbo mwingine uitwao ‘Under the Mango Tree’ ambao nao ulihit. Kwa mujibu wa Jodie, Kuchi Kuchi ni sauti na sio neno na ni wimbo maalum kwa mtoto japo hakuimba kwaajili ya mtoto wake kwakuwa hana mtoto bado. “Ni sauti inayoeleza upendo kati ya mama na mtoto.”

Jodie anasema pamoja na Kuchi Kuchi kumpa mafanikio makubwa ya kiuchumi, wimbo huo umemkuza kiakili pia.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents