Tragedy

Updates: Ukweli wa habari ya kijana (Gabriel Munisi) aliyefanya mauaji Ilala naye kujiua kwa risasi (Audio)

Dada wa Christina Alfred Newa, msichana aliyenusurika kuuawa na aliyekuwa mchumba wake, mfanyabiashara wa magari jijini Mwanza, Gabriel Munisi (35), aliyejiua juzi baada ya kuua watu wawili na kujeruhi wengine wawili jijini Dar es Salaam katika tukio linalohusishwa na wivu wa mapenzi, amezungumza na kukanusha baadhi ya habari zilizoandikwa na magazeti na blogs nchini.

1424343_755264624500789_596758088_n
Marehemu Gabriel Munisi

Awali, gazeti la Mwananchi liliripoti kuwa Munisi aliamua kufanya mauaji hayo baada ya mchumba wake Christina kupata mpenzi mpya, Francis Shumila ambaye ni Mkenya. Kwa mujibu wa dada yake na Christina na Alpha aliyeuawa, aitwaye Caroline Newa, Francis Shumila aliyejeruhiwa kwenye tukio hilo na kufariki jana, ni mume wake na wala sio mpenzi wa Christina kama vyombo vya habari vilivyoripoti.

“Mimi Caroline Newa kwanza nianze kulalamika kwamba taarifa nyingi zilizotolewa si za kweli. Waliochukua hizo habari, hawakupata watu sahihi wa kuwapatia hizo habari,” Caroline ameiambia Power Breakfast ya Clouds FM leo asubuhi.

Amesema tukio hilo lilitokea kwenye nyumba ya familia yao ya Mzee Alfred Newa, yenye watoto wanne, Caroline, Christina ambaye jina lake jingine ni Nandomondo, Alpha na kaka yao Aloy ambapo yeye alikuwa amesafari lakini wengine wote walikuwepo hapo nyumbani akiwemo mama yao, Bi. Hellen Newa na mume wake Francis Kiranga Shumila ambaye ni nahodha wa meli.

Amesema mdogo wake Christina alikuwa amesitisha uhusiano na Munisi kutokana na mateso aliyokuwa akiyapata kutoka kwa mpenzi wake huyo.

“Na mara ya mwisho kusitisha uhusiano huo, ilibidi sisi kama familia tuhusishe polisi ya Dar es Salaam pamoja na polisi ya mkoa wa Mwanza kwenda kumuokoa Christina Newa kutoka kwenye nyumba ya Gabriel Munisi ambako alikuwa amemfungia kwa wiki nzima akimtesa, akimpiga, akimfungia ndani na kumtishia bastola kwamba atamuua,” amesema Carol.

Caroline ameeleza kuwa Munisi alikuwa akitoa vitisho hivyo mara kwa mara na hata katika makosa madogo.

“Kutokana na kuachwa na Christina, Gabriel Munisi alikuwa na hasira sana kwakuwa amekuwa anakuja. Jengo la pili kutoka nyumbani kwetu hapa Ilala Sharishamba ni hoteli inaitwa Double M, ni ghorofa sisi nyumba yetu ni ya chini. Amekuwa anakuja anapanga kwenye hiyo hoteli huko juu anakaa anatuchunguza. Na hii juzi huyo Christina Nandomondo Newa alikuwa anarudi Cyprus mchana wake. Mimi nilikuwa safari Moshi. Mume wangu alikuwa anaendesha gari Captain Francis Kiranga Shumila, pembeni yake alikuwa amekaa mdogo wangu aliyekuwa anafanya kazi Barclays, marehemu Alpha Alfred Newa, halafu nyuma alikuwa amekaa Christina Nandomondo Newa, mdogo wangu mwingine pamoja na mama yangu Hellen Newa, wakiwa wanatoka pale wamuache Alpha kazini kwake Barclays, wakitoka hapo Nando amalizie shopping zake za mwisho apelekwe airport.

Lakini sasa kwa bahati mbaya wakiwa wanataka kuondoka wameshafunga geti kila kitu, kilichotokea Gabriel Munisi alitoka kusikojulikana na kuanza kuwashambulia, akawashambulia sana kwa risasi na yeye akajiua.”

IMG-20131119-00045-1024x768
Gabriel Munisi baada ya kujiua kwa risasi juzi

Caroline anasema pamoja na familia kuripoti polisi vitisho vya mauaji vilivyokuwa vikitolewa na Munisi, polisi waliwadhihaki na kukataa kuchukua hatua yoyote.

“Tulioneakana kwamba sisi ni wazushi,” amesema Carol.

Amesema siku ya tukio, mdogo wake Christina alimpigia simu kumueleza yaliyotokea na jinsi Gabriel alivyotimiza kile alichokuwa akikisema mara kwa mara na kwamba kutokana na kuwa na pressure aliamua kuiweka kimya simu yake na kuomba asiambiwe kitu. Jana alipokuja ndipo alipoelezwa na majirani kuhusiana na taarifa za kupotosha zilizoandikwa na vyombo vya habari kuhusiana na tukio hilo.

“Mimi hapa nilifika usiku na nilikuwa sina nguvu, jana tena mume wangu amekata roho, Kapteni Shumila, kwahiyo pia jana hali yangu haikuwa sio nzuri. Leo asubuhi nimeamka kusali ndio nimeoneshwa baadhi ya magazeti na blogs. Nikapatwa na mshangao, cha kwanza kabisa nilichoona majina yamekosewa, cha pili nikaona facts ziko twisted.”

Caroline amesisitiza kuwa ana uhakika hakuna mwaandishi wa habari aliyefika nyumbani kwao kupata habari za uhakika kuhusiana na tukio hilo.

“Mimi naona sio sawa,” amesema.

Tunaipa pole familia ya Alfred Newa kwa tukio hilo.

Msikilize Caroline hapa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents