Habari

Kijana ahukumiwa miaka 7 jela kwa kumng’oa meno mwanawe

Mahakama ya Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam imemhukumu Elihsa Sumila (35) kutumikia kifungo cha miaka saba jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumjeruhi mtoto wake na kumsababishia meno mawili kung’oka.
b3707b7114b39836997b34181db60f3f

Akisomewa hukumu hiyo juzi Hakimu Mkazi, John Msafiri alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka baada ya kuleta mashahidi watano akiwemo daktari.

Msafiri alisema baada ya kusikiliza ushahidi huo ameweza kujiridhisha na mashitaka hayo bila kuacha shaka yoyote.

Akisoma baadhi ya ushahidi uliotolewa mahakamani hapo alisema mshitakiwa alimpiga mtoto wake ngumi ya mdomoni na kusababisha meno mawili kung’oka na kuongeza kuwa sababu za kumpiga mtoto huyo inatokana na kupewa taarifa kwamba alikuwa ni mtoro shuleni.

“Baada ya kurudi nyumbani baba mtoto alianza kumpiga kwa fimbo kwenye mwili na kumsababishia maumivu,” alisema .

Wakili wa serikali Sylvia Mitanto aliiomba mahakama impe adhabu kali mshitakiwa kwani kitendo cha kunyanyasa watoto ni kibaya na hakikubaliki na pia amemsababishia mtoto wake ulemavu wa kudumu.

Mshitakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwani kosa hilo amelifanya bahati mbaya.

Hakimu alisema mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka saba jela.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti, 2014 maeneo ya Ukonga Mazizini wilayani Ilala kwa kumjeruhi mtoto wake kwa kumpiga na fimbo sehemu mbalimbali za mwili na mgumi mdomoni ambapo alisababisha meno mawili kutoka.

Source: Habari Leo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents