Siasa

Kibaki akubali yaishe

TOFAUTI zilizopo kati ya Serikali na chama cha upinzani cha ODM sasa zinaweza kupungua na hatimaye kwisha.

NAIROBI, Kenya

 

TOFAUTI zilizopo kati ya Serikali na chama cha upinzani cha ODM sasa zinaweza kupungua na hatimaye kwisha.

 

Hiyo ilijitokeza juzi baada ya Rais Mwai Kibaki kukutana na ujumbe mzito wa Umoja wa Ulaya (EU) na kusema yuko tayari kukutana na kiongozi wa ODM, Bw. Raila Odinga haraka iwezekanavyo.

 

Ujumbe huo pia ulitangaza kuwa utasubiri kusikia matokeo ya mazungumzo ya viongozi hao wawili, kabla haujachukua hatua yoyote.

 

Kamishna wa EU, Bw. Louis Michel, alisema Umoja huo haujafikia uamuzi wa kuchukua hatua yoyote mpaka sasa kuhusu hali ya kisiasa nchini Kenya.

 

Akizungumza juzi kwenye mkutano uliojumuisha mawaziri, Rais Kibaki alisisitiza kuwa sasa yuko tayari kwa mazungumzo ili kuondokana na hali mbaya ya kisiasa iliyoigubika nchi.

 

Kamishna Michel alisema Kenya ni nchi muhimu katika eneo hii la Afrika, kwa kuzingatia ukweli kuwa imekuwa mfano dhahiri wa demokrasia iliyokomaa na nguzo ya utulivu katika Afrika.

 

Aliipongeza Kenya kwa kuendesha upigaji kura kwa amani, lakini akalaumu ghasia zilizojitokeza baada ya uchaguzi.

 

Alisema ikiwa rafiki wa Kenya, EU ina matumaini kwamba hali ya sasa kisiasa nchini itatengemaa kupitia mazungumzo ya kisiasa.

 

Akiunga mkono juhudi za watu mashuhuri wa Afrika, Kamishna huyo alisema suluhisho la tatizo la kisiasa la Kenya, halina budi kumalizwa na Wakenya wenyewe.

 

Alisema ingawa Bunge la Ulaya limepitisha azimio ambalo si zuri kwa Serikali ya Kenya, “EU haitachukua hatua yoyote dhidi ya Kenya, lakini itasubiri matokeo ya mazungumzo.”

 

Hata hivyo, Rais Kibaki alisema aina yoyote ya ghasia dhidi ya Wakenya wasio na hatia, haitavumiliwa.

 

“Usalama wa nchi ni muhimu, na Serikali itaendelea kuimarisha usalama katika maeneo yaliyoathirika ili kuhakikisha maisha ya wananchi na mali zao yanalindwa,” alisema Rais Kibaki.

 

Kamishna Michel alifuatana na Mwakilishi wa EU nchini Kenya, Bw. Eric Van Der Linden na Balozi wa Ufaransa nchini, Bibi Elizabeth Barbie.

 

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Waziri wa Mambo ya Nje, Bw. Moses Wetangula na Waziri wa Fedha, Bw. Amos Kimunya, Mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu wa Baraza la Mawaziri, Bw. Francis Muthaura na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Thuita Mwangi.

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents