Habari

Kesi ya Masogange yaahirishwa hadi Aprili 20, apewa onyo baada ya kuchelewa Mahakamani

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemtaka msanii Agnes Gerald maarufu kama Masogange (28), anayekabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya, kuheshimu masharti ya dhamana.

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbroad Mashauri, alitoa rai hiyo Jumanne hii baada ya video queen huyo kutokuwepo mahakamani wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa kutajwa.

Awali, Wakili wa Masogange, Nictogen Itege alidai mshitakiwa huyo alikuwa njiani akija mahakamani hapo.

Hata hivyo, hakimu alimhoji wakili huyo mbona yeye (Itege) yuko mahakamani hapo, ambapo alimjibu walipita njia tofauti na Masogange.

Baada ya kueleza hayo, hakimu Mashauri alimweleza wakili huyo amwambie mteja wake anatakiwa aheshimu masharti ya dhamana.

Upande wa jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Aldof Mkini, ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo liahirishwe hadi tarehe nyingine kwa kutajwa. Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 20, mwaka huu kwa kutajwa.

Muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa shauri hilo, Masogange alionekana mahakamani hapo.

Masogange ambaye amejizoelea umaarufu nchini kutokana na kupamba video za wasanii anakabiliwa na mashitaka mawili ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin na Oxazepam.

Katika kesi hiyo namba 77 ya mwaka 2017, Masogange anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14, mwaka huu, katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).

Pia anadaiwa kati ya Februari 7 na 14,2017 alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam.

Masogange aliposomewa mashitaka hayo kwa mara ya kwanza alikana na upande wa jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika.

Hakimu Mashauri alimtaka mshitakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mmoja atatia saini dhamana ya sh. milioni 10 na asitoke nje ya jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama.

Masogange alifanikiwa kutimiza masharti hayo ya dhamana, hivyo aliachiwa huru kwa dhamana hadi kesi hiyo ilipotajwa Jumanne hii.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents