Siasa

Kanisa Katoliki laishukia serikali

KANISA Katoliki nchini limeelezea kukerwa kwake na hali ya mambo nchini hivi sasa, inayoonyesha kukithiri kwa vitendo vya rushwa, ufisadi na uroho wa madaraka, vinavyofanywa na baadhi ya viongozi serikalini.

na Edward Ibabila, Musoma

 

KANISA Katoliki nchini limeelezea kukerwa kwake na hali ya mambo nchini hivi sasa, inayoonyesha kukithiri kwa vitendo vya rushwa, ufisadi na uroho wa madaraka, vinavyofanywa na baadhi ya viongozi serikalini.

 

Kwa upande mwingine, kanisa hilo limeelezea kusikitishwa kwake na mizigo anayobebeshwa mwananchi wa kawaida, kupitia gharama za maisha anazolazimika kuzilipia kama vile ankara za umeme na ada za leseni.

 

Hiyo ni kauli ya kwanza kutolewa na Kanisa Katoliki nchini, tangu kuibuka kwa kashfa za ufisadi, zilizohitimishwa hivi karibuni na kubainika kwa ubadhirifu wa mabilioni ya fedha kupitia akaunti ya kulipa madeni ya nje iliyoko Benki Kuu (BoT).

 

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini (TEC), Thadeus Lwaiche, ambaye ni askofi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dodoma, wakati wa ibada ya kuwekwa wakfu Askofu mpya wa Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Maria Mama wa Mungu la mjini Musoma jana.

 

Bila kutafuna maneno mbele ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo, Askofu Lwaiche alisema matatizo ya rushwa na ufisadi yanayoikabili nchi kwa sasa yanatokana na baadhi ya viongozi serikalini kuwa wabinafsi na wasiowajibika, hali ambayo alisema inachochea umaskini miongoni mwa jamii na taifa kwa ujumla na kusababisha kaulimbiu ya maisha bora kwa kila Mtanzania ionekane haina maana yoyote.

 

“Nchi yetu inakabiliwa na matatizo ya rushwa na ufisadi, ambayo yanasababishwa na ubinafsi na kutowajibika kwa baadhi ya watu waliopewa majukumu ya kuwatumikia wananchi. Mambo haya machafu yanazidisha umaskini kwa jamii na taifa na kusababisha kaulimbiu ya maisha bora kwa kila Mtanzania isiwe na maana,” alisema.

 

Kwa upande mwingine, kiongozi huyo wa kidini alibainisha kuwa hatua ya serikali kupandisha gharama za leseni na umeme ni kukwepa hali halisi ya matatizo yaliyopo kwenye Shirika la Umeme nchini (Tanesco), na kuongeza kuwa hatua hiyo ni njia ya mkato ambayo kwa vyovyote vile inawaathiri zaidi wananchi wengi wenye vipato kidogo.

 

Kwa upande wa ubadhirifu wa Benki Kuu (BoT), ambapo imethibitishwa kuwa sh bilioni 133 zilifujwa, Rais huyo wa TEC aliwapongeza bila kuwataja majina, wale wote waliopaza sauti kuweka wazi uozo huo na kuwataka kuendelea kufanya hivyo, kwani ni njia sahihi ya kuonyesha utumishi wao kwa Watanzania.

 

Aidha, alimpongeza Rais Kikwete kwa hatua aliyochukua kutokana na ubadhirifu uliofanyika BoT.

 

Baada ya kukabidhiwa ripoti kuhusu akaunti hiyo na Kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa hesabu ya Ernst & Young, Rais Kikwete alitengua uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa BoT, Daudi Ballali, na kuiagiza bodi ya benki hiyo kuwajadili wote waliohusika na kuwachukulia hatua stahili.

 

Aidha, alimuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akishirikiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Takukuru pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kufanya uchunguzi dhidi ya wote waliotajwa kuhusika katika kashfa hiyo, na kuwachukulia hatua, ikiwamo ya kurudisha fedha zote ambazo zililipwa kimakosa.

 

“Hata hivyo kuna mambo mengi yanayohitaji majibu kutoka serikalini. Kuna baadhi ya mambo yanayohitaji majibu ya kina, lakini yanatolewa ufafanuzi na majibu mepesi, hali ambayo si nzuri kwa maendeleo ya taifa na kanisa,” alisema.

 

Kuhusu vurugu zinazoendelea nchini Kenya, Askofu Lwaiche aliwataka wanasiasa nchini humo kutafuta mizizi ya vurugu hizo na kuiondoa, kwa kuzingatia masilahi ya taifa lao na kuheshimu uhai wa Wakenya, ambao wanapoteza maisha na wengine kuyakimbia makazi yao.

 

Aliwataka waumini wa kanisa hilo nchini kutoa michango kwa ajili ya wananchi wa Kenya walioathiriwa na vurugu za kisiasa.

 

Kwa upande wake, Lowassa aliwaambia watu waliokusanyika kushuhudia tukio hilo kuwa jamii haiwezi kutenganisha dini na maendeleo ya watu, kama ambavyo dini haiwezi kutenganishwa na umaskini.

 

Akizungumza na maelfu ya watu waliofurika kwenye ibada hiyo, akitoa nasaha za kumpongeza Askofu Msonganzila, waziri mkuu alisema kwa kiasi fulani umaskini unaletwa na watu kutofanya kazi kwa bidii na maarifa, kutojituma na kutokuwa wabunifu.

 

“Tunahitaji kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kupata maisha bora. Hakuna njia fupi na rahisi ya kupata maisha bora… mtusaidie kuhimiza waumini wenu wajibidiishe katika kazi ili kuondokana na umaskini… wawe wavumilivu na wawe na subira ya mafanikio ambayo yatakuwa endelevu,” alisema.

 

Ibada hiyo ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu Msonganzila ilihudhuriwa na Balozi wa Vatican Tanzania, Askofu Mkuu Joseph Chennoth, maaskofu 28 kutoka hapa nchini wakiwemo wawili wa kutoka Kenya na Uganda, pamoja na viongozi kadhaa wa serikali na chama.

 

Katika salamu zake, waziri mkuu alimwomba Askofu Msonganzila apambane na mmomonyoko wa maadili ambao umeikumba Tanzania na kusababisha matukio ya mimba kwa watoto wa shule, ubakaji wa watoto kama kinga ya maambukizi ya VVU, mauaji ya vikongwe na maalbino, kwa imani za ushirikina, ambayo alisema yameshamiri kwa kiwango kikubwa.

 

“Naiona kazi kubwa mbele yako ya kujenga imani thabiti ya Kikristu miongoni mwa waumini wako ili mauaji ya aina hii yasitokee jimboni mwako… naamini penye imani ya kweli ya kidini matukio haya hayawezi kutokea,” alisema.

 

Alisifu ushirikiano mzuri uliopo baina ya Kanisa Katoliki na serikali na jinsi kanisa hilo linavyojishirikisha kutoa huduma bora za afya, elimu na maji, tena bila ubaguzi wa aina yoyote.

 

Ili kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Kwangwa ya mkoa, alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Luteni Kanali (mstaafu) Issa Machibya, asimamie upatikanaji wa hati ya kumiliki ardhi ya eneo hilo.

 

Ombi la hati ya eneo hilo, lilitolewa na Askofu Mkuu Anthony Mayalla wa jimbo la Mwanza, ambaye alikuwa anasimamia Jimbo la Musoma tangu Askofu Justin Samba alipofariki dunia mwaka mmoja na nusu uliopita.

 

Kabla ya uteuzi huo, Askofu Msonganzila alikuwa Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents