Habari

Jeshi la polisi kupeleka askari wake Afrika Kusini, kuwahoji Agnes na Melisa waliokamatwa na shehena ya dawa za kulevya wiki iliyopita

Jeshi la polisi nchini linaendelea na uchunguzi wake juu ya tukio la wasichana wawili raia wa Tanzania Agnes Gerald (25) na Melisa Edward (24) waliokamatwa Ijumaa (July 5) katika uwanja wa ndege wa kimataifa OR Tambo nchini Afrika Kusini kwa kukutwa na takriban kilo 150 za dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine.

Nzowa(1)

Akiongea na gazeti la MWANANCHI kwa njia ya simu juzi (July 11) kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema wakati uchunguzi wa kubaini wahusika wakuu wa dawa hizo unaendelea, watapeleka askari wa jeshi hilo nchini Afrika Kusini kwaajili ya kuwahoji wasichana hao ambao bado wameshikiliwa na polisi nchini humo.

Nzowa ameongeza kuwa anaamini wasichana hao watatoa ushirikiano kwa kuwataja wahusika sahihi, na wote watakaohusika watakamatwa.

“Tutawapeleka askari wetu kuwahoji, tumekwishaanza uchunguzi wa hili…wote watakaohusika katika hili tutawakamata, lakini tunakwenda polepole hatua kwa hatua kuhakikisha tunawanasa wahusika sahihi,” alisema Nzowa.

Upande mwingine mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA), Moses Malaki amesema uchunguzi unaendelea na mamlaka imeliachia jeshi la polisi liendelee na kazi yake. Lakini ameendelea kusema ameshangazwa na jinsi ambavyo kiasi kikubwa kama hicho kilipitishwa uwanjani hapo licha ya kuwepo watu wanaouhusika na usalama, na kuongeza kuwa wataangalia nani waliokuwa zamu siku ya tukio.

“Sitaki kusema tutafanya nini, lakini ninachotaka kukwambia ni kwamba uchunguzi umeanza na suala zima tumewaachia polisi na sisi tutatoa ushirikiano kwa kila hatua watakayotutaka, lazima kukomesha hili. Tutaangalia nani walikuwa zamu siku hiyo,” alisema Malaki.

Ijumaa ya (July5) shirika la habari la Afrika Kusini (SABC) lilitangaza kukamatwa kwa wasichana wawili waliotokea Tanzania na kukutwa na mabegi sita yenye dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine maarufu kama ‘Tik’ nchini humo yenye thamani ya R million 42.6, ambao jeshi la polisi nchini Tanzania kupitia kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa lilithibitisha kuwa ni raia wa Tanzania na kuwataja kuwa ni Agnes Gerald na Melisa Edward.

SOURCE: MWANANCHI

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents