Siasa

Jaji Aonya Kesi Ya Epa Isiwe Mzaha

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Kiongozi mstaafu, Amir Manento, ameitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP)kupeleka ushahidi madhubuti na haraka mahakamani.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Kiongozi mstaafu, Amir Manento, ameitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP)kupeleka ushahidi madhubuti na haraka mahakamani.

Alisema vinginevyo washitakiwa wote wanaweza kuachiwa huru na kesi hizo zinazowahusu viongozi na wafanyabiashara zikaonekana kama mchezo wa kuigiza machoni mwa jamii.

Akizungumza kwenye hafla ya kilele cha miaka 60 ya tamko la haki za binadamu juzi, Jaji Manento alisema ushahidi huo lazima upelekwe haraka ili usaidie kufikiwa kwa maamuzi ya tuhuma hizo mapema.

Alisema Jeshi la Polisi ambalo ndilo linahusika na upelelezi kwa kushirikiana na ofisi ya DPP wanapaswa kujizatiti kwenye ushahidi ili kinachofanyika sasa kisije kikaonekana kama kiini macho au mchezo wa kuigiza.

“Kupandisha watu mahakamani kisha mkakosa ushahidi wa uhakika wa kuwatia hatiani wakaachiwa huru kunaweza kuonekana kama mchezo wa kuigiza, lazima polisi na DPP wajizatiti kupeleka ushahidi wa uhakika,“ alisema Manento.

Tayari watuhumiwa 20 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa madai ya kuhusika na wizi wa EPA. Jumla ya Sh bilioni 133 ziliibwa kilaghai katika akaunti hiyo.

Tangu sakata la EPA liibuliwe nchini, kumekuwa na hisia tofauti miongoni mwa jamii juu ya utashi wa serikali wa kuwafikisha mahakamani wahusika wote wa wizi huo.

Miongoni mwa hisia ambazo zimekuwa na msukumo mkubwa ni mustakabali wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited ambayo inatuhumiwa kujichotea kilaghai dola za Marekani milioni 30 sawa na Sh bilioni 40 kutoka EPA, lakini hadi sasa hakuna hata mtuhumiwa mmoja wa kampuni hiyo aliyefikishwa mahakamani.

Kampuni ya Kagoda inahisiwa kuwa ndiyo muasisi wa wizi wa fedha za EPA; ikiwa imemharibia kazi Waziri wa Kwanza wa Fedha mwanamke wa Tanzania, Zakia Meghji, ambaye aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo mara tu alipounda serikali Januari 2006.

Meghji kwa kupotoshwa na aliyekuwa gavana wa BoT, Marehemu Daudi Ballali, aliandika barua kwa kampuni ya ukaguzi ya Deloitte Dutche akitetea uchotaji wa fedha uliofanywa na Kagoda kuwa zilikuwa ni kwa masuala ya kiusalama, kabla ya kuitengua barua hiyo.

Waziri huyo hakurejeshwa kwenye baraza la mawaziri baada ya kuundwa upya kufuatia kujiuzulu kwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kutokana na sakata la Richmond.

Awali, akihutubia wananchi katika maadhimisho ya juzi, Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, alisema serikali itaendelea kuimarisha idara ya mahakama kwa kuongeza bajeti ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa wakati.

Alisema hali hiyo inaweza kusaidia kuhakikisha haki inatolewa kwa kila anayestahili.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents