Siasa

Ikulu yambana Chenge

SERIKALI imesema aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge anayetuhumiwa kumiliki dola za Marekani 1 milioni (Sh 1.2 bilioni) nje ya nchi, sasa anachunguzwa na vyombo mbalimbali vya kitaifa na kimataifa ili kubaini iwapo ana kesi ya kujibu mahakamani

Na Muhibu Said

SERIKALI imesema aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge anayetuhumiwa kumiliki dola za Marekani 1 milioni (Sh 1.2 bilioni) nje ya nchi, sasa anachunguzwa na vyombo mbalimbali vya kitaifa na kimataifa ili kubaini iwapo ana kesi ya kujibu mahakamani.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya tuhuma zinazomkabili Chenge ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), kufikishwa rasmi serikalini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba, aliliambia gazeti hili jana na kuwa, uchunguzi wa serikali umeshaanza na iwapo serikali itajiridhisha kuwa Chenge ana kesi ya kujibu, atafikishwa mahakamani ambako mambo yote yatajulikana.

“Suala lake (Chenge) limeshafika serikalini na ndio maana akajiuzulu. Uchunguzi wa kina unaendelea kuona huyu bwana ana hatia au hana. Tusubiri likifika mahakamani, mambo yote yatawekwa wazi,” alisema Waziri Simba.

Alipotakiwa kutaja vyombo vinavyomchunguza Chenge, Waziri Simba alisema: “Vyombo vingi vya ndani na nje ya nchi”.

Hata hivyo, alisema hawezi kutaja majina ya vyombo hivyo akisema kuwa, kufanya hivyo pamoja na kueleza hatua ya uchunguzi iliyofikiwa kupitia vyombo vya habari, kunaweza kuharibu uchunguzi husika.

“Naye (Chenge) ana haki, lakini sheria lazima ifuate mkondo wake,” alisema Waziri Simba alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana.

Aprili 13, mwaka huu, ikiwa ni siku moja baada ya Chenge kudaiwa kumiliki fedha hizo, Waziri Simba alikaririwa na gazeti hili akisema sheria itachukua mkondo wake kuona amezipataje.

Waziri Simba alisema hatua hiyo itachukuliwa baada ya taarifa rasmi kuhusu utajiri wa Chenge kufika serikalini.

Alisema taarifa rasmi zikifika, sheria itachukua mkondo wake kwani hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba, hata yeye (Simba) hayuko juu ya sheria.

Waziri Simba aliongeza kwamba, taarifa zikifika, itaangaliwa katika kumbukumbu za Chenge katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwani Chenge kama viongozi wengine, amejaza fomu za kutaja mali zake, hivyo kama amedanganya, itajulikana.

Alipoulizwa anachukuliaje taarifa za waziri kumiliki fedha nyingi kiasi hicho, alijibu: “Hata mimi nashangaa kama wewe, kama alizipata kihalali au la.”

Alisema hadi wakati huo taarifa hizo zilikuwa zikifanyiwa kazi nchini Uingereza na kuwataka wananchi kuwa na subira katika jambo hilo.

“Lakini kuna mtu nimemwambia, labda kauza ng’ombe wao wote ndio akapata hizo pesa, labda watu hatujui, au ana biashara nyingine,” alikaririwa akisema Waziri Simba.

Kauli hiyo ya Waziri Simba ilitolewa siku moja, baada ya Gazeti la The Guardian linalochapishwa nchini Uingereza katika toleo lake la Aprili 12, mwaka huu, kueleza kuanza kwa uchunguzi dhidi ya Chenge, kutokana na akaunti yake kukutwa na dola 1 milioni.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, taasisi ya kuchunguza makosa makubwa ya jinai nchini humo ijulikanayo kwa jina la Serious Fraud Office (SFO), inafanya uchunguzi kuhusu fedha hizo, ili kuangalia iwapo zina uhusiano wowote na zile zinazoaminika kutolewa kwa njia ya rushwa wakati Tanzania iliponunua rada ya kijeshi kutoka nchini humo kwa paundi milioni 28 (Sh70 bilioni), mwaka 2002.

Gazeti hilo lilieleza uchunguzi huo wa SFO unatarajia kuanza katika kipindi cha wiki sita zijazo, kuanzia wakati huo.

Kwa mujibu wa habari hizo, uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba, moja ya mambo yanayofuatiliwa ni kujua iwapo fedha hizo zinazoaminika kuwa za Chenge, zilizowekwa katika akaunti moja iliyoko katika Kisiwa cha Jersey, Uingereza, zina uhusiano wowote na zile zinazoaminika kutoka katika Kampuni ya BAE System, inayotuhumiwa kuinyonya Tanzania kwa kuiuzia rada hiyo kwa bei kubwa kuliko ilivyotakiwa.

The Guardian katika habari yake hiyo iliyowekwa katika mtandao wa intaneti, liliripoti kuwa taarifa hizo zinakuja ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kwa kushirikiana na SFO na taasisi za uchunguzi za Uswisi na Jersey zilipoanza kuchunguza kuhusu kashfa nzima ya ununuzi wa rada.

Gazeti hilo lilimkariri Chenge akikiri kwamba fedha hizo ni mali yake na akatumia fursa hiyo kukanusha kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha hizo na kashfa nzima ya ununuzi wa rada, uliofanywa wakati yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) katika serikali ya awamu ya tatu.

Septemba 15, mwaka jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, walimtaja Chenge katika orodha ya vigogo 11, wakiwamo viongozi kadhaa wa serikali nchini kuhusika na ufisadi wa mabilioni ya shilingi za walipakodi.

Baadaye, Septemba 19, Waziri Chenge aliliambia gazeti hili kuwa walioibua hoja ya ufisadi dhidi ya viongozi wa serikali kama wakipata au kama wana ushahidi, yeye binafsi anatoa ruksa waupeleke katika vyombo vya dola ili ufanyiwe kazi.

Alisema hapendi malumbano, isipokuwa yote yaliyozungumzwa atahitaji kuyaona kwa maandishi na uonyeshwe ushahidi wa yeye kuhusika moja kwa moja na ufisadi.

Aprili 17, mwaka huu, alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JNIA), Chenge aliwaambia waandishi wa habari kuwa tuhuma za Sh1 bilioni anazodaiwa kumiliki katika akaunti Uingereza, ni za “vijisenti”.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kuziita vijisenti Sh 1.2 bilioni, alisema: “Kila mtu ana viwango vyake na ana haki ya kusema anavyotaka. Na mtu akikutuhumu, unajua nafsini mwako”.

Hata hivyo, siku mbili baadaye, Chenge alikaririwa na vyombo vya habari akiwaomba radhi Watanzania kutokana na kauli yake hiyo akisema kuwa, ilitokana na kuathiriwa na kabila lake la Kisukuma.

Siku chache baadaye, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu, alikaririwa na vyombo vya habari akitangaza kuhusu uamuzi wa Chenge wa kujiuzulu Uwaziri wa Miundombinu, uliopongezwa na Rais Jakaya Kikwete kwamba, ni jambo pekee alilokuwa akilitegemea kutoka kwa Chenge.

 

 

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents