Habari

Human Rights Watch: Watoto milioni 1.5 wa Tanzania hawapo shuleni

Shirika lisilo la kiserikali ya Human Rights Watch linaloshughulikia haki za watoto na wanawake limetoa ripoti yake ambayo inadai kuwa takribani watoto milioni 1.5 wa Tanzania hawajapata haki yao ya elimu kutokana na changamoto zinazowakabili wao binafsi pamoja na familia zao.

Aidha ripoti hiyo ya taasisi hiyo yenye kurasa 98 iliyoandikwa na Elin Martinez ambaye pia ni mtafiti wa Human Rights Watch imesema asilimia 40 ya vijana wa hapa nchini hawapati elimu bora katika masomo yao ya elimu ya sekondari baada ya mwaka jana kuwahoji wanafunzi 220 wa shule mbalimbali za sekondari, wasiokuwa shuleni, wazazi, walimu, wanaharakati na wadau wengine wa elimu.

Katima maelezo yake aliyoyatoa Elin Jumanne hii katika mkutano na wadau mbalimbali wa elimu hapa nchini wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa usimamizi wa elimu kutoka ofisi ya Rais Tamisemi, Juma Kaponda, amesema, “Kufutwa kwa ada na michango katika shule za sekondari nchini Tanzania imekuwa ni hatua kubwa katika kuimarisha ujiungaji wa elimu ya sekondari hapa nchini.”

Elin Martinez mtafiti wa shirika la Human Rights Watch

“Lakini serikali inapaswa kwenda mbali zaidi na kushughulikia swala la idadi kubwa ya wanafunzi katika vyumba vya madarasa, ubaguzi na unyanyasaji wa namna mbalimbali unaoathiri elimu ya vijana wengi,” ameongeza.


Agnes Odhiambo mtafiti mwandamizi wa Human Rights Watch

Naye Agnes Odhiambo ambaye ni Mtafiti mwandamizi wa shirika hilo amesema, “Watoto hao hawajaenda shule kutokana na shida nyingi zikiwemo za kifedha. Japo serikali inatoa elimu bure lakini bado watoto wanatoa elimu kama ya usafiri kwenda shule, kununua sare za shule hiyo ni changamoto kubwa wanayoipata hasa kwa wale wanaotoka kwenye familia zisizojiweza. Pia kuna ukosefu wa madarasa ya kutosha, walimu, vitabu na vitu vingine vingi vinavyohitajika kuelimisha watoto.”

“Lakini pia kuna matatizo mengine ya sera na ubaguzi hasa kwa watoto wa kike, unyanyasaji wa kijinsia, matatizo ya adhabu kali kwa mfano kwa hapa Tanzania kuna adhabu za viboko, au kufukuza watoto shuleni wanaopata mimba.”

Kaimu Mkurugenzi wa usimamizi wa elimu kutoka ofisi ya Rais Tamisemi, Juma Kaponda

Wakati huo huo Kaponda ambaye alikuwepo katika mkutano huo kwa ajili ya kuiwakilisha serikali amesema, “Kuna baadhi ya vitu kwenye ripoti yao waliotuelezea pale mbele hawajaviweka wazi labda kwenye kitabu cha ripoti vitakuwepo. Sisi kama serikali tutaenda kuipitia na tutakutana nao kwa kukaa kikao ili kuchambua zaidi utafiti wao.”

Tazama picha nyingine za wageni walioudhuria kwenye mkutano huo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents