Burudani

Hiki ni kitu wanachopaswa kukifahamu wasanii wanaohofia kuachia kazi mpya kipindi hiki

Mwezi March ndio huo unaelekea ukingoni. Ahh huu mwezi ulikuwa na vimbwanga! Ni mwezi ambao kwa kiasi kikubwa utabaki kwenye kumbumbuku za aina yake kwenye kalenda ya mwaka 2017.

Ni mwezi uliokumbwa na matukio yaliyotawala mazungumzo katika kila kona ya nchi kuanzia vibarazani, magazetini, redioni na runingani, na zaidi hasa kwenye mitandao ya kijamii ambayo kadri miaka inavyokwenda imezidi kuwa na nguvu mno kiasi cha kuanza kutengeneza ajenda za nchi.

Tukio kubwa zaidi katika mwezi huu ni uvamizi wa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika studio za Clouds Media Group akiwa na askari waliokuwa wamebeba silaha nzito pamoja na kuondolewa kwenye nafasi uwaziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo kwa mheshimiwa Nape Nnauye aliyejitoa kutafuta suluhu la uvamizi huo. Matukio haya mawili yametikisa nchi na kishindo chake kilikuwa kikubwa kiasi cha kuhisiwa hadi na mataifa ya nje. Haya ni matukio yaliyoandikwa zaidi katika vyombo vya habari vya kimataifa pengine kuliko yote yaliyotokea tangu mwaka huu uanze.

Matukio haya mawili yamebakiza fumbo gumu ambalo bado linaendelea kuumiza vichwa vya wanahabari wengi wa Tanzania. Na si fumbo tu, ni uoga ulioanza kumea kwa sisi waandishi katika namna ya kuziandika habari zinazoikosoa serikali na huku pia tukipata tafsiri mpya ya kipi ni kikomo cha uhuru wa vyombo vya habari. Kwa wawiliki ambao tayari wamepewa onyo na mkuu wa nchi, hofu kubwa waliyonayo sasa ni namna baadhi ya viongozi wa serikali walivyo na mamlaka katika maudhui yanayotangazwa.

Baada ya utangulizi huo, ningependa kuzungumza sasa kiini cha makala hii. Matukio haya yana athari gani katika tasnia ya burudani? Kwa mtazamo wangu, yana athari kubwa, chanya na hasi.

UPANDE WA KWANZA WA SHILINGI (ATHARI CHANYA)

Mazungumzo ya siasa na maamuzi ya serikali yamechukua sehemu kubwa ya nafasi iliyokuwa imetawaliwa na soga za udaku na burudani. Vijana ambao ni walaji wakubwa wa taarifa za kidaku, sasa wamezifungua akili zao kupokea taarifa nyingi za masuala ya siasa. Kwa mwezi huu, mijadala mikuu katika makusanyiko ya vijana ama katika mitandao ya kijamii imekuwa ya kisiasa zaidi ukilinganisha na ile ya burudani.
Hiyo ni dalili nzuri kwamba vijana sasa wameamka na wanaguswa zaidi na maamuzi yanayochukuliwa na serikali yao. Ni ishara kuwa elimu ya uraia imewakaa akili mwao na tofauti na zamani, hawapuuzi tena mambo yanayoendelea katika serikali yao. Na ndio maana, shinikizo kubwa zaidi analolipata mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kutokana na kashfa zinazomuandamana linatoka kwa vijana. Na kwa matukio kama ya kukamatwa Nay wa Mitego baada ya kuachia wimbo unaoikosoa serikali, ni dhahiri kuwa siasa itaendelea kujipenyeza kwenye ufalme wa masuala ya burudani.


UPANDE WA PILI WA SHILINGI (ATHARI HASI)

Kuna wasiwasi mkubwa kwa wasanii kuachia kazi zao kipindi hiki. Wengi wanaamini kuwa hiki si kipindi kizuri kutoa nyimbo mpya kwasababu focus ya walaji wao ipo kwenye masuala ya siasa na kile kinachoendelea nchini. Wanaamini kuwa masikio na macho ya wengi hayana utayari wa kuburudika wakati baadhi ya maamuzi yanayochukuliwa na serikali yanawaathiri kwa namna moja ama nyingine na hivyo kuwaondoa kwenye ‘mood’ ya kuburudika. Kama wasanii wakihofia kuachia kazi zao katika kipindi hiki, ni wazi kuwa tasnia ya burudani inapata pigo kwa kiasi chake. Na dhihirisho kuwa siasa ndio kila kitu.

NINI KIFANYIKE?

Kuna frustrations za hapa na pale ambazo zinatokana na baadhi ya maamuzi ya serikali. Wasanii kazi yao kubwa zaidi ya yote ni kuburudisha. Maana yake ni kwamba, hiki ni kipindi muhimu zaidi kwa wao kufanya kazi yao – kuwaburudisha mashabiki. Hivyo,basi, tofauti kabisa na imani yao, huu ndio muda muhimu zaidi kwa wao kuachia kazi nyingi. Kazi zinapotoka nyingi, zitawasaidia mashabiki kuwahamisha kwa muda katika frustrations hizi za kisiasa na kujiburusisha. Ukweli ni kwamba wakati mwingine vijana hujikuta tukipigia kelele vitu ambavyo hatuwezi kuvibadilisha. Hasira hizi hutunyong’onyeza kiasi cha kutuondoa kwenye mstari na kukata tamaa zaidi. Hapo ndipo wasanii wanapaswa kuingilia kati kwa kuachia kazi kali zitakazotufanya tuyafurahie maisha na kujipa moyo kuwa kila kitu kitanyooka.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents