Tragedy

Hausigeli amnyonga mtoto wa bosi wake

Msichana anayefanya kazi za ndani maeneo ya Manzese, Dar es Salaam, Tabu Isaya (16), anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumnyonga hadi kumuua mtoto wa mwajiri wake na kisha kuutupa mwili wake makaburini.

Na Joseph Mwendapole

 
Msichana anayefanya kazi za ndani maeneo ya Manzese, Dar es Salaam, Tabu Isaya (16), anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumnyonga hadi kumuua mtoto wa mwajiri wake na kisha kuutupa mwili wake makaburini.

 

Sababu za Taabu kuchukua hatua ya kumuua mtoto huyo wa miezi minane inadaiwa kuwa ni hasira za kutolipwa mishahara ya miezi sita hadi sasa na mwajiri wake huyo.

 

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Bw. Jamal Rwambow, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi na kwamba mtuhumiwa huyo atafunguliwa mashtaka ya mauaji.

 

Jirani wa eneo alilokuwa akifanya kazi msichana huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema msichana huyo alikuwa akilalamika mara kwa mara kutolipwa mshahara kwa muda mrefu na mwajiri wake.

 

Alisema msichana huyo ni mwenyeji wa mkoa wa Dodoma na alikuwa akiishi na mwajiri wake maeneo hayo.

 

Alisema wakati wa tukio hilo, mama wa mtoto huyo, Bi. Asia Ali alikuwa katika biashara zake maeneo ya Ubungo.

 

“Mara kwa mara alilalamika kuwa halipwi mshahara na aliahidiwa kuwa mwezi Desemba mwaka jana angelipwa malimbikizo yake lakini baada ya kuona halipwi akawa anataka kurudi kwao Dodoma,“ alisema jirani huyo.

 

Alisema mazishi ya mtoto huyo yalifanyika jana mchana katika makaburi ya Ufi jijini.

 

Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Bw. Jamal Rwambow alisema awali, msichana huyo wa kazi alitoa taarifa za uongo kituo cha polisi cha Urafiki lakini walipombana walibaini ukweli wa tukio hilo.

 

Alisema awali, msichana huyo alidanganya kuwa aliporwa mtoto huyo na watu maeneo ya Manzese wakati akimpeleka hospitali baada ya mtoto huyo kuugua ghafla.

 

“Askari walitafakari kauli hiyo na kubaini kuwa ni ya uongo kwani mtu kupigwa na kuporwa mtoto mchana na watu wakishuhudia si rahisi. Hivyo walimbana na akasema ukweli kuwa hakuporwa mtoto huyo,“ alisema.

 

Alisema baada ya kumhoji zaidi, msichana huyo alibadili kauli na kusema kuwa mtoto huyo alifariki wakati akijaribu kumlisha chakula kwa nguvu na kwamba alimbana pua kwa muda mrefu.

 

Kamanda Rwambow alisema kuwa baada ya kumbana pua kwa muda mrefu mtoto huyo alifariki na ndipo alipokwenda kumtupa.

 

“Katika kutaka kupoteza ushahidi alimfunga katika mfuko na kwenda kumtupa,“ alisema kamanda Rwambow.

 

Hivi karibuni serikali ilipandisha mishahara kwa sekta binafsi, ambapo kwa watumishi wa ndani ulipanda na kufikia sh. 60,000 kwa mwezi.

 

Hata hivyo, serikali ilifafanua kuwa wale watakaolipwa sh. 60,000 ni wale wanaofanya kazi na kuondoka lakini wale wanaoshi na waajiri wao watakuwa wakilipwa sh. 20,000.

 

Serikali imekuwa ikisisitiza kwamba mwajiri anashauriwa kumuongozea mfanyakazi wake mshahara zaidi ya huo uliopangwa na serikali.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents