Burudani

Global Publishers yawaomba radhi Zitto Kabwe na Diva

Kupitia gazeti la Amani la Septemba 11-17, 2014, kulichapishwa habari ukurasa wa mbele iliyosomeka: “DIVA: ZITTO NI MUME WANGU.” Ikikolezwa na dondoo ‘Adai ni mke anayetambulika kisheria’ na ‘Asema hayuko tayari kuachana naye kirahisi,’. Na sasa uongozi wa gazeti hilo umekusudia kwa nia njema kutoa ukweli juu ya habari hiyo.

zitto

Ufafanuzi huu unalenga kumaliza mkanganyiko uliojitokeza hasa baada ya kuwepo kwa madai kutoka kwa mhusika ambaye ni Loveness Malinzi (Diva) kuwa, hakuzungumza na gazeti kile kilichoandikwa na kwamba alikuwa anazushiwa; madai haya aliyawasilisha chumba cha habari kwa njia ya simu na sehemu kuyaweka kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Instagram.

Kama hilo halitoshi, Diva alikana kuzungumza na mwandishi wa habari hiyo ambapo alisema mazungumzo yao yalihusu mwaliko wa Kipindi cha Global TV Online ambacho kinarushwa na mtandao unaoendeshwa na Kampuni ya Global Publishers inayomiliki pia Gazeti la Amani na si vinginevyo.

Malalamiko haya ya Diva yalikuja muda mchache baada ya gazeti kutoka likiwa na habari hiyo ambapo jopo la wahariri wa Amani kabla ya kuchapisha habari hiyo walijiaminisha kuwa ni ya kweli kutokana na taarifa pamoja na vielelezo vya rekodi ya sauti ya mazungumzo alivyoviwasilisha mwandishi kwenye dawati kuthibitisha kuwa alifanya mazungumzo na mhusika kuhusiana na msingi wa habari nzima iliyoandikwa.

Kama tulivyoeleza, baada ya habari hiyo kutoka na kipande cha sauti kuingizwa kwenye Tovuti ya Global Publishers, ndipo yalipoibuka madai hayo huku baadhi ya wasomaji wakieleza kuwa ile siyo sauti ya Diva; hapo ndipo uongozi wa gazeti ulipoamua kufuatilia ukweli na kubaini yafuatayo.

Pamoja na ukweli kuwa Mheshimiwa Zitto Kabwe (Mbunge wa Kigoma Kaskazini) na Diva wana ukaribu, mazungumzo kati ya mwandishi na mwanadada huyo kuhusiana na kauli yake ya: “Zitto ni Mume Wangu,” hayakufanyika na kwamba mwandishi alipika habari na kutengeneza sauti ya Diva kwa lengo la kuwahadaa wahariri kwa nia mbaya!

Kwa msingi huo sisi kama chombo cha habari makini, kinachosimamia weledi, kulinda na kuheshimu haki za binadamu; tunachukuwa nafasi hii kumuomba radhi Diva, Mheshimiwa Zitto, sanjari na jamii kwa ujumla kwa usumbufu wowote uliosababishwa na habari hiyo. Aidha, uongozi unapenda kuutangazia umma kuwa, hatua kali za kinidhamu zimeshachukuliwa dhidi ya mwandishi husika sambamba na onyo kwa viongozi wote wa gazeti kwa udhaifu uliojitokeza katika habari hiyo.

Tunaomba jamii ielewe kwamba Global Publishers siku zote inasimamia UKWELI na kamwe hairuhusu kabisa habari za uongo kuandikwa katika magazeti yake.

Jamii iendelee kutuamini na kushirikiana nasi katika kusimamia weledi wa uandishi wa habari. Milango ya kukosolewa iko wazi, hivyo kwa mwenye malalamiko yoyote juu ya habari zetu, iwe ni uongo au kutotendewa haki, asisite kuwasiliana na viongozi kwa hatua zaidi. Ndimi, Mhariri Kiongozi, Magazeti Pendwa.

Global Publishers

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents