Burudani

Genevieve ni Miss Tanzania

Genevieve Emmanuel ambaye ni mtoto wa Meneja wa timu ya soka ya Yanga ya Dar es Salaam inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, Emmanuel Mpangala, ndiye Miss Tanzania mwaka 2010.

Geneveive aliibuka mshindi baada ya kuwabwaga wenzake 29 waliokuwa wakiwania taji hilo, hivyo kujinyakulia gari aina ya Hyundai i10 yenye thamani ya shilingi milioni sita, huku mshindi wa pili akiwa ni Miss Arusha, Glory Mwanga (kushoto katika picha ya chini) ambaye alijinyakulia Sh milioni sita na Consolatha Lukosi (kulia katika picha ya chini) ambaye ni Miss Ilala namba tatu, pia alikamata nafasi hiyo katika Miss Tanzania.

Mrembo huyo ambaye pia ni Miss Temeke 2010, sasa amelirudisha taji la Miss Tanzania jijini Dar es Salaam baada ya kuwa mkoani Mwanza kwa miaka miwili mfululizo.

Taji hilo lilikuwa linashikiliwa na Miriam Gerald ambaye alitwaa taji hilo mwaka jana akitokea mkoani Mwanza, akilirithi kutoka kwa Nasreem Karim ambaye alilitwaa mwaka 2008 na kumaliza utawala wa Dar es Salaam katika mashindano ya urembo hapa nchini.

Nasreem aliyekuwa mrembo wa Kanda ya Ziwa akitokea mkoani Mwanza, aliwabwaga warembo wenzake 27 waliokuwa wakiwania taji hilo. Kwa miaka mingi taji la Miss Tanzania lilikuwa likichukuliwa na warembo kutoka kanda za Dar es Salaam, ambazo ni Ilala, Temeke na Kinondoni, lakini tangu Nasreem amalize utawala huo taji hilo kwa miaka miwili sasa limehama Dar es Salaam.

Baada ya Saida Kessy aliyetwaa taji akitokea mkoani Arusha mwaka 1997, hakuna mrembo mwingine nje ya Dar es Salaam aliyetwaa taji hilo baada ya hapo.

Mrembo huyo anakuwa wa tatu kutoka Temeke kutwaa taji la Miss Tanzania, ambapo wengine walikuwa mwaka 2001 na 2004.

Akitangaza matokeo ya mashindano hayo juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Prashant Patel alitangaza Taji la Miss mwenye kipaji kuchukuliwa na Flora Florence ambaye ni Miss Morogoro, huku mrembo wa Utalii wa ndani akiibuka Salma Mwakalukwa ambaye alikuwa mshindi wa pili Miss Ilala.

Balozi wa Redd’s aliibuka Consolatha Lukosi. Miss Ilala 2010 Bahati Chando hakuingia kumi bora.

Akizungumza baada ya matokeo hayo, mama mzazi wa Miss Tanzania, Maria Mpangala alisema ushindi wa mwanawe ni zawadi kwa familia yao na kwamba walimsaidia kwa kila hali kufikia hatua hiyo.

Kwa mujibu wa mama huyo, Geneveive alimaliza kidato cha sita mwaka huu katika sekondari ya Ruaha iliyopo Iringa na alikuwa akisomea masomo ya Historia, Jiografia na Lugha (HGL).

Katika shindano hilo, Miss Kanda ya Kati, Wilemi Etami aliteleza na kuanguka chini baada ya kumaliza hatua ya kujmbulisha.

Burudani mbalimbali zilisindikiza shindano hilo kutoka kwa wasanii wa kundi la THT pamoja na TMK Wanaume Family.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents