Bongo Movie

Freemason: Dhana inayopanda mbegu ya ujinga na uvivu kwa vijana wa Tanzania

“Jamaa ana nyumba mbili Mbezi Beach, ana gari tatu na maduka mawili makubwa, aah yule ni Freemason mwanangu, haiwezekani avipate hivi hivi”!! Huo ni mfano wa kauli za aina hiyo zilizogeuka kuwa maarufu sana kwenye midomo ya watanzania.

Freemason ni neno lililojipatia makazi ya kudumu kwenye fikra za watanzania wengi wavivu, wagumu wa kufikiri na wepesi wa kusahau. Si mjini tu hata vijijini usishangae kukuta kundi la vijana waliokimbia shule wakilaumu maisha magumu na kuzungumza story za Freemason.

Katika kipindi cha Super Mix cha East Africa Radio cha ijumaa, June 1, kulisikika mtu aliyedaiwa kupewa namba ya mhusika wa Freemason Tanzania na kumpigia kujua mchakato wa kujiunga na chama.

Haijulikani mtu huyo alipewa na nani namba hizo kwakuwa mwenye namba ni mfanyakazi wa kituo hicho ambaye simu hiyo kwake iligeuka kuwa kituko cha mwaka na kuamua tu kumchezea akili kijana huyo mwenye imani kubwa kuwa kwa kujiunga na Freemason basi tabu na shida alizonazo atazipungia mkono wa kwaheri.

Kijana huyo aitwaye Babu Elias, mwenyeji wa Kilimanjaro, mile 6 ambaye kwa sasa yupo jijini Dar es Salaam na mwenye umri wa miaka 30, anasema anataka kujiunga na Freemason kwasababu maisha ni magumu na biashara zinakwenda mrama.

Kutokana na mazungumzo hayo, tunapata picha ni kwa kiasi gani mdudu huyu ameingia kwenye akili za watu wavivu wasiotaka kufanya kazi.

Siku hizi neno hili limeshakuwa kama fashion mdomoni mwa watu. Kila mtu, awe msanii ama mwanasiasa akionekana amefanikiwa tu basi wabongo hawachelewi kusema, “ahh yule Freemason!”

Mbaya zaidi ni kuwa wengi huizungumzia dhana hii kwa mifano na story wanazoziskia tu vijiweni. Matokeo yake wengi hawajui maana halisi ya jambo lenyewe.

AY, Diamond na hayati Stephen Kanumba ni miongoni mwa watu wanaosemwa na watu ambao ni haki kuwaita wavivu wa kufikiri, kuwa wamejiunga na chama hicho kisa mafanikio makubwa waliyoyapata bila kujua namna walivyotoka mbali.

Wengi wanadhani ukijiunga na chama, basi kesho asubuhi utakutana na begi lililojaa hela mlangoni mwako.

Ukweli unabaki pale pale kuwa Freemasonry: chama ambacho kinajumuisha watu wenye imani na interest moja, kilichoanza tangu karne ya 16, kikiwa katika mifumo mbalimbali duniani kote na wanachama takriban milioni sita, lakini ni jambo la kupiga vita mawazo ya baadhi ya watu kuwa kila aliye tajiri amejiunga na chama hicho.

Jambo la msingi ambalo watu wanapaswa kujua kuhusu dhana hii ni kuwa wanachama wa chama hiki (na sio dini kama wengi wanavyodhani) ni watu matajiri tayari ambao hujihusisha sana na utoaji wa misaada (Philanthropy).
Wabongo wengi kama Babu Elias, wanaamini kuwa maskini akijiunga na Freemason basi baada ya muda mfupi atakuwa tajiri bila kufikiria pesa hizo watazitoa wapi.

Freemason si chama cha watu wenye njaa. Japo utajiri si kigezo cha kuwa mwanachama, hali halisi ni kuwa wanachama wengi ni watu matajiri wenye pesa nyingi kiasi cha kushindwa kujua pa kuzipeleka.

Na ndo maana ni watoaji wazuri wa misaada.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents