Bongo Movie

Filamu ya One The Incredible ‘BongoNaFlava’ yaonyeshwa kwa mara ya kwanza Goeth-Institut Upanga

Filamu mpya ‘BongoNaFlava’ ya rappa One The Incredible imeonyeshwa kwa mara ya kwanza katika ukumbi wa Goeth-Institut Upanga jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.
13230300_1132271670158027_1242531775386134713_n

Filamu hiyo imeweza kuwakutanisha mastaa wa muziki kama Fid Q, Wakazi, Makamua, Lamar pamoja na washiriki wengine.

Kupitia ukurasa wa instagram, One aliandika: Firstviewing at Goeth e Institut – Upanga, this Thursday. Hii ndio mara yangu ya kwanza kama muigizaji… Karibu Goethe Institut – Upanga, alhamisi hii uione filamu ya #BongoNaFlava iliyotayarishwa chini ya usimamizi wa director nguli @rrahc itaoneshwa kwa mara ya kwanza. #Pichakubwa

Malle Hanzi ni mmoja kati wa watu walio shuhudia tukio hilo, naye aliamua kuandika uchambuzi wa filamu hiyo.

Jioni ama naweza kusema ni Usiku wa Tarehe 19/05/2016 nilikuwa maeneo ya Upanga sehemu yenye jengo liitwalo GOETHE INSTITUT. Goethe Institut ni taasisi iliyo chini ya serikali ya Ujerumani. Taasisi hii imeanzishwa mwaka 1951 ikiwa na makao makuu yake katika jiji la Munich lakini ina matawi zaidi ya 150 katika nchi mbalimbali duniani na Tanzania ikiwemo.

Dhumuni la kuanzishwa kwa taasisi hii ni kusambaza/kufundisha utamaduni wa kijerumani na pia kubadilishana tamaduni na mataifa mengine kupitia filamu, muziki, fasihi n.k

Jioni ya Tarehe hiyo katika “Thieta” ya taasisi hiyo kulikuwa na filamu iitwayo “Bongo na Flava” iliyokuwa ikioneshwa kwa mara ya kwanza. Habari njema ni kwamba inaweza ikaoneshwa tena katika tamasha la ziff mwaka huu. Katika filamu hii imehusisha wahusika kama One the Incredible, Fid Q, Wakazi, Cheusi (wa siri ya mtungi), Lamar, Songa, Makamua, Salu T, Saigon na wengineo huku ikiwa imetayarishwa na kuongozwa na RlahC, Karabani na wengineo.

Kusema ukweli ni Filamu nzuri sana inayosadifu sanaa na maisha ya kila siku. Watayarishaji na waigizaji wa Filamu wamejitahidi sana katika kuikamilisha Filamu hii. Pongezi za moja kwa moja zimuendee One The Incredible ambaye ameigiza kama mhusika mkuu akifahamika kama Zopa. Kiukweli One kavaa uhusika ipasavyo; amefanya kazi nzuri sana.

Stori ya hii filamu inamhusu One (zopa) ambaye ni kijana aliyetoka kijijini mkoani kigoma na kwenda jijini Dar es salaam baada kuambiwa na rafiki yake kwamba kuna kazi atampatia. One anapofika jijini Dar es salaam anapatafuta anapokaa rafiki yake na kupapata lakini mama yake na rafikiye anamuambia rafiki yake yuko jela kwa kesi ya mihadarati. One anaomba hifadhi ya muda mfupi lakini anakataliwa na kufukuzwa.

One anaingia mtaani akiwa hajui anaanzia wapi anaishia wapi? Ndipo anajikuta analala katika vibaraza vya nyumba za watu na mwisho kabisa anavamiwa na vibaka na kuibiwa kila kitu. Baada ya kuhangaika hangaika ndipo anakutana na Makamua anayeamua kumpa hifadhi katika Ghetto lake na hapo ndipo muvi inapoanza. One anajikuta akifanya kila aina ya kazi ili kuwa na maisha mazuri na kuwa msanii mkubwa.

Jina la filamu BONGO NA FLAVA ndilo limetumiwa na waandaaji kuinadi filamu hii. Bongo inaweza kuwa na maana zaidi ya moja; baadhi ya maana ni 1. Bongo humaanisha Akili na 2. Bongo humaanisha Tanzania n.k. Neno flava (Flavor) tafsiri yake ni Ladha. Sina hakika kama wenye hii filamu walitaka kumaanisha Akili na Ladha au Tanzania na Ladha.

Inawezekana jina Bongo na Flava likawa na uhusiano kidogo na Bongo Flava kwa maana ya aina ya muziki ambao unapatikana Tanzania. Hii inanipa ukakasi kidogo kuamini hilo maana katika Filamu hakuna mahali umesikika muziki wa Bongo Flava zaidi ya Hip Hop ingawa kuna muimbaji wa R&B (Makamua). Inawezekana kukawa na mahusiano kama Bongo Flava hujumuisha aina hizo za muziki pia.

Kwenye filamu hii kuna mahali One alifika studio ya prodyuza mmoja akakutana na mlinzi ambaye alianza kumuita kwa jina la Bongo Fleva. Baadaye alimuuliza (Nukuu isiyo rasmi) “wewe ni bongo fleva?” One akasema “Unaweza kusema hivyo” yule mlinzi akarudia kumuuliza tena “Kwa hiyo wewe ni Bongo Fleva” One akajibu tena “Mimi nafanya Muziki”.

Kwa upande wa mmoja nilichokiona katika kipande hiko ni kushindwa kujiamini kwa One inawezekana pia alichanganya Maelekezo ya Scene inavyotaka na Imani yake binafsi. Jibu lake la kwanza ni kama alikubali yeye ni Bongo Fleva na jibu la pili ni kama alijaribu kuikataa kiaina.

Kwa upande mwingine inawezekana pia One aliamua kujivika uhusika wa Baadhi ya wana Hip Hop ambao akiwa na Wanahip hop anasema mwanahiphop na kuiponda Bongo Fleva na akiwa na wanabongo fleva anaenda nao sawa kwamba Bongo Fleva na Hip Hop ni kitu kimoja zote ni aina za muziki.

Kitu kingine nilichokiona ni pale ambapo One anatoka Jela baada ya kukamatwa na Bangi. Ukiangalia jinsi alivyoingia jela miezi sita iliyopita na jinsi alivyotoka utaona hakuna tofauti yoyote ile kimuonekano hata ndevu zake ziko saizi ile ile. Kwa jinsi nizijuavyo jela na mahabusu zetu ukilala wiki moja tu lazima urudi uraiani na mabadiliko, itakuwa miezi sita kweli. Jela/mahabusu zetu hazijawahi kuwa na matokeo ya namna hii.

Kuna “scene” moja pia One alitakiwa kumeza kete za madawa ya kulevya ili azisafirishe kwenda Italy lakini akashindwa kuzimeza akiwa katika chimbo la wazungu wa unga ila akaomba akazimezee nyumbani akapewa aondoke nazo.

Katika hali ya kawaida tu inawezekana vipi muuza madawa ya kulevya akamuamini mtu kwa siku moja tu ambayo ndiyo wamekutana na kumpa mzigo wa madawa na kuondoka nao nyumbani kwake akaumeze.? Pengine watu wenye uzoefu wa mambo haya wanaweza kunishawishi.

Hii ni aina ya Filamu ambayo haupaswi kukaa unaangalia na Familia yako ama na watu ambao mnaheshimiana nao sana kutokana na matumizi ya Lugha yaliyotumika. Lugha iliyotumika ni isiyo na kificho kihivyo kwa mfano: maneno kama Ms*nge nk ni maneno ambayo yametumika kama maneno ya kawaida kabisa. Nafikiri waandaaji walipanga kutumia maneno yenye uhalisia zaidi na ndiyo hutumiwa na mitaani kama “vivumishi vikurupushi” visivyo rasmi katika maongezi hasa ya vijana. Hii ni filamu inayopaswa kuangaliwa na watu wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea.

Yote kwa Yote, licha ya vijichangamoto vidogo vidogo lakini kiukweli hii ni moja kati ya filamu nzuri kabisa kuwahi kutokea katika kiwanda cha sanaa Tanzania. Sina hakika kama bodi ya Filamu Tanzania imeipitisha; kama wameipitisha ama wakiipitisha kama ilivyo kaa tayari kuitazama huku ukichukua tahadhari hasa uko na watu gani wakati unaangalia. Narudia tena kuwapongeza waandaaji kwa kazi nzuri. Hongereni sana.

Imeandikwa na
Malle Hanzi
0715076444
©2016

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents