Habari

Video: Filamu ya ‘Kiumeni’ iliyogharimu tsh milioni 50 kuonyeshwa kwa mara ya kwanza Jumatano hii Dar

Filamu ya Kitanzania inayosubiriwa kwa hamu, Kiumeni ya muigizaji na mtayarishaji wa filamu nchini, Ernest Napoleon itaonyeshwa kwa mara ya kwanza Jumatano hii Mlimani City Century Cinemax Jijini Dar es salaam.

Waigizaji wa filamu hiyo Ernest Napoleon (kushoto), Idris Sultan pamoja Antu Mandoza wakizungumza na waandishi wa habari Jumatano hii Jijini Dar es salaam

Filamu hiyo ambayo imeandaliwa kwa kipindi cha miezi mitatu na kugharimu zaidi ya tsh milioni 50 imewakutanisha waigizaji kama Muhogo Mchungu, Irene Paul, Idris Sultan, Ernest Napoleon pamoja na waigizaji wengi wachanga ambao walionyesha uwezo mkubwa.

Akiongea na waandishi wa habari Jumatano hii akiwa katika ukumbi wa Century Cinemax, Mlimani City Jijini Dar es salaam muda mchache baada ya waandishi kuonyeshwa filamu hiyo, Ernest Napoleon alisema filamu hiyo ni filamu ambayo itawafanya watanzania na wapenzi wa filamu nchini kupenda filamu zao kutokana ubora wa filamu hiyo.

“Kesho ni siku ambayo filamu yetu ya Kiumeni ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu itaonyeshwa kwa mara ya kwanza hapa Century Cinemax, Mlimani City. Kuanzia saa 6 jioni watu wataanza kupata picha za red carpet na saa 8 usiku filamu itaanza kuonyeshwa. Kwahiyo ni filamu ambayo tumeigizia uswazi kabisa, stori ni nzuri hata baadhi ya vijana ambao wameonekana tumewatoa huko huko mtaani na wengine hawakuwai hata kuigiza lakini wameonyesha uwezo mkubwa,” alisema Napoleon.

Aliongeza,”Filamu ni nzuri na ina ubora ndio maana hata hapa Century Cinemax tunaendelea kupewa nafasi, mara ya kwanza wakati tunazindua filamu ya Going Bongo tulipewa siku tatu za kuionyesha lakini baada ya kuona watu wanapenda wakatuongezea wiki na baadaye wiki mbili kwa maana ikaonyeshwa kwa wiki mbili. Filamu ya Kiumeni ilivyowafuata tu wakaniambia itaonyeshwa kwa wiki mbili. Kwa hiyo hiyo ni dalili nzuri kwa filamu zetu kwa sababu tulianza hawatuamini mpaka sasa wanatuamini,”

Pia alisema baada ya uzinduzi wa Tanzania ataenda kufanya uzinduzi nchini Kenya na baada ya hapo itaachiwa kwenye mfumo wa DVD ili iweze kupatikana nchini kote.

Kwa upande wa Idris Sultan ambaye amecheza kwenye filamu hiyo kama muuza dawa za kulevya, amesema filamu hiyo itawafanya mashabiki wake kujua kwamba anaweza kufanya vitu vingi tofauti na washabiki wake wanavyodhani kwamba ni mchekeshaji pekee.

“Kwenye filamu hii nimecheza kama muuza dawa za kulevya na tayari nilishawai kufungwa kwajili ya biashara hii, ukiniangalia utagundua huyo siyo yule Idris wakuchekesha ambaye amezoeleka kuonekana. Huku nipo serious kabisa na tena ni mfanyabiasha hatari, na kusema kweli nimeweza kubeba uhusika kama nilivyotakiwa kwahiyo mashabiki watapata kitu tofauti kutoka kwangu,” alisema Idris Sultan.

Kwa upande wa muigizaji mchanga mwanadada Antu Mandoza ambaye alionyesha uwezo mkubwa kwenye filamu hiyo, amesema anamshukuru Ernest Napoleon pamoja na team yake kwa kumuamini na kumpatia nafasi kubwa ndani ya filamu hiyo.

“Kusema kweli namshukuru Mungu sana kwa hapa nilipofikia kwa sababu kazi ilienda vizuri na kesho inaenda mtaani nikiwa kama msanii mchanga. Naamini hii kazi itanitangaza kwa sababu ni kazi ambayo naamni nimeonyesha kitu cha utofauti katika uigizaji,” alisema Antu Mandoza.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents