Habari

Exclusive: January Makamba alijibu swali la kama ana mpango wa kugombea Urais mwaka 2015 (Video)

Tukiwa tumebakiza mwaka mmoja kabla ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania kufanyika mwaka 2015, tayari majina kadhaa ya wanasiasa yamekuwa yakitajwa kwenye orodha ya wale wanaoonekana kuwa na nia ya kugombea Urais.

Miongoni mwa majina hayo ni pamoja na la Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba. Tumezungumza na January kwenye mahojiano naye maalum na miongoni mwa kile tulichotaka kufahamu ni pamoja na kama kweli ana nia ya kugombea Urais 2015.

January anasema:

Kumekuwa na maono na maneno lakini kubwa kumekuwa na ushawishi kutoka kwa makundi mbalimbali. Mwanzo walianza vijana ambao wamekuwa wanakuja hapa, baadaye wakaanza baadhi ya wazee, watu kutoka kwenye vyuo, wanataaluma. Mwanzoni sikuwa nachukulia kwa uzito sana, nilijua labda ni mashabiki. Kila mwanasiasa ana mashabiki na kila mwanasiasa hakosi mtu ambaye anaweza kumwambia kwamba ‘unafaa kuwa rais’ ndio nature ya siasa. Kwahiyo ukiwa unajua, unasikiliza tu.

Lakini sasa kwa kadri muda ulivyokuwa unaenda watu wamezidi kuwa wengi na wengi ni watu ambao ni wazito na wengine ni watu ambao wanatoa sababu nzito. Sasa katika kuamua.. kwasababu nafasi hiyo ni kubwa sana. Katika kuamua kwamba aidha unagombea au haugombei kuna mambo kadhaa lazima uyatafakari.

Lazima utafakari kwanza kazi yenyewe hiyo unaiweza? Ambayo baadhi ya watu wanadhani unaiweza, waliokuja kukushawishi. Na kwamba Je wanaokushawishi hawakushawishi kwa maslahi yao? Na katika kutafakari kama unaiweza lazima wewe mwenyewe ufanye tafakuri ujifahamu. Lakini uzungumze na watu wengine vilevile, uangalie wengine wanaotaka kuomba nafasi hiyo, uangalie changamoto zilizopo kwenye nchi kwa sasa, utakafakari aina ya uongozi unaohitajika kwaajili ya changamoto hizo.

Utazame uzoefu na uwezo wako na exposure uliyopata, ukomavu wako wa siasa, uwezo wako wa kuwaunganisha Watanzania.
La pili lazima utafakari kwamba wananchi sasa wanataka nini. Wananchi sasa wanataka mabadiliko makubwa ya namna mambo yanavyoendeshwa, wanataka mabadiliko makubwa kwenye maisha yao. Yote hayo yataletwa kutokana na fikra na dira ambayo viongozi wataitoa.

Sasa Je una uwezo wa kutengeneza dira hiyo ya mabadiliko makubwa ambayo watanzania wanayataka? Kwahiyo nayo lazima uitafakari kwa kina na inahitaji muda. Kwasababu unapoomba nafasi hii, hauiombi kwaajili yako, na familia yako, na wapambe wako. Hauombi cheo, unaomba uongozi wa juu ambao ni muhimu sana kwenye kutoa dira na muelekeo wa nchi.
Kwahiyo kwenye kuamua ni lazima utafakari kwa kina ni mambo gani hasa makubwa ambayo yanaweza kuibadilisha nchi yetu na yakatoa matumaini mapya kwa watu.

La tatu ni kwamba kazi ya kujenga nchi bado haijaisha, wenzetu waliianza, Mwalimu Nyerere na Marais waliofuatia. Kujenga nchi kwa maana ya kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja na kujenga nchi kwa maana nchi ipate maendeleo. Na utaona kwamba kipindi cha mwaka, miaka miwili iliyopita imeanza kujitokeza nyufa nyufa ya Watanzania kuanza kubaguana katika misingi mbalimbali.

Je wewe unapoomba hii nafasi, unaweza kupata support ya Watanzania kwenye kila kona ya nchi hii na wakakuona kama kiongozi unayeweza kuwaunganisha?

Kwahiyo unapoamua kugombea, ni lazima ugombea wako na uongozi wako utoe ishara ya umoja wa Watanzania. Je kimataifa.. kwasababu nchi yetu ina heshima duniani, na heshima hiyo imejengwa kwa miaka mingi. Kwasababu kiongozi wa nchi ni ishara ya nchi duniani. Je kwa uongozi wako na Urais wako utatoa ishara njema ya Tanzania duniani? Utaendelea kuifanya nchi yetu ipate marafiki zaidi? Diplomasia ya nchi yetu iendelea kung’ara na heshima ya nchi iendelee kuwepo.

Kwahiyo pamoja na kwamba ushawishi umekuwepo, kwangu mimi katika kipindi hiki, nimekuwa nikichukua muda mrefu sana kutafakari yote hayo na itakapofika wakati tutatamka kwamba tuko tayari.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents