Bongo MovieBongo5 MakalaBurudani

Exclusive Interview: Mzee Chillo, aelezea alikokuwa kabla ya uigizaji wa filamu, mafanikio na changamoto

Ahmed Olotu maarufu kama Mzee Chillo ni muigizaji maarufu wa filamu Tanzania ambaye hadi sasa ameshaigiza zaidi ya filamu 100. Kutokana na uwezo wake mkubwa, Mzee Chillo anachukuliwa kama miongoni mwa waigizaji wa filamu Tanzania bora kabisa kuwahi kutokea.

Mzee Chillo

Tumezungumza naye kutaka kufahamu mengi kuhusiana na yeye.

Wengi wanakuchukulia kama muigizaji bora kabisa wa kiume japo umeanza kuonekana kwenye filamu tayari ukiwa na umri mkubwa, unaweza kutueleza ulikuwa wapi kabla ya kuingia kwenye filamu na kama fani ya uigizaji ulikuwa nayo tangu zamani?

Hii ni fani niliyokuwa nayo tangu zamani lakini sio kwamba nilikuwa nafanya fani miaka yote.

Ulikuwa unafanya nini awali?

Mimi niliwahi kuwa mfanyakazi wa serikali, nimefanya kazi kwenye balozi, nimefanya biashara, yote hayo nimeyafanya, baadaye sasa ndio nikarudi kwenye sanaa.

Ni nani aliyekushawishi sasa uingie kwenye kiwanda cha filamu Tanzania?

Ni Lucy Komba, sijui alijuaje, halafu kuna Tuesday Kihangala.

Uigizaji ndio kitu pekee unachokifanya kwa sasa, au kuna shughuli zingine za kiofisi unazoendelea nazo pia?

Hapana, sasa hivi nafanya filamu peke yake.

Unasifika sana kwa namna unavyoubeba uhusika kwenye filamu unazoigiza, unaweza kufanya hivyo hasa ukizingatia kuwa watu wengi wanadai kuwa filamu nyingi za Kibongo hazina uhalisia?

Usema ukweli ni kujituma halafu kitu chenyewe ni mtu kukijali, sio part-time ni full-time na kujaribu kufanya mazoezi, sio kukurupuka tu kufanya filamu. Kupita kwenye makundi mbalimbali kufanya mazoezi, kulipenda hilo jambo na kujituma bila ya kuona kwamba nimechoka. Na pia kumsikiliza mwelekezaji wako kwamba anataka ufanye nini ujitahidi kufanya kile alichosema ufanye.

Wengi wanaamini kuwa kigezo kikubwa kwenye filamu za Tanzania ni uzuri na ndio maana kuna wasichana wengi warembo ambao hawana background yoyote au uwezo wa kuigiza wameingia kwenye filamu kwasababu tu ni warembo, unaizungumziaje kasumba hii?

Script au filamu haiendani na urembo wa msichana. Kinachoendana pale ni cast kwamba unataka msichana wa namna gani katika story yako au katika movie yako, sio suala la uzuri au sura ya mtu. Sura ya mtu kwenye cast inaendana kwamba unataka awe na tabia gani. Awe mjeuri, awe mpole, awe mkali, awe changundoa, awe ananyanyaswa. Sio suala la uzuri, hili sio shindano la urembo.

Kuna mapungufu gani kwenye filamu za Tanzania?

Mapungufu ni kwamba kuna watu ambao huwa wanakurupuka tu kwamba wanataka wafanye filamu bila kujipanga vizuri kifedha, kujipanga vizuri kwa location, kujipanga vizuri kwa cast kwamba namhitaji nani na nani. Kingine ni kwamba kuna ambao wameingia kwenye tasnia ya filamu kwa nia ya kuonesha sura au kwa bahati mbaya wasichana wanaotaka kuonesha sehemu zao ambazo hazitakiwi kuonekana kwenye public na bahati mbaya hata wale watayarishaji wanaridhika na jambo hilo kwamba wasichana waoneshe utamaduni ambao si wa kwetu.

Halafu kuna tatizo la matumizi labda ya jela, matumizi ya kituo cha polisi, uniform za polisi au za jeshi, bado hatujapata ushirikiano na bado kuna wasiwasi kwamba watu wanaweza kuzitumia vibaya hizo uniform au kutumia zana nakadhalika. Na pia kuna ambao kwasababu amefanya filamu nyingi anaona kwamba anaweza kuwa director bila kujifunza.

Soko la filamu likoje? Linakuridhisha?

Kwenye malipo haliniridhishi. Malipo hayaendani na kazi tunayoifanya.

Kuna dalili za mapungufu haya kuja kupungua ama kuisha kabisa na pia waigizaji wakawa wanalipwa vizuri kama wanavyostahili?

Dalili zipo kama kweli tukiwa na umoja ambao una nguvu. Ninaamini serikali itakuwa inamulika upande huu wa umoja wenye nguvu ambao upande mmoja utakuwa na meno na upande wa pili watakuwa wanaangalia maslahi ya waigizaji. La pili ni kwamba sasa hivi naona watu hata mataifa ya nje wanajaribu kuja kufanya filamu hapa, kufungua ofisi zao nakadhalika. Sasa hiyo pia itatokea mchujo kwamba wao bila shaka hawatotaka watu ambao hawatabeba uhalisia kamili lazima watataka watu wanaofahamu kufanya kazi.

Umeshawahi kutafutwa na watayarishaji wa filamu wa nje ya Tanzania?

Nimewahi kufanya movie mbili ambazo zipo Marekani moja ikiwa ni Bongoland 2 na nyingine ni Going Bongo.

Umewahi kufanya filamu zako mwenyewe?

Hapana sijafanya filamu yangu mwenyewe.

Haufikirii kuanzisha kampuni yako kama wasanii wengi wengi wanavyofanya?

Sitaki kukurupuka. Suala la kuanzisha kampuni linataka uwezo mkubwa, linataka fedha kubwa na support kubwa. Nimeona hata wale waliojaribu, haijachukua muda wameanguka au wengine wanakuwa kampuni ni jina lakini mmiliki ni mtu mwingine. Inabidi umtii yule mtu mwingine hata kama hata kama anataka ufanye kitu kingine ambacho ni kinyume cha film industry.

Mwisho, juzi tumeona jinsi ambavyo bodi ya filamu imeizuia kutoka filamu ya Dr Cheni ‘Nataka Kuolewa’ ambayo imesema inaenda kinyume na desturi za Tanzania na pia hata Ray naye aliwahi kukutana na pingamizi katika filamu yake ya Sister Marry, unahisi ni sawa kwa bodi hii kufanya hivi ama wakati mwingine inawaonea na kuwasababishia hasara pia?

Tuwape nafasi Film Board wafanye kazi na tuwape ushirikiano badala ya kuwafanya wao ni maadui. Wao wako pale kwa niaba ya serikali na kwa niaba yetu sisi sote. Naamini tukifanya ushirikiano nao vizuri, tutafika mahali pazuri. Mtoto anapoomba ruhusa ya kwenda sehemu fulani na mzazi akimwambia hapana asikasirike ‘kwanini ameniambia nisiende kwenye ile party, baba hanipendi’ hapana ana maana yake. Na hivyo hivyo kwenye bodi ya filamu, wanapoangalia kitu ambacho wanaona kina kasoro, tusiwe na ile impression kwamba ‘movie yangu ni nzuri sana hawa kwanini wanaikosoa!’ hapana tuwasikilize.

Tuwasikilize na tufanye kile wanachokisema. Na mara nyingi masahihisho yanakuwa madogo sana. Lakini sasa kwasababu sisi tumejichukulia kuwa ni maprofesheno, tunaweza kufanya movie nzuri, ‘huyu mwingine anayenikosoa ni nani?’ Kumbe yule yupo kwaajili yetu sisi kuona kwamba kweli hii ni filamu inayoweza kuonwa na familia zote. Tuwape ushirikiano naamini watafanya kazi nzuri.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents