Siasa

CUF yamtega Kikwete

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kutekeleza moja kati ya mambo mawili, kama masharti ya kutaka kurejesha imani ya chama hicho kwake

na George Maziku




CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kutekeleza moja kati ya mambo mawili, kama masharti ya kutaka kurejesha imani ya chama hicho kwake, kama mhimili wa mazungumzo ya kusaka suluhu ya mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Masharti hayo yalitolewa jana na Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, wakati akiwahutubia wanachama na wapenzi wa CUF wa Mkoa wa Dar es Salaam, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.

Akianisha sharti la kwanza, Profesa Lipumba alisema iwapo Rais Kikwete ana nia ya dhati ya kutaka kuyaokoa mazungumzo hayo, basi afanye kila lililo katika uwezo wake kuhakikisha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinasaini makubaliano yaliyofikiwa na kamati ya mazungumzo bila mabadiliko yoyote.

Aidha, iwapo ataona hilo haliwezekani, Profesa Lipumba alimtaka Rais Kikwete kuwakutanisha Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, ili walizungumze suala la utawala Zanzibar na kuhitimisha makubaliano hayo.

Profesa Lipumba alisema kuwa, masharti hayo si magumu kwa Rais Kikwete kuyatekeleza, hasa ikizingatiwa kuwa chama chake kimeshabainisha kuwa, kimsingi kimeyakubali maafikiano ya kamati ya mazungumzo.

“Iwapo kweli (Rais Kikwete) anataka tumuamini tena kwamba dhamira yake katika kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar iko pale pale, basi CUF iko tayari kumsaidia kwa kukubaliana na mojawapo kati ya njia hizi mbili,” alisema Profesa Lipumba huku akishangiliwa na wafuasi waliokuwa wakimsikiliza.

“Nimeamua kufanya hivi baada ya kumsikiliza mwenyekiti mwenzangu wa upande wa pili, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Jakaya Kikwete, akitoa maelezo kuhusiana na mazungumzo hayo katika ukumbi huu huu wa Diamond Jubilee tarehe 2 Aprili, mwaka huu, lakini kwa bahati mbaya maelezo hayo yakiwa yamejaa upotoshaji na ubabaishaji wa hali ya juu,” alisema.

Alisema kuwa, hadi hivi sasa chama chake kimeonyesha ukomavu wa kisiasa kwa kukubali kukaa pamoja na CCM kutafuta ufumbuzi wa suala hilo, lakini inaonekana kuwa wenzao wana lengo jingine.

Aliongeza kuwa, iwapo Rais Kikwete atashindwa kuyaokoa mazungumzo hayo, CUF isihusishwe kwa namna yoyote na jambo lolote litakalotokea.

Alisisitiza msimamo wa awali wa chama chake wa kupinga pendekezo lililotolewa na NEC ya CCM, kutaka suala la muafaka liamuliwe na wananchi kwa njia ya kura ya maoni, na kulielezea pendekezo hilo kuwa ni kiini macho, na ucheleweshaji wa kutekelezwa kwa makubalaino yaliyofikiwa.

Wakati huo huo, katika kuonyesha dhamira yake ya kuirudisha ajenda hiyo kwa wananchi, mwenyekiti huyo wa CUF alitangaza rasmi mpango wa chama chake kufanya maandamano ya amani nchi nzima kushinikiza watawala kuharakisha kusainiwa kwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya vyama vya CCM na CUF kuhusu mgogoro wa kisiasa Zanzibar.

Alisema kuwa maandamano hayo yataanza Jumamosi wiki hii visiwani Zanzibar, na yataongozwa na yeye mwenyewe.

“Natangaza rasmi kuanzisha maandamano ya amani ya wananchi wa Tanzania kuwashinikiza watawala kuharakisha utiwaji saini muafaka, tutaanzia Zanzibar Jumamosi na tutaendelea katika mikoa mingine ya Tanzania, maandamano ni haki ya wananchi na hatuhitaji kibali kuandamana,” alisema Profesa Lipumba.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa wa vyama vya upinzani vilivyoko katika ushirikiano na CUF, ambavyo ni CHADEMA, TLP na NCCR-Mageuzi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema kuwa hakuna haja ya kukaa na kuzungumza na CCM kwani viongozi wa chama hicho si waadilifu na hawaaminiki.

“Kuzungumza na CCM ni kupoteza muda bure. Hawa watu si waadilifu na hawaaminiki. Hawa dawa yao ni nguvu ya umma tu, nawapongeza viongozi wa CUF kwa kukataa kuendelea na mazungumzo, sisi tuko pamoja nao na tutaungana pamoja katika maandamano ya Jumamosi,” alisema Mbowe.


 


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents