Bongo5 MakalaBurudani

Counting the Cost: Pengo la B12, Adam Mchomvu na DJ Fetty kwenye XXL

Kama wewe ni msikilizaji mzuri wa Clouds FM hususan kipindi cha XXL utakuwa umehisi mabadiliko makubwa ya sauti ulizozizoea kuzisikia. Sauti ya B12, Adam Mchomvu na DJ Fetty hazipo tena.

clouds

Na sasa inasikika sauti maarufu sana kwenye matangazo ya burudani ya kituo hicho ambayo wakati mwingine inaweza kukuchanganya na ukadhani ni B12. Huyo ni Raymond Mshana ambaye kwa sasa amekabidhiwa kipindi hicho kigumu na maarufu zaidi kwenye uwanja wa vipindi vya mchana vyenye mrengo wa burudani.

Kwa Ray kukabidhiwa kipindi hicho ni sawa na mlinda mlango kwenye mpira wa miguu anapotakiwa kuzuia magoli, kukaba washambuliaji na yeye mwenyewe kufunga magoli. Kwa hali ya kawaida kwenye mpira wa miguu haiwezekani. Mtangazaji huyo anatakiwa kuziba pengo la watu watatu ambao kila mmoja ni supastaa mwenye mashabiki wake, DJ Fetty ambaye kicheko chake kitamu hakisikiki tena, Adam ambaye ujinga wake wenye maana huzivunja mbavu za wasikilizaji wengi na B12 ambaye kwa wengi anakubalika kama mtangazaji bora zaidi wa vipindi vya mchana.

Kwa wiki kadhaa kumekuwepo na tetesi za watangazaji hawa kusimamishwa kazi. Alianza DJ Fetty ambaye hata hivyo sababu yake ya kusimamishwa kazi haijathibitishwa kama ni sawa na ile iliyowaponza Adam, B12 na Diva ambaye gazeti la Risasi limeandika kuwa naye amesimamishwa kazi.

Gazeti hilo limeandika:

Habari za chini kwa chini kutoka kwa chanzo chetu zinasema kuwa uongozi wa Clouds umefikia hatua hiyo baada ya kuchoshwa na tabia ya utovu wa nidhamu wa watangazaji hao.

Hata hivyo, madai ya mitaani yanasema kwamba watangazaji hao wamepigwa chini kwa kosa la kukacha sherehe za maadhimisho ya miaka 14 ya Clouds FM,yaliyofanyika hivi karibuni katika Viwanja vya Mwembeyanga, Temeke, Dar.
Risasi Mchanganyiko lilimvutia waya Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba na kumwuliza juu ya ishu hiyo ambapo alikiri.

“Ni kweli tumefikia uamuzi wa kuwasimamisha B 12, Diva na Mchomvu baada ya kukiuka baadhi ya makubaliano baina yao na ofisi hivyo kusababisha usumbufu mkubwa ambao ulitulazimu kuingia gharama ambazo hazikutarajiwa.

“Hatutakuwa nao kwa muda usiojulikana ingawa watu wengi wamekuwa wakinihoji juu ya hilo lakini watachotakiwa kuelewa ni kwamba hakuna ofisi isiyokuwa na sheria na taratibu za kuongoza watu wake, sasa hao wamevunja taratibu zetu,” alisema Ruge bila kufafanua zaidi.

Alipoulizwa ni taratibu zipi watangazaji hao walizovunja alisema: “Nashindwa kueleza kosa la kila mmoja ila naomba nieleweke kuwa hao watangazaji kwa sasa tumewasimamisha kwa muda usiojulikana wakati tukifikiria cha kufanya. Muhimu hapo ni kwamba wamekwenda kinyume na tulivyokubaliana.”

Binafsi Bongo5 haijathibitisha taarifa hizi na inafuatilia kwa ukaribu kupata kauli kutoka kwenye uongozi wa kampuni hiyo. Kuna tetesi ambazo bado hazijathibishwa pia kuwa DJ Fetty ameacha kabisa kazi kwenye kituo hicho cha redio kuendelea na mambo mengine.

Hata hivyo taarifa ninayoifahamu ni kuwa Diva alikuwa amelazwa na alifanyiwa upasuaji. Siku mbili zilizopita aliandika kwenye Instagram:

Thank You Guys wote ambao in one way or other mmekuwa mkinipigia… bbm me, whatsapp me and sms me nawengine DM nyingi just to wish me get well soon……. i am forever thankful, wote mliokuja niona at the hospital … wote mliokuwa mnajali… I really Appreciate. Promise I’ll get well soon and will get over the Fibroid Surgery and Will Be back normal … and Yes love all My fans… without you nisingekuwa mie….. love you all. kiss kiss from ya girl Diva … Special Thanks kwa bongo fleva Artist dah… aisee mnanipenda… wote mliokuwa mnanicheck nawashukuru sana!. Mungu awabariki.”

8f29525e581811e39b501254994b6a4e_8

Alhamis hii Diva amepost picha kwenye Instagram na kuandika: Clouds. ….. Diva……. tunajenga barabara. To my fans….. siwezi kuwaacha kwenye mataar. Love you guys this much …… take it easy. I see you. For life @bdozen @babajonii_online.”

XXL ndicho kipindi kinachoathirika zaidi kwa sasa na ingawa Ray ni mtangazaji mzuri, hata afanye nini hawezi kuziba nguvu ya watangazaji watatu ambao kwa wengi hao ni miongoni mwa watangazaji bora wa vipindi vya burudani nchini.

“XXL now days ina mtangazaji anatangaza kama habari za vifo za radio Tanzania…n I was like WTF????by the way am not listening to it anymore,” ameandika mtu mmoja kwenye picha ya Adam aliyoiweka Instagram.

“Kumfukuza Mchomvu clouds ni sawa na kuhamishia ikulu tandale kwa tumbo,” ameandika mwingine.

Hata hivyo kupitia Instagram, Adam amekanusha tetesi kuwa hayupo tena kwenye kituo hicho kama wengi wanavyodai.

“Kwa waliozusha #MROPOKO wa siku @divathebawse @bdozen kupigwa chini #MJENGONI #CLOUDS #stillnumberone #XXLforLIFEstyle swallow tht,” aliandika Adam kwenye picha ya mtu aliyesinzia huku mdomo wake mkubwa ukiwa wazi.

Kama walivyoondoka Masoud Kipanya na Fina Mango kwenye Power Breakfast na Gadner G Habash kwenye Jahazi na vipindi hivyo kuyumba kwa muda mrefu kabla havijakaa sawa kutokana na wasikilizaji kukubali matokeo na kuamua tu kuwazoea hosts wapya, ndivyo XXL na Ala za Roho vinavyoyumba. Bila kusahau pia kipindi cha Leo Tena ambacho nacho hakina sauti zilizozoeleka za Dina Marios na Gea Habib waliopo kwenye likizo ya uzazi. Clouds FM imepoteza kwa muda majembe muhimu kwenye lineup yake.

Katika kipindi ambacho watangazaji hao wamesimamishwa, vipindi vyao vinapoteza wasikilizaji wengi na kama wakiwekwa benchi kwa muda mrefu, vipindi vya muda kama wao kwenye redio zingine vitavutia wasikilizaji wapya ambao wakati mwingine hukamatika kabisa.

Hata hivyo tukubali ukweli kuwa, hata kama mtangazaji akiwa muhimu vipi kwenye kituo cha redio, pale anapokiuka sheria muhimu za kazi ni muhimu kupewa onyo, kupigwa faini, kusimamishwa na hata kufukuzwa kazi kabisa kama ilivyo kwenye kazi zingine.

Clouds FM si kituo pekee kinachozikosa kwa muda sauti zilizozoeleka kwenye maskio ya wasikiliza wengi kwakuwa East Africa Radio pia inazikosa sauti za watangazaji wake Steve Kabuye aliyekuwa akitangaza kipindi cha The Cruise ambaye aliamua kuacha kazi na Michael Omwony aka Flava aliyekuwa akifanya kipindi cha East Africa Drive.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents