Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki ilimhukumu mtumishi wa ndani kwenda jela miaka miwili, baada ya kupatikana na hatia ya kumuibia bosi wake mali ya Sh. 500,000.
Binti huyo mwenye ujauzito wa miezi minane, Hanifa Omari (18), alifikia hatua hiyo baada ya kunyimwa mshahara wa miezi mitatu.
Hukumu dhidi yake ilisomwa na Hakimu Mkazi John Msafiri wa mahakama hiyo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Msafiri alisema kutokana na mshtakiwa kukiri kuiba mali ya bosi wake, mshtakiwa atatumikia kifungo hicho ili iwe fundisho.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alikuwa mtumishi wa ndani wa Omari Jafari, lakini siku ya tukio aliiba fedha taslimu, simu za mkononi na nguo mbalimbali, vyote vikiwa na thamani ya fedha hizo.
Katika utetezi wake, mshtakiwa alidai alikuwa anamdai bosi wake mshahara wake Sh. 90,000 za miezi mitatu, ambapo kila mwezi Sh. 30,000.