| Madanguro, Gesti bubu ni tatizo Dar |
|
|
|
| Wednesday, 25 June 2008 | |
|
Ukaguzi uliofanywa na kamati ya kudhibiti ukimwi ya halmashauri ya manispaa ya kinondoni imetoa ripoti ya ukaguzi wake inayodaiwa kubaini kuwa bado kuna tatizo lwingi wa madanguro, grosari pamoja na gesti bubu ambazo hufanywa baa kinyume na taratibu. Hayo yalisemwa alipouwa akiwakilisha taarifa ya utekelezaji wa kamati kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu katika Mkutano wa Baraza la madiwani wa manispaa hiyo. Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni Julian Bujugo, aliyataja maeneo walipobaini madanguro hayo kuwa ni Manzese na Makumbusho. Akitoa mchango katika Kamati hiyo, Diwani wa Manzese Elias Manumbu, alisema pamoja na kuwapo kwa madanguro pia katika eneo lake hasa Uwanja wa Fisi linaongoza kwa kuwapo nyumba za wageni bubu ambazo gharama zake ni za chini sana jambo linalochangia maambukizi ya ugonjwa huo. “Ukiletewa data za manispaa hii utaona kuwa Tandale ndio inayoongoza kwa maambukizi ya Ukimwi, gesti bubu ziko nyingi sana na chumba ni Sh 200 hadi 300, tunaomba tusaidiwe,” alisema diwani huyo. Naye Diwani wa Kimara, Mahamudu Mringo alikemea vitendo vya wamiliki wa grosari kugeuza biashara hiyo na kuifanya baa bila kujali leseni zao, sheria wala mamlaka zinazowasimamia. “Biashara ya vileo iko kisheria na mdhibiti mkuu ni sisi pamoja na polisi, tusije tukawaruhusu hawa wafanyabiashara ya vileo watuendeshe, sheria zipo tuwadhibiti,” alisema. Pamoja na hayo alisema katika barabara ya Morogoro eneo la Kimara kumekuwa kukitokea ajali takribani kila wiki na kuua. “Jamani naomba nilitangaze eneo lile kama hifadhi ya wanyama kama ilivyo Mikumi ili tuwekewe matuta vinginevyo tutakwisha,” alisema. Akijibu baadhi ya hoja, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Afya na Elimu, Omar Kimbau, alisema suala la gesti linajulikana na tayari manispaa imeanza kulifanyia kazi kwa kuwapeleka maofisa wake ili wadhibiti biashara hiyo. Awali kabla ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji Kamati ya Fedha na Uongozi kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, Meya wa Manispaa hiyo, Salum Londa, alimtaka Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), kuacha kutumia siasa na kuharibu fikra za watu kuhusiana na manispaa ya Kinondoni. Alisema hivi karibuni Mbunge huyo wakati akihutubia Dar es Salaam alizungumza mambo mengi kuhusiana na manispaa hiyo ikiwamo kumshangaa Londa kuwa kwa nini anatoa taarifa ya hesabu badala ya watendaji ama mkurugenzi.
|
| < Prev | Next > |
|---|







