| TIN Namba kwa kila mfanyakazi. |
|
|
|
| Wednesday, 25 June 2008 | |
|
Wizara ya Fedha na Uchumi imesema inaendelea na maandalizi ya kuwasajili watu wote wanaofanya kazi katika sekta rasmi ili wawe na namba ya utambulisho ya mlipa kodi (TIN) zoezi ambalo linatarajia kukamilika hivi punde. Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Jeremia Sumari aliliambia Bunge jana kuwa maandalizi hayo yatakapokamilika wafanyakazi wote watakuwa na namba za utambulisho. Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhonga Ruhwanya (Chadema) ambaye alitaka kufahamu sababu ya mfanyakazi anayekatwa kodi kutopewa TIN namba yake itakayomtambulisha kuwa ni mlipa kodi. Sumari alisema lengo la kuanzisha TIN namba ni kwa ajili ya kuwatambua walipa kodi nchini pamoja na shughuli zao. Alisema namba ya mlipa kodi hutolewa kwa mujibu wa sheria ya kodi. Alisema kwa sasa mfanyakazi hana TIN namba kwa vile mwajiri wake ndiye aliyepewa namba hiyo. Wakati huohuo, Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe alisema jana kuwa serikali imechukua hatua za awali za kuanza ujenzi wa jengo la makao makuu ya mahakama na mpaka sasa tayari kiwanja kimepatikana karibu na Hoteli ya Holiday Inn, Dar es Salaam. Aliongeza kuwa fedha zimepatikana chini ya mpango wa maboresho ya sekta ya sheria na ujenzi wa jengo la kudumu la mahakama ya rufani utaanza wakati wowote kuanzia sasa. Mahakama kama mhimili mwingine wa nchi kwa sasa haina jengo zuri ikilinganishwa na mihimili mingine yaani Serikali na Bunge, alisema. Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Bububu, Masolwa Cosmas Masolwa (CCM), aliyetaka kujua mikakati ya serikali ya kujenga jengo linalolingana na hadhi ya mhimili wa mahakama.
|
| < Prev | Next > |
|---|







