SwahiliEnglish
            Lost Password?    Click here to register

Pinda ahofu mafua ya ndege nchini PDF Print E-mail
Wednesday, 30 April 2008
Waziri Mkuu Pinda
 
 
na Hellen Ngoromera


SERIKALI imewataka wananchi kuchukua tahadhari ya kukabiliana na ugonjwa wa mafua makali ya ndege nchini, kwa sababu ugonjwa huo kwa sasa umeshaingia Juba, kusini mwa Sudan, ambayo inapakana na Uganda na Kenya.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alibainisha hayo jana wakati akizindua Mpango wa Tahadhari na Udhibiti wa Ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege, uliofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

“Tishio la kuingia na kuenea kwa ugonjwa huu nchini mwetu ni kubwa kuliko tulivyodhani siku za nyuma na hii inatokana na kama nilivyosema na ukweli ni kwamba ugonjwa umeingia kusini mwa Sudan.

“Hali hii inaashiria kuwa ugonjwa huu unaenea kwa kasi kubwa. Kutokana na ukweli huu, sasa hofu imezikumba nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa huenda ukafika katika nchi hizi wakati wowote,” alisema Pinda.

Kwa mujibu wa waziri mkuu, kutokana na sababu hizo, kuna haja ya kuchukua tahadhari, ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kuzuia kuingia na kusambaa.

Alisema kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Wanyama Ulimwenguni (OIE), ugonjwa huo ulianzia Hong Kong mwaka 1997 na kusambaa katika nchi 61, zikiwemo 11 za Bara la Afrika, ambazo ni Benin, Burkina Faso, Cameroon, Cote d’voire, Djibouti, Ghana, Niger, Nigeria, Misri Sudan na Togo.

Taarifa za Shirika la Afya Duniani za Januari mwaka huu zinaeleza kwamba, ugonjwa huo husambazwa kwa binadamu hususan wale wanaohudumia wanyama wa kufugwa kama kuku.

Takwimu za shirika hilo zinaonyesha kuwa mwezi huo, jumla ya watu 348 walikuwa wameambukizwa ugonjwa huo, ingawa kati ya wagonjwa hao 216 walipoteza maisha kwa maradhi hayo.

Kwa upande wake Waziri Mkuu aliongeza kuwa, baada ya kutambua kuwa tishio la ugonjwa huo kwa sasa ni kubwa, serikali imeweka ugonjwa huo kama mojawapo ya majanga ya taifa.

Aliongeza kuwa katika hilo, serikali imeamua kuchukua hatua madhubuti za tahadhari za kujiandaa kukabiliana na ugonjwa huo endapo utaibuka nchini.

Alisema pamoja na juhudi za serikali, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu mkubwa wa wataalamu wa ugani na wadau wengine pamoja na mahitaji ya soko lililosababisha mwamko wa ufugaji wa kuku.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa wapo wataalamu wa ugani wa mifugo 2,581 ikilinganishwa na mahitaji ya wataalamu 16,050 kulingana na lengo la serikali la kuwa na mtaalamu wa ugani wa mifugo katika kila kata na kijiji.

“Hali hii ya ukosefu wa wataalamu inahatarisha sana jitihada za serikali kupambana na ugonjwa huu, ili kukidhi mahitaji hayo serikali itajaza nafasi hizo kwa awamu. Inatarajiwa kwa mwaka wa fedha 2007/08 serikali kuajiri wataalamu wa ugani 1,250 wanaotokana na wahitimu katika soko la ajira,” alisema.

Alisema mahitaji ya mazao ya kuku yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na kuwapo walaji wengi wa nyama na mayai yatokanayo na kuku wa asili na kisasa, na kuwa kwa hapa nchini kuna kuku wa asili milioni 34 wanaofugwa, milioni 20 wa kisasa, bata milioni 1.2, bata mzinga 900,000 na kanga 400,000.

Kwa upande wa uzalishaji wa kuku wa mayai umeendelea kuongezeka pia, kwani kwa mwaka 2005/06 pekee kulikuwa na vifaranga milioni 26.8 vya kuku wa biashara, ambavyo vilizalishwa nchini na vingine milioni 2.1 vilivyoagizwa kutoka nje.

Alisema mayai ya kutotoa vifaranga milioni 8.4 yaliagizwa kutoka nje na kuwa uzalishaji wa mayai uliongezeka kutoka bilioni 1.8 mwaka 2005/06 huku ulaji wa mayai kwa mtu kwa mwaka ukiongezeka kwa asilimia 20.7 kutoka 53 hadi 64.

“Takwimu hizi zinaashiria umuhimu wa kuku nchini…kama hatutakuwa makini kuzuia na kuwakinga kuku hawa na maradhi kama mafua ya ndege, wananchi wengi wataathirika kiuchumi,” alisema Waziri Mkuu Pinda.

Naye Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, John Magufuli, alisema kwa sasa bado ugonjwa huo haujafika Tanzania. Aliongeza kuwa ili kuudhibiti, serikali imepiga marufuku uingizwaji wa nyama na ndege wanaosafirishwa kutoka nje.

Pamoja na mambo mengine, alisema kwa sasa serikali imeanzisha maabara ya kisasa yenye uwezo wa kuchunguza kuhusu kuwapo kwa ugonjwa huo.

Alisema maabara hiyo iliyopo Temeke imeshazifanyia uchunguzi zaidi ya sampo 3,000 za nyama na ndege, ili kutambua uwepo wa ugonjwa huo.

“Kwa sasa hatuna wasiwasi kwani tuna maabara ya kisasa yenye uwezo wa kuchunguza uwepo wa ugonjwa huo ambayo tumepewa msaada na Serikali ya Marekani, siku za nyuma tulikuwa tukipeleka sampo zetu nje ya nchi lakini sasa wataalamu tunao na wanafanya kazi kiuhakika,” alisema Magufuli.

Alisema pamoja na mambo mengine, wataendelea kuchukua tahadhari mbalimbali za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo. Aliwataka wananchi kuendelea kula nyama.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa kutoka Ubalozi wa Marekani nchini, Dk. Stefan Wiktor, alisema wametenga dola milioni mbili za Marekani, ili kudhibiti ugonjwa huo nchini.

 

Source: Tanzania Daima

Comments
Search
Only registered users can write comments!

3.26 Copyright (C) 2008 Compojoom.com / Copyright (C) 2007 Alain Georgette / Copyright (C) 2006 Frantisek Hliva. All rights reserved."

Tag it:
Delicious
Furl it!
Spurl
NewsVine
Reddit
YahooMyWeb
Digg
blogmarks
feedmelinks
co.mments
 
< Prev   Next >
Total Members
total 21215 registered
female 5270 female
male 15865 male
month 20 new this month
New: kelly31
Who's Online Now
We have 37 guests online and 11 members online
swejacky Amiry said salehe moody x Tito Chamillionaire Danielita Jozeedaking kindgirl Tukwa kelly31
Bongo5 Chat Zone 2.0
Total of members in the chatroom:
2006-2007 © Copyright Bongo5.com