|
Rostam sasa akimbilia mahakamani
|
|
|
|
|
Monday, 28 April 2008
|
|
Na Mwandishi Wa Majira
BAADA ya kupigwa 'stop' na Bunge la Jamhuri ya Muungano kuwasilisha hoja yake binafsi kuhusu mkataba wa kuzalisha umeme kati ya kampuni hewa ya kuzalisha Umeme ya Richmond na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mbunge wa Igunga, Bw. Rostam Aziz (CCM) sasa ameamua kwenda mahakamani akiibuka na madai mengine.
Katika kile kinachoweza kuonekana kama 'hasira ya kupigwa stop' Bungeni, Bw. Rostam sasa ameyageukia magazeti anayodai yamemchafulia jina kwa kumwandika vibaya na kufungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania akidai fidia ya mabilioni ya fedha.
Katika Mkutano wa 11 wa Bunge uliomalizika wiki iliyopita mjini Dodoma, Mbunge huyo, alijikuta akigonga mwamba katika mkakati wake wa kuwasilisha hoja binafsi ambayo kwa upande mwingine ilionekana kama namna ya kutaka kutoa utetezi wake na mpango wa kuibua yaliyofichika katika sakata la Richmond lililomng'oa madarakani aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa 'akisindikizwa' na aliyekuwa Waziri wa Madini na Nishati Bw. Mustafa Karamagi na mwenzo wa Afrika Mashariki, Dkt. Ibarahim Msabaha.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, Bw. Rostam alipigwa 'stop' kutokana na kwamba hoja aliyotaka kuwasilisha tayari ilishazungumzwa ndani ya Bunge na kwamba maelezo yake hayakuwa na tofauti na barua aliyomwandikia Spika.
Bw. Rostam amefungua kesi ya madai namba 53 katika Mahakama Kuu ya Tanzania akilishtaki gazeti la Mwanahalisi na kutaka kulipwa jumla ya sh. bilioni tatu kwa maelezo kwamba gazeti hilo limemchafulia jina kwa kuandika habari zisizo za kweli dhidi yake jambo lililomvunjia heshima ndani ya jamii.
Katika kesi hiyo, anamshitaki Mhariri wa gazeti hilo, Mkurugenzi Mtendaji na Meneja wa Pritench Company Limited na Standard Printers Limited wachapishaji wa gazeti hilo.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosainiwa na Wakili wake, Bw. K.M Fungamtama, amedai kuwa katika toleo namba 084 la Februari 13 hadi 19 mwaka huu gazeti hilo katika ukurasa wake wa kwanza, pili na tatu lilichapisha habari ikiambatana na picha ya Mbunge huyo yenye kichwa kisemacho "Richmond ya Rostam Aziz-Ikulu", 'Ndiye aliyeileta nchini', 'Lowassa alimuingiza.'
Pia amedai katika toleo namba 085 na Februari 20 hadi 26 mwaka huu kulikuwa na habari yenye kichwa kisemacho "Kikwete alimtosa Lowassa" katika habari hiyo amelalamikia maneno yaliyosema; "Aidha mfanyabiashara na Mbunge wa Igunga Bw. Rostam Aziz aliingia mjini Dodoma Jumanne 5 Februari, siku moja kabla ya Ripoti ya Tume Kuwasilishwa akitokea nje ya nchi kwa lengo la Kuzima harufu ya jinamizi la Richmond."
Katika ukurasa wa pili wa toleo namba 087 la Machi 5 hadi 11 kulikuwa na Habari iliyosema "Richmond yasambaratisha habari Corporation," pia katika toleo namba 093 la Apili 16 hadi 22 mwaka huu lilikuwa na habari isemayo " Rostam Taabani" ikieleza nia ya mbunge huyo kutaka kujiuzulu baada ya kuzuiwa kuwasilisha hoja yake Bungeni.
Mbunge huyo amedai habari hizo si za kweli na zimemwathiri kwa njia moja ama nyingine kutokana na nafasi yake kama mfanyabishara na mwanasiasa anayeheshimika ndani ya jamii kwani zimemchafulia jina lake.
Alisema habari hizo zimemfanya aonekane mtu asiye na maadili, fisadi asiyefaa kuwa kiongozi na anayejihusisha 'dili' haramu
Ameiomba mahakama kulipwa fedha hizo sambamba na gazeti hilo kuomba radhi kupitia kurasa zake za mbele baada ya uamuzi kutolewa.
Source: Majira
|