Habari

BoT kumekucha

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
Joachimu Liyumba na Meneja Mradi wa Benki hiyo, Deograthias Kweka, jana
walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
Joachimu Liyumba na Meneja Mradi wa Benki hiyo, Deograthias Kweka, jana
walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za
kuisababishia hasara Serikali ya zaidi ya Sh 221 bilioni.

 

 

Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani saa 9:00 alasiri huku Liyumba akisomewa mashitaka matatu na Kweka shitaka moja.

 

 

Akisoma hati ya mashitaka wakili wa serikali, John Rwabuhanga
alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Hadija Msongo kuwa kati ya mwaka 2001 na
2006, Liyumba akiwa mwajiriwa wa serikali, alitumia vibaya madaraka
yake kuidhinisha malipo ya ujenzi wa majengo pacha bila idhini ya Bodi
ya Wakurugenzi wa BoT na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya
Sh221,197,229,200.95.

 

 

Kweka alidaiwa kuwa, kati ya mwaka 2001 na 2006, akiwa Meneja
Mradi wa BoT, aliisababishia hasara serikali ya zaidi ya Sh221 bilioni.

 

 

Hata hivyo, waashitakiwa hao walikana mashitaka na upande wa mashitaka
ulidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

 

 

Hakimu Msongo alitaja masharti matano ya dhamana ambayo ni kila
mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali na
barua zao za utambulisho zitoke kwa waajiri wao.

 

 

Pia washitakiwa hao wanatakiwa kila mmoja kutoa nusu ya fedha
zilizoibwa kama dhamana, ambayo ni zaidi ya Sh50 bilioni au hati ya
mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

 

 

Masharti mengine ya dhamana ni kuwasilisha hati zao za kusafiria,
kutosafiri nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila kuwa na kibali cha
mahakama na kuripoti katika ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) saa 2:00 asubuhi kila Ijumaa.

 

 

Baada ya kutolewa masharti hayo mmoja wa mawakili wanaomtetea Liyumba,
Alexander Kyaruzi alisimama na kuieleza mahakama kuwa wanazo hati za
mali kwa ajili ya dhamana kwa mshitakiwa wa kwanza.

 

 

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Fredrick Manyanda aliiomba mahakama
wapewe muda ili wazihakiki hati hizo ili kujua kama ni halali na kupata
uhakika wa thamani ya mali iliyotajwa katika hati hizo.

 

 

Hakimu Msongo alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuahirisha
kesi hiyo hadi Februari 10 mwaka huu itakapotajwa tena. Na washitakiwa
walirudishwa rumande.

 

 

Taarifa ya ukaguzi ya BoT ya mwaka 2005, minara hiyo ambayo ujenzi wake
uligubikwa na utata, iliigharimu benki hiyo Sh500 bilioni.

 

 

Utata katika suala hilo upo katika gharamaa za ujenzi wake na kampumi iliyopewa zabuni kufanya kazi hiyo.

 

Habari zilizopatikana nje ya mahakama zinasema kuwa hadi sasa Sh600
bilioni, zimetumika katika ujenzi wa majengo pacha ya BoT yaliyoko
jijini Dar es salaam jengo la Benki Kuu Zanzibar la Gulioni.

 

 

Katika taarifa yake ya mwaka wa fedha 2005/06, BoT ilisema hadi kufikia
Juni 2006, miradi hiyo ilikwishatengewa Sh430 bilioni. Katika mwaka wa
fedha 2004/05, gharama za ujenzi wa mradi huo zilikadiriwa kuwa
Sh238.59 bilioni, lakini hadi sasa gharama hizo zimeongezeka zaidi ya
mara mbili ya makadirio ya awali.

 

 

Jengo la PPF, lililopo katika makutano ya mtaa wa Ohio na Pamba,
linalofanana kidogo na moja ya minara hiyo, liligharimu Sh19 bilioni
hadi lilipozinduliwa rMachi 20, mwaka 2001 na Rais mstaafu Benjamini
Mkapa.

 

 

Jengo linalokadiriwa kugharimu fedha nyingi zaidi hapa nchini ni Umoja
House, lilipo katika Mtaa wa Mirambo, jijini Dar es Salaam
linalohifadhi ofisi za balozi tatu za Uingereza, Ujerumani, Uholanzi na
Umoja wa Ulaya ambalo lilijengwa kwa Sh23 bilioni mwaka 2003.

 

 

Hii ina maanisha kuwa maghorofa pacha ya Benki Kuu yanaigharimu
Serikali karibu mara 20 ya gharama za Umoja House na mara 30 ya gharama
za jengo la PPF.

 

 

Mara baada ya kuanza kazi, Gavana wa sasa wa BoT, Profesa Beno Ndulu
alisema atafuatilia suala hili ili kubaini kama kuna ubadhilifu katika
mradi wa kujenga majengo hayo pacha na lile la Zanzibar.

 

 

Matumizi mabaya ya fedha za umma katika ujenzi wa majengo hayo, ni
miongozi wa tuhuma zilizofichuliwa na kambi ya upinzani sambamba na
ufisadi wa mabilioni katika Akaunti ya Madeni Nje (EPA), ambao
ulisababisha aliyekuwa gavana wa BoT Daudi Balali kufukuzwa kazi pamoja
na baadhi ya watuhumiwa wakiwemo watumishi wa benki hiyo, kufikishwa
mahakamani kwa kuisababisha hasara serikali.

Source: Nora Damian – Mwananchi

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents