Habari

Benki ya Dunia yanufaisha shule 120 zinazofanya vizuri kitaaluma

Benki ya Dunia imetoa ufadhili wa elimu kwa shule za msingi 120 zinazofanya vizuri kitaaluma kutokana na mpango uliopo wa ‘Lipa Kulingana na Matokeo’ ambao umeangalia matokeo ya darasa la nne na la saba ya mtihani wa Taifa kwa shule hizo zilizopo mkoa wa Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema hayo jijini Dar es Salaam alipokuwa akimkaribisha Rais wa benki hiyo, Dk Jim Yong Kim alipotembelea mojawapo wa shule hizo za msingi ambayo ni Zanaki katika Manispaa ya Ilala.

“Benki ya Dunia inasaidia sana elimu, shule nyingi zimejengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na vyuo vikuu kwenye miundombinu pamoja na rasilimali watu,” alieleza.

Aidha Ndalichako alisema wamewekeana makubaliano na benki hiyo ya kuendelea kujenga madarasa ambapo dola za Marekani milioni 75 (shilingi bilioni 157.5 ) zimetengwa na benki hiyo kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri zaidi ya kujifunzia pamoja na elimu maalumu.

Kwa upande wake, Rais wa Benki ya Dunia anayezulu nchini kwa ziara ya siku tatu, Dk Kim alisema anafurahishwa na matokeo ya shule hiyo ya Zanaki, hivyo ameahidi kuendelea kuisaidia sambamba na kuitaka serikali kuwekeza zaidi kwenye elimu.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents