Bongo5 MakalaBurudani

Ben Pol, Walter, Linex, Ditto, Barnaba, Angel, Linah, Recho washiriki kwenye album ya Valentine’s Day, sikiliza vionjo hapa

Valentine’s Day inakuja tena kwa surprise zake kibao kwenye burudani. Wakati ambapo wapendanao wakijiandaa kuliongezea mbolea penzi lao, THT imeamua kuwasaidia kufikisha ujumbe mtamu kwa njia ya nyimbo. Jumba hilo la vipaji Tanzania, litaachia album mahsusi kwaajili ya siku hiyo muhimu ya Wapendanao duniani itakayoshirikisha wasanii wote wenye sauti tamu zitakazowabembeleza wapendanao wanapokuwa pamoja katika siku yao.

IMG-20140208-WA0002

Album hiyo yenye jumla ya nyimbo 15, inaitwa With Love.. Vol 2.

Hebu fikiria Lameck Ditto anapoimba hit single ya Linex ‘Moyo wa Subira’ na kujaribu kumgalaza msanii huyo wa Kigoma kwa kumpa tution ya namna ambavyo alitakuwa kuuimba wimbo huo. Hata hivyo kwenye album hiyo pia, Linex naye analipiza kisasi kwa Ditto kwa kuuimba wimbo wake ‘Wapo’ na yeye pia akiiitumia sauti yake ya kipekee kubandika msumari wa moto kwa kuupitisha wimbo huo njia tofauti kabisa ambazo Ditto hakuweza kuipitisha single yake ya kwanza hasa pale alipoamua kuongeza vionjo vya Kiha (kabila).

Nani kamfunika mwenzie? Swali hilo linaweza kupata jibu zuri zaidi kutoka kwa mtu atakayekuwa na kopi ya album hii.
Unapata ladha gani pale wimbo wa Ditto ‘Tushukuru Kwa Yote’ unapoimbwa kwa sauti ya kuvutia ya kike? Khadija ameuchukua wimbo huo na kuuimba vizuri kiasi ambacho unaweza kushawishika na kuitafuta original version ya Ditto na ukataka ulinganishe kutaka kujua ipi ni kali zaidi!!

Lakini wakati ambapo wengi wanaamini kuwa ni wasanii wachache wa kike nchini wanaweza kumrudisha darasani Recho kwa kuziimba tena nyimbo zake, vipi nikisema kuwa Vummy ameweza kufanya hivyo? Muimbaji huyo wa ‘Utanikumbuka’ ameuimba wimbo wa Recho ‘Upepo’ kwa ustadi mkubwa kiasi ambacho hata kama Recho akisikia, ni lazima aunganishe mikono yake yote miwili na kumpigia makofi ya kusimama (standing ovation) muimbaji huyo kwa kazi nzuri aliyoifanya.
Bahati mbaya, Recho hajaweza kulipiza kisasi kwa Vummy japo kisasi chake kimelipwa na muimbaji mwingine wa THT aitwaye Sundy ambaye haoni hatari kumgalagaza dada yake Vummy kwa kuukamua vyema wimbo wake ‘Utanikumbuka’.

Nao Ben Pol na Recho wameamua kuwakaba koo, Amini na Linah kwa kuuchukua wimbo wao ‘Mtima Wange’ na kuutuliza kidogo kuuweka uendane na Valentine’s Day. Ni wimbo mwingine mzuri wa kuusikiliza.

Amini anaendelea kuingizwa darasani kwenye album hii pale ambapo mshindi wa EBSS 2012, Walter Chilambo anapouchukua wimbo wake ‘Ni Wewe’ na kuuimba kama vile aliutunga yeye. Hapa Amini ni lazima moyo umwende mbio kidogo na pengine kupata hasira ya kutaka kuuchukua wimbo wowote wa Walter na kulipiza kisasi.

Lakini mambo yanamgeukia pia Linah pale ambapo Lulu anapoukamata wimbo wake ‘Atatamani’ na kuuimba kama vile waliutunga pamoja.

Linah hakubali kuabishwa na mdogo wake na anaamua kumuonesha Lulu kuwa yeye bado ni dada yake tu kwa kuuchukua wimbo wa Pipi uitwao ‘First Time’ na kuthibitisha kuwa bado ataendelea kuwepo kwenye orodha ya wasanii wa kike wenye sauti tamu kuwahi kutokea nchini. Utampenda zaidi Linah ukimsikia kwenye wimbo huu.

Raha zaidi inakuja pale ambapo Barnaba anajaribu kushindana na sauti ya kike ya Recho kwa kuimba wimbo wake ‘Nashukuru Umerudi’. Humu Barnaba anajikuta akipita zaidi na ‘Falsetto’ ili kuifikia ‘peak’ ya sauti ya Recho kwenye wimbo huo na hakuna shaka kuwa amefanikiwa kuuimba vyema wimbo huu na pengine kuwaonjesha upande mwingine wa sauti yake. Saxophone inayosikika katika sehemu kadhaa kwenye wimbo, inaongeza utamu zaidi wa kuusikiliza.

Pamoja na kuuimba kwa ustadi wimbo huu, Barnaba habaki na amani tena pale ambapo Mwasiti anapomkaba koo kwa kuuimba wimbo wake Sorry. Mwasiti kamrudisha kwenye darasa la muziki Barnaba? Huenda wewe ukawa na jibu zuri zaidi.
Pressure inazidi kupanda kwa Barnaba kwakuwa Ally Nipishe naye anaangusha ‘bombshell’ yake kwa kuuchukua wimbo wake ‘Tulizana’ ambao anauimba kwa ustadi mkubwa. Kama ‘theme’ ya album hii ilivyo, anautuliza kidogo na hivyo kuupa ladha tamu ya kusikilizika zaidi.

Naye mmoja wa wakilishi wa Tanzania kwenye shindano la Tusker Project Fame msimu wa 6, Angella Karashani anaonesha kuwa majaji wa shindano hilo walimuonea tu pale anapouchukua wimbo uitwao ‘Zinda’ na kuupa ladha tamu usiyoweza kuiepuka kupenya kwenye matundu ya masikio yako na melody yake kusambaa kwenye ubongo wako na kutengeneza makazi kwa muda.

Album hii imetayarishwa kwenye studio za Surround Sounds chini ya maproducer Ema The Boy, Nash Designer na Tuddy Thomas. Kama utaikosa, utakuwa umekosa kitu kizuri kwenye masikio yako mwaka huu.

Sikiliza vionjo hapa:

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents