Burudani

BASATA latoa maelezo ya kwanini limemfungia Shilole mwaka mmoja kutojihusisha na muziki

Baraza la Sanaa la taifa, BASATA, limemfungia Shilole kutojihusisha na masuala ya muziki ndani na nje ya Tanzania kwa mwaka mmoja.

11330616_296972493806688_1211325526_n

BASATA limempa barua Shilole jana yenye taarifa za kufungiwa kwake.

Adhabu hiyo imetolewa kufuatia tukio la msanii huyo kupigwa picha za aibu wakati akitumbuiza nchini Ubelgiji miezi kadhaa iliyopita.

Hii ni taarifa rasmi ya BASATA:

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kama msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini limemfungia msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya Zuena Mohamed kwa jina la kisanii Shilole kufanya shughuli za sanaa nchini kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe 24/07/2015 hadi tarehe 24/07/2016.

Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 09/05/2015 akiwa katika onyesho lake la Muziki nchini Ubelgiji alikiuka maadili ya kazi ya sanaa mbele ya hadhira ya wapenda sanaa za Tanzania na hivyo akadhalilisha utu wake na jamii ya Kitanzania kimaadili.

Pia itakumbukwa kwamba mnamo mwezi Oktoba, 2013 BASATA ilimuonya na akakiri kwa kuomba msamaha kwa tabia yake ya kucheza bila kuzingatia utu na maadili awapo jukwaani.

BASATA ilimpa nafasi ya kutoa maelezo yake kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kitendo chake cha kudhalilisha maadili, utu na sanaa ya Tanzania lakini akakaidi kutoa maelezo. Hivyo basi BASATA imejiridhisha kwamba alikiuka maadili ya kazi ya sanaa kwenye onesho lake la huko Ubelgiji makusudi na amekiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za uendeshaji wa Sanaa.

Hivyo basi kutokana na ukiukwaji huo wa sheria na kanuni za uendeshaji wa shughuli za sanaa nchini, Baraza la Sanaa la Taifa chini ya Kanuni ya 30(1)(d) ya G.N 322 ya 2005 limemsimamisha kujishughulisha na kazi za Sanaa nchini kwa muda wa Mwaka Mmoja tokea tarehe 24/07/2015.

Hivyo haruhusiwi kufanya au kushiriki kwa namna yoyote ile shughuli yoyote ya onesho la sanaa nchini au nje ya nchi. Iwapo atafanya kinyume cha hayo kutapelekea kupewa adhabu zaidi ikiwa ni pamoja na yeyote yule utakaye shirikiana naye.

Ni matumaini ya Baraza la Sanaa la Taifa kwamba wasanii na waandaaji wa shughuli za sanaa wataendelea kutambua umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Shilole aliwahi kusema kuwa hata yeye hakupenda kile kilichotokea jukwaani wakati akitumbuiza nchini humo kwa sababu ilikuwa bahati mbaya na hakudhamiria kukaa uchi kama wengi wanavyosema.

Shishi ambaye ni mama wa watoto wawili alisema kuwa nguo mpya aliyoivaa siku hiyo ndio ilimponza kwasababu hakuwa ameifanyia majaribio ya kutumbuiza akiwa ameivaa.

“Kiukweli kwasababu hili jambo limetokea inatakiwa nguo ninapoinunua niwe naifanyia training kwanza kabla ya kwenda jukwaani, kwahiyo kwasababu ile nguo ilikuwa mpya kwangu na sikuweza kuijua vizuri […] yaani hii nguo nimeikuta huku huku, nguo imekuja kunitokea bahati mbaya wakati niko kwenye performance, ilitatuka wakati niko kwenye motion,” Shishi aliiambia Clouds FM.

Aliongeza kuwa alisikitishwa na mtu aliyempiga picha hizo na kuamua kuzisambaza mtandaoni bila kujua kuwa itamuumiza yeye kama mwanamke.

“Nasisitiza tena sikudhamiria na wala sikupenda hiyo kitu itokee, ila nasikitika kwamba kama mimi mwanamke yule mtu aliyenipiga picha na kudhamiria kuziweka kwenye mitandao alikuwa na maana gani, hakufikiria mimi nitaunmia kiasi gani au mashabiki wangu wataumia kiasi gani? Ni mtu mbaya mwenye roho mbaya sijui nimuiteje huyo mtu aliyefanya hivyo, sio mtu mzuri.”

Unachukuliaje adhabu hiyo? Ni halali ama Shilole ameonewa?

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents