Habari

Balozi za Tanzania nje zaanza kupunguza wafanyakazi

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema imeanza kupunguza maofisa walioko katika balozi na kuweka wapya ili kupanua wigo wa uwakilishi na kubana matumizi.

719a4429

Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Aziz Mlima wakati akizungumzia mambo mbalimbali yanayofanywa na wizara hiyo kwenye kipindi cha TUNATEKELEZA na kituo cha runinga cha TBC 1.

Mlima alisema kuwa ili kupanua wigo wa balozi katika kutangaza utalii nchini, waliamua kuwaondoa maofisa walioko kwenye balozi 35 na ofisi mbili za uwakilishi zilizopo nchi mbalimbali ili kupeleka watu wenye uwezo wa kutumia nafasi hiyo vyema.

“Tumeamua kubana matumizi hususani kupunguza mahitaji yasiyo ya lazima, ikiwemo watumishi. Tunaangalia mchango wa maofisa waliokuwepo kwenye balozi zetu kama anahitajika mmoja au la,’’ alisema Mlima.

“Miongoni mwa majukumu ya balozi zetu ni pamoja na kutangaza fursa za utalii na vivutio vilivyopo nchini kwetu ili kuongeza watalii kutoka nje kuja hapa. Kwa hivyo, tumeona ni vyema kuwabadilisha waliokuwepo na kuweka watu wapya ambao watakuwa wachache wenye uwezo wa kufanya kazi hii kikamilifu.”

Aliongeza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuongeza uwakilishi mzuri katika balozi hizo na kuboresha mazingira ya maofisa wao walioko nje kwa kutumia rasilimali chache zilizopo.

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents